Sunday, March 19, 2017

WAZIRI MKUU AMUWALIKISHA RAIS UZINDUZI WA JUKWAA LA UCHUMI AFRIKA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasili nchini Mauritius leo (Jumapili, Machi 19, 2017) kwa ajili ya kumuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli katika mkutano wa kuzindua Jukwaa la Uchumi Barani Afrika (AEP).

Kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Sir Seewoosagur Ramgoolam Waziri Mkuu amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritius Mheshimiwa Vishnu Lutchmeenaraidoo.

Uzinduzi wa jukwaa hilo unatarajiwa kufanyika kesho mjini Port Louis ambapo utawakutanisha viongozi wakuu wa nchi za Afrika, wanazuoni, wafanyabiashara pamoja na watu kutoka kwenye asasi mbalimbali za kiraia barani Afrika.

Pamoja na kuhudhuria mkutano huo, pia Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Mauritius litakalofanyika Machi 23, 2017.

Aidha, Waziri Mkuu mara baada ya kumaliza mkutano huo anatarajia kutembelea maeneo maalumu ya uwekezaji, viwanda vya sukari na nguo.

Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Dkt. Khalid Salum Mohammed na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa . Charles Mwijage pamoja na maofisa wengine wa Serikali.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.