Sunday, January 19, 2020

SIMAMIENI ELIMU KWA WATOTO WA KIKE-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini wasimamie ipasavyo suala la elimu hususani kwa watoto wa kike na kuchukua hatua kwa watakaowakatisha masomo.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inawataka  watoto watoe taarifa za watu wanaotaka kuwakatisha masomo yao kwa viongozi  wa shehiya (vijiji) waliopo kwenye maeneo yao.

Alitoa agizo hilo jana jioni (Jumapili, Januari 19, 2020) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo cha Mafunzo ya Amali cha Daya kilichopo Mtambwe wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba.

Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuwalinda watoto wa kike lengo likiwa ni kuhakikisha wanamaliza masomo yao na hatimaye waweze kujikwamua wao pamoja na familia zao.

Alisema watoto wa kike wanatakiwa waheshimiwe na jamii kwa kuachwa waendelee na masomo yao bila ya usumbufu wowote na atakayebainika kukatisha masomo adhabu yake ni miaka 30 jela.

“Wanafunzi wa kike hakikisha mtu yeyote atakayekugusa, kukufuatilia nenda kamshtaki kwa kiongozi wa Shehiya husika. Vijana jihadharini na watoto wa shule ukikutwa naye jela miaka 30.”

Awali, akisoma taarifa za ujenzi wa chuo hicho, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bibi Madina Abdallah  alisema mpaka kukamilika kwake mradi huo utagharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 25.8 kati yake Dola milioni 23.4 zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) huku dola milioni 2.4 zikitolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alisema kwa mujibu wa mkataba wa mradi huo kazi ya ujenzi inajumuisha vituo viwili vya Mafunzo ya Amali ambavyo ni Makunduchi Unguja na Daya Pemba. Pia upanuzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Utalii Maruhubi na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume pamoja na ununuzi wa vifaa vya kufundishia.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.