*Awasisitiza wananchi wasikubali kugawanywa
MUUNGANO
wa Tanganyika na Zanzibar ambao tarehe 26 Aprili 2020 utafikisha miaka
56, umekuwa daraja lisilotetereka la kuwafikisha Watanzania katika azma
yao ya kupata maendeleo, amani na ustawi.
Halikadhalika,
Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015 – 2020, nayo
inazielekeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutekeleza majukumu yake
kikamilifu kwa lengo la kuhakikisha Muungano unakuwa imara zaidi na
kwamba amani na utulivu vinaendelea kuwepo nchini.
Katika
kutekeleza maelekezo hayo ya Ilani, Januari 17 hadi 20 mwaka huu Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa alifanya ziara katika visiwa vya Unguja na Pemba
ikiwa ni miongoni mwa harakati kuimarisha muungano na ushirikiano kati
ya SMZ na SMT.
Akizungumza
na wananchi kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu aliwakumbusha kuhusu
kuenzi jitihada za waasisi wa Taifa hili yaani Hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume za
kutuunganisha kupitia muungano.
Alionya
kuwa wananchi wasikubali kuhadaiwa na watu wachache wenye kupinga
muungano kwani kwa kufanya hivyo watahatarisha amani ya nchi
inayowafanya watembee kifua mbele na kuwa kimbilio la mataifa mengine
yenye machafuko.
“Nchi
yetu imepata mafanikio makubwa ya kuwa na amani na utulivu tangu tupate
uhuru mwaka 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Imekuwa
kimbilio la watu wa Mataifa ya jirani kila wapatapo matatizo ya uvunjifu
wa amani katika nchi zao. Hivyo, hatunabudi kuienzi.”
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kuwahimiza Watanzania kushirikiana katika
kuulinda na kuutetea Muungano wa Tanzania pamoja na Mapinduzi Matukufu
ya Zanzibar na kamwe wasiruhusu watu kuingiza sumu ya kutaka kuwagawa.
“Watanzania
tusikubali mtu yeyote kutugawa kwa sababu sisi undugu wetu ni wa damu,
hivyo ni vema tukaendelea kuudumisha muungano wetu tusiruhusu watu
kuingiza sumu ya kutaka kutugawa kwani nia za watu hao hazina tija.”
Waziri
Mkuu aliongeza kuwa ni muhimu wananchi wakashirikiana na Serikali zote
mbili katika kuyaendeleza mafanikio yaliyopatikana kutokana na uwepo wa
muungano, kama uboreshwaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Pia
waendelee kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha uchumi katika pande
mbili za Muungano hususan katika kubuni na kutekeleza miradi ya
maendeleo kwa manuafaa ya wananchi wa pande zote. “Muungano una tija
kubwa kwetu sote tuulinde.”
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi
wanazoendelea kuzichukua katika kuboresha maendeleo ya wananchi wa pande
zote mbili.
Aidha, mbali na kuwahamasisha wananchi hao washirikiane katika kudumisha muungano, pia Waziri Mkuu aliwataka wananchi waendelee kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda tunu yetu ya amani kwani suala la ulinzi ni jukumu la kila mmoja.
“Mkuu
wa Mkoa wa Mjini Magharibi shirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama
kuimarisha ulinzi wa watalii na raia pamoja na mali zao ili kulinda
hadhi ya mji huu ambao unatembelewa na watalii wengi.”
Mkuu
wa mkoa na Viongozi wengine waimarishe umoja bila kujali itikadi za
kivyama. Waziri Mkuu alisifu viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa
walioshiriki kwenye ziara yake na kujionea wenyewe utekelezaji mzuri wa
Ilani ya CCM.
Kadhalika,
Waziri Mkuu akiwa kisiwani Pemba alikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba
za Polisi Mfikiwa, Chakechake na ujenzi wa nyumba za Polisi Finya.
Alisema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Akiwa
katika mradi wa nyumba zilizopo Mfikiwa Waziri Mkuu alikagua maendeleo
ya ujenzi wa nyumba sita za Askari Polisi zinazojengwa katika eneo hilo
lililopo wilayani Chakechake. Kati ya nyumba hizo sita, tano tayari
zimekamilika na zinatumika.
Nyumba
moja ipo kwenye hatua za kukamilika. Pia, Waziri Mkuu alishuhudia
matofali zaidi ya 32,000 katika eneo hilo la Mfikiwa ambayo yameshindwa
kutumika kutokana na changamoto ya fedha. Ujenzi wa nyumba moja
unakadiriwa kugharimu sh. milioni 35 iwapo zitajengwa kwa mfumo wa force account.
Kwa
upande wa nyumba zinazojengwa katika eneo la Finya, nako kumejengwa
nyumba tano za askari polisi ambazo licha ya kuwa zimeezekwa bado
hazijakamilika ili kuanza kutumiwa na askari hao.
Waziri
Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi Mhandisi Hamad Masauni kwa juhudi kubwa alizozifanya za kujitolea
vifaa vya ujenzi vilivyosaidia kuanza kutekelezwa kwa miradi hiyo.
Aliongeza
kuwa ni jukumu la wadau wengine nao kumuunga mkono ili kukamilisha
ujenzi wa nyumba zilizobaki na kujenga nyumba nyingine kwa kutumia
tofali zilizopo. Pia aliielekeza Wizara ya Mambo ya Ndani itenge fedha
kwenye bajeti ijayo ya 2020/2021 kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo;.
“Makamanda
wote wa Mikoa ya Polisi, wasipimwe na kuondolewa katika majukumu yao
kwa kigezo cha kushindwa kujenga nyumba za askari iwapo hawajapewa fungu
la kutekeleza miradi ya namna hiyo.
Katika hatua nyingine,viongozi
mbalimbali wa vyama vya upinzani wakiwemo wa vyama vya CUF, NRA, UPDP,
NSSR-MAGEUZI ambao walishiriki katika ziara ya Waziri Mkuu Zanzibar
waliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) pamoja
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kuimarisha huduma za
kijamii.
Viongozi
hao walisema kuwa wapo tayari kushirikiana na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli pamoja na Rais Dkt. Ali Mohammed Shein kwa sababu viongozi hao
wanafanya kazi kubwa na nzuri ya kuwahudumia wananchi. Pia waliahidi
kuulinda na kuutetea Muungano wa Tanzania na Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar.
“Maendeleo
hayana chama naunga mkono jitihada zinazofanywa na SMT na SMZ na
nimefurahia ziara ya Waziri Mkuu hapa kisiwani Unguja na ninamuunga
mkono Rais Dkt. Magufuli tumepata maendeleo ambayo hatukuyatarajia,”
alisema Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa NRA Bw. Khamis Faki katika mkutano
wa hadhara uliofanyika Shehia ya Bambi.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.