Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya mwaka 1977, Ibara 52, jukumu la msingi la Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali katika sekta zote na Bungeni, Aidha Tangazo la Serikali Na. 144 Aprili 2016, lililofanyiwa mabadiliko tarehe 7 Oktoba 2017, limeaninsha majukumu mengine yanayosimamiwa na kuratibiwa na Ofisi hiyo.
Katika kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Ofisi hiyo yanaboreshwa, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko, ameamua kukutana na watumishi wa Ofisi hiyo katika makundi ya Maafisa, Watumishi wasio maafisa na Wakurugenzi kwa nyakati tofauti, ambapo leo tarehe 16 Februari 2020, ameanza kukutana na maafisa wote wa ofisi hiyo, Jijini Dodoma.
Akiongea na maafisa hao amewataka kuzingatia taratibu, sheria na kanuni za utumishi wa umma katika kuratibu na kusimamia shughuli za serikali. Aidha, amebainisha kuwa katika kuhakiksha utekelezaji unakuwa wa ufanisi ataandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa hao ili kuboresha utendaji kazi wao.
“Maafisa ndio watu wanaoanza kuchakata shughuli nyingi za utekelezaji, Taarifa za uratibu wa shughuli za serikali zikiandaliwa vizuri kabla ya kumfikia mkurugenzi matokeo yake huwa ni mazuri. Niwasihi jitumeni na ongezeni umakini katika kutekeleza majukumu, pia shirikishaneni, ili muweze kufanikiwa kutekeleza vyema jukumu la msingi la ofisi hii” Amesisitiza, Katibu Mkuu, Mwaluko.
Aidha,Katibu Mkuu mwaluko amesisitiza ushirikiano katika utendaji wa majukumu usizingatie kada tu, au maafisa ndani ya Idara na vitengo bali ushirikiano pia uwe kati ya Idara na vitengo, lengo ni kuhakikisha kila afisa anakuwa na uwezo wa kumudu kuratibu na kusimamia shughuli za serikali kwa ufanisi.
Majukumu ya msingi yanayosimamiwa kwa sasa na Ofisi hiyo ni:- Uratibu wa Shughuli za Serikali; Kuongoza Shughuli za Serikali Bungeni; Kuratibu Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa; Usimamizi na Uratibu wa Shughuli za Dharura na Maafa.
Aidha Ofisi hiyo ndiyo inaratibu, Shughuli za Uwezeshaji wananchi kiuchumi, na Maendeleo ya Sekta Binafsi, shughuli za Kuwezesha Maendeleo ya Uwekezaji na shughuli za Kuboresha mazingira ya Biashara nchini.
Shuguli nyingine zinazoratibiwa na kusimamiwa na ofisi hiyo ni Mapambano dhidi ya janga la UKMIWI na usimamizi wa athari zake kwa Tanzania Bara, Mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya , Shughuli za Uchaguzi nchini, Masuala ya Vyama vya Siasa na Ofisi hiyo ndiyo inayochapa rasmi nyaraka za Serikali.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.