Wednesday, April 4, 2018

HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2018/2019


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasilisha hotuba  kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya  fedha  za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2018/2019, bungeni mjini Dodoma Aprili 4, 2018.
1.           Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2018/2019.

2.           Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019.

3.           Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutokana na fikra na uongozi wao makini katika ujenzi wa Taifa letu. Ni dhahiri kuwa juhudi zao katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali, zinaleta manufaa makubwa kwa wananchi.

4.           Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tumewapata Waheshimiwa Wabunge wapya kutokana na chaguzi ndogo zilizofanyika. Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Mhe. Dkt. Godwin Mollel (Mbunge wa Jimbo la Siha) na Mhe. Maulid Mtulia (Mbunge wa Jimbo la Kinondoni) kwa kuchaguliwa na kisha kuapishwa na Bunge lako Tukufu ili waendelee kuwatumikia wananchi wa majimbo yao na Watanzania kwa ujumla. Ni matumaini yangu kuwa Bunge lako Tukufu litaendelea kuwapatia ushirikiano wa kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

5.           Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Bunge lako lilimpoteza aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mheshimiwa Leonidas T. Gama. Vilevile, baadhi ya waheshimiwa Wabunge na wananchi tunaowawakilisha walipata misiba ya ndugu, jamaa na marafiki. Aidha, kulitokea maafa na majanga ambayo yalisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Pia, kumekuwepo na ajali za barabarani ikiwemo ajali mbaya iliyotokea tarehe 24 Machi 2018 wilayani Mkuranga na kugharimu maisha ya Watanzania 26. Ninaomba Mwenyezi Mungu awajalie afya njema waliopata majeraha. Aidha, ninatoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki kwa misiba iliyotokea. Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu mahali pema peponi. Amina!

6.           Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutoa salamu za pole kwa Waheshimiwa Wabunge wenzetu waliopata majeraha mbalimbali kufuatia ajali ya gari tarehe 29 Machi 2018 walipokuwa wakitoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam. Wabunge hao ni Mheshimiwa Haji Ameir Haji (Mbunge wa Makunduchi), Mheshimiwa Khamis Ali Vuai (Mbunge wa Mkwajuni), Mheshimiwa Bhagwanji Maganlal Meisuria (Mbunge wa Chwaka), Mheshimiwa Makame Mashaka Foum (Mbunge wa Kijini) na Mheshimiwa Juma Othman Hija (Mbunge wa Tumbatu). Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie afya wenzetu hawa ili waweze tena kuungana nasi kutekeleza majukumu yao katika Bunge lako hili Tukufu.

7.           Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee, niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mhe. Mohammed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mhe. Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi; na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge. Aidha, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kuaminika na kuchaguliwa kuongoza Kamati hizo.

8.           Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, nawashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake kwa kutekeleza majukumu yao na kukamilisha kuandaa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2018/2019.

9.           Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee kabisa, napenda kumshukuru Mhe. Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu; Mhe. Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu; Mhe. Stella Alex Ikupa, Mbunge Viti Maalumu na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu; Makatibu Wakuu Bibi Maimuna K. Tarishi, Profesa Faustin R. Kamuzora, na Bwana Eric F. Shitindi, Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wafanyakazi wote kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

10.         Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo nchi marafiki, taasisi na mashirika ya kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda na kuiletea nchi maendeleo.

11.        Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kuniunga mkono na niwapongeze kwa kutekeleza shughuli za maendeleo jimboni kwa ufanisi, wakati mimi Mbunge wao nikitekeleza majukumu ya kusimamia utendaji wa Serikali. Kipekee, ninamshukuru mke wangu mpendwa, Mary na familia yangu kwa upendo wao, uvumilivu na maombi yao wakati wote ninapotekeleza majukumu yangu ya kitaifa. Nawashukuru sana.

MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI

 
12.        Mheshimiwa Naibu Spika, mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019 ni kuboresha utendaji wa Serikali na kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/2019. Aidha, Mpango na Bajeti umezingatia azma ya Serikali ya kufikia malengo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao umepangwa kuhitimishwa mwaka 2020/2021 ukiwa na dhima kuu ya “kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea ukuaji uchumi na maendeleo ya watu”. Vilevile, Mpango huu umezingatia azma ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 na utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 pamoja na utekelezaji wa hotuba yake wakati akizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015.

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO


13.        Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa tunaingia kwenye Bunge la tatu la bajeti kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hatuwezi kumsahau Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutimiza ndoto na matarajio ya Watanzania kwa kujenga nchi yenye uchumi imara. Katika kipindi hiki, tumeshuhudia mambo makubwa aliyoyafanya yakiwemo kujenga ari ya uzalendo kwa kuilinda na kuisemea nchi yetu bila woga; kudumisha amani, utulivu na mshikamano; kuimarisha ulinzi na usalama kwa kukomesha vitendo vya mauaji yaliyojitokeza Mwanza, Amboni (Tanga), Mkuranga, Kibiti, Rufiji (Pwani) pamoja na kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

14.        Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nyingine alizofanya ni kujenga nidhamu ndani ya utumishi wa umma na kukemea uzembe; kuendesha vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwenye taasisi za umma; kuanzisha mahakama ya rushwa na ufisadi; kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi zikiwemo za madini na maliasili. Aidha, amefufua Shirika la Ndege la Tanzania; ameanzisha ujenzi wa reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (SGR); ameendeleza ujenzi wa barabara zikiwemo barabara za juu (flyovers) na amenunua meli na vivuko. Kazi nyingine ni ujenzi wa vyanzo vipya vya umeme kama vile Stiegler’s Gorge; usambazaji umeme hadi vijijini na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania).

15.        Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine makubwa aliyoyafanya ni kuimarisha huduma za afya hususan upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaatiba katika vituo vya kutolea huduma za afya; kutoa elimumsingi bila malipo kwa watoto wa Kitanzania; ujenzi wa miradi ya maji; na kuimarisha bei za mazao ya kibiashara. Aidha, Mheshimiwa Rais ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali mjini Dodoma. Haya ni baadhi tu ya mambo aliyoyafanya na yatatolewa ufafanuzi wa kutosha kupitia wizara za kisekta.

HALI YA UCHUMI


16.         Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi. Viashiria vya kiuchumi vinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 6.8, kiwango ambacho kilikuwa juu zaidi ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Uchumi wa Kenya ulikuwa kwa asilimia 6.1, Rwanda asilimia 6.0, Uganda asilimia 5.5, Burundi asilimia 0.0 na Sudan Kusini asilimia hasi 6.3. Hata hivyo, takwimu za hivi karibuni kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha kwamba katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2017, pato halisi la Taifa lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.1 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2016. Shughuli zilizochangia ukuaji huo  kwa viwango vikubwa ni pamoja na uchimbaji wa madini na mawe asilimia 17.5; huduma za usambazaji maji safi na majitaka asilimia 16.7; uchukuzi na uhifadhi wa mizigo asilimia 16.6; habari na mawasiliano asilimia 14.7 na ujenzi asilimia 14.1.  Aidha, sekta ya kilimo, misitu na uvuvi ilikua kwa asilimia 3.6, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu mwaka 2010.

17.        Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia Desemba 2017, deni la Taifa lilikuwa Dola za Marekani milioni 25,419.6. Viashiria vyote vya deni vinaonesha kuwa deni linahimilika kwani, thamani ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 19.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya deni la nje kwa uuzaji wa bidhaa nje ni asilimia 81.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; na thamani ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 117.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 200. Kwa kuzingatia vigezo hivyo, bado tuna uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ili kugharamia shughuli za maendeleo. Kwa ujumla, viashiria vya kuimarika kwa uchumi, vinatoa mwelekeo mzuri wa kufikiwa kwa malengo yetu ya kuwa nchi ya kipato cha kati inayoongozwa na uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

SIASA


18.        Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka 26 sasa imepita tangu mfumo wa siasa wa vyama vingi uanzishwe nchini. Katika kipindi hicho tumeona ushiriki wa Watanzania katika siasa ukiendelea kuongezeka na uhuru wa kujiunga na vyama vya siasa kwa kuridhishwa na itikadi za vyama hivyo pia ukiongezeka. Ni vyema tukajenga utamaduni wa kuheshimu wananchi pale wanapoamua kujiunga na chama cha siasa watakachokipenda.  Jukumu letu kama viongozi wa siasa ni kunadi sera zetu kwa wananchi na kuhamasisha ujenzi wa demokrasia inayolenga kuleta maendeleo kwa wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote pamoja na kudumisha amani, utulivu, mshikamano na kujenga umoja wa kitaifa.

19.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, kumefanyika chaguzi ndogo za Wabunge katika majimbo matano na Madiwani katika kata 59 kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu mbalimbali. Chaguzi hizi zilisimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ufanisi. Katika chaguzi ndogo za ubunge zilizofanyika katika majimbo ya Songea Mjini, Singida Kaskazini, Longido, Kinondoni na Siha; Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishinda majimbo yote. Vilevile, katika uchaguzi wa Madiwani, CCM ilishinda katika kata 58 na CHADEMA ilishinda katika Kata moja. Nichukue nafasi hii kuvipongeza vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika chaguzi hizo na kipekee nakipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata ushindi mkubwa na wa kishindo katika maeneo mengi.

20.        Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Msajili imeendelea kuhakikisha kuwa demokrasia ya vyama vingi vya siasa inaimarika. Katika mwaka 2017/2018, Ofisi ya Msajili iliratibu kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa ambacho pamoja na kufanya uchaguzi wa Viongozi wa Kamati za Baraza hilo, kilijadili mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria Mpya ya Vyama vya Siasa na marekebisho ya Kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa. Vilevile, Ofisi ya Msajili inaendelea kukusanya maoni ya wadau kwa lengo la kuandaa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 pamoja na kanuni zake.

 

MUUNGANO


21.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, kumefanyika vikao mbalimbali vya kisekta vya ushirikiano kati ya Wizara za SMT na SMZ kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Muungano wetu. Baadhi ya changamoto hizo ni masuala ya fedha, biashara na ajira katika taasisi za Muungano. Katika kipindi hicho, viongozi na wataalamu wa pande mbili za Muungano walikutana kwa ajili ya kujadili hoja zinazohusu sekta za fedha, biashara, viwanda na uwekezaji, ujenzi na uchukuzi, maliasili na utalii.

SERIKALI KUHAMIA DODOMA


22.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza zoezi la kuhamishia shughuli za Serikali Kuu Dodoma. Tangu utekelezaji wa zoezi hilo uanze mwezi Septemba 2016, jumla ya watumishi wa umma 3,829 kutoka Wizara na taasisi mbalimbali wamehamia Dodoma katika awamu ya kwanza na ya pili, na awamu ya tatu inaendelea. Katika kufanikisha azma hii, Serikali inaboresha miundombinu ya barabara, reli, uwanja wa ndege, umeme, mifumo ya maji safi na maji taka, ofisi, makazi na kuimarisha huduma za elimu, afya, mawasiliano na michezo.

23.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kuijenga Dodoma kuwa mji bora na wa kisasa unaoendana na mahitaji na mifumo ya miji bora duniani. Ili kufikia azma hiyo, Serikali inashirikiana na wadau ikiwemo sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kuujenga Mji wa Dodoma. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye mara tu baada ya kuhamia Dodoma amezindua “Kampeni ya Kijanisha Dodoma” inayolenga kuifanya Dodoma kuwa ya kijani. Kampeni hiyo inahusisha kuendeleza, kutunza na kuhifadhi maeneo ya ukanda wa kijani.

24.        Mheshimiwa Naibu Spika, niupongeze Umoja wa Mataifa na mashirika yake kwa kufungua ofisi zake za muda mjini Dodoma mwezi Desemba 2017. Natoa wito kwa mashirika mengine ya kimataifa na mabalozi waige mfano huu wa kuhamishia ofisi zao Dodoma. Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Mashirika ya Kimataifa na wanadiplomasia katika kurahisisha maandalizi yao ya kuhamia Dodoma. Aidha, natoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuendelea kuwekeza Dodoma kwani kuna fursa nyingi za uwekezaji ikizingatiwa nafasi yake kijiografia inayosaidia mikoa yote hapa nchini kufikika kwa urahisi na haraka zaidi. Nichukue fursa hii kuipongeza Kamati inayoratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma inayosimamiwa na Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Bibi Maimuna K. Tarishi, Katibu Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge).

 

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI


25.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mipango mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi kujiletea maendeleo.  Moja ya jitihada zilizofanywa na Serikali ni kuanzisha mifuko ya uwezeshaji ambayo inatoa mikopo kupitia vikundi vya vijana, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na makundi mengine yenye mahitaji maalum.

26.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ulidhamini mikopo yenye thamani ya takriban shilingi bilioni 13 kwa SACCOS 58, VICOBA 172 na kampuni mbili. Aidha, Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali Wananchi umetoa mikopo ya Shilingi bilioni 62.8 kwa wajasiriamali 85,982. Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.4 kwa vikundi 5,169 katika Halmashauri 153. Mfuko wa Kilimo Kwanza ulitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 62.7 kwa miradi 189 katika wilaya 76.

27.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 783 ambapo vijana 840 kutoka Halmashauri mbalimbali walinufaika. Aidha, katika kipindi hicho, Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia asilimia 5 ya mapato yao ya ndani zilitenga shilingi bilioni 15 ikiwa ni mikopo ya masharti nafuu kwa vijana. Vilevile, Halmashauri 48 zilitenga ekari 217,882 kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali kwa vijana nchini. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

28.        Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Serikali inaratibu jumla ya mifuko na programu 31 za uwezeshaji ambazo usimamizi wake upo katika taasisi mbalimbali za Serikali na za binafsi. Kila mfuko au programu imeanzishwa kwa sheria yake au taratibu maalumu zinazosimamia utendaji wa mfuko husika. Serikali imeona kuna umuhimu wa kupunguza idadi ya mifuko kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji wake ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Hivyo, tumeanza kufanya mapitio ya utendaji wa mifuko hiyo kwa nia ya kuunganisha baadhi ya mifuko yenye majukumu yanayofanana. Hatua hiyo, itasaidia kuwa na mifuko michache yenye tija ambayo itaharakisha kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.

 

Ukuzaji Ujuzi


29.        Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kukuza ujuzi wa nguvukazi tuliyonayo ni miongoni mwa ajenda muhimu ya kisera katika kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi. Serikali inatoa msukumo wa kipekee kupitia Programu ya Ukuzaji Ujuzi nchini kwa lengo la kuwapatia ujuzi na stadi za kazi wananchi hasa kundi la vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili waweze kumudu ushindani katika soko la ajira na hivyo kuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa uchumi jumuishi wa viwanda.

30.        Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi mwaka 2014, unaonesha kuwa asilimia 79.9 ya nguvukazi ni yenye kiwango cha chini cha ujuzi, asilimia 16.6 kiwango cha kati wakati ni asilimia 3.6 tu ndiyo yenye kiwango cha juu. Ili kufikia uchumi wa viwanda, Serikali imedhamiria kubadili mwenendo huo kwa kuhakikisha nguvukazi yenye kiwango cha juu cha ujuzi inafika asilimia 12 na kiwango cha kati asilimia 34. Kwa msingi huo, Serikali inaendelea kutekeleza programu ya kukuza ujuzi pamoja na programu nyingine ili kukidhi matakwa ya uchumi wa viwanda.

31.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, jumla ya vijana 7,817 wamewezeshwa kupata ujuzi kupitia programu hiyo. Kati yao, vijana 220 walipata mafunzo kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam na vijana 3,440 kupitia Taasisi ya Don Bosco. Mafunzo waliyopewa ni katika fani za ufundi stadi wa ushonaji nguo, useremala, uashi, TEHAMA, uchongaji wa vipuri, ufundi magari, umeme, bomba, vyuma, terazo, vigae na ujuzi wa kutengeneza bidhaa za ngozi. Aidha, kupitia VETA vijana 3,989 walipata mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi kwa fani za uashi, useremala, ufundi magari, upishi na uhudumu katika hoteli.

32.        Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo ya vitendo yalitolewa pia kwa wahitimu 168 kupitia viwanda na kampuni mbalimbali katika fani ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi. Vilevile, Serikali imeandaa na kuzindua Mwongozo wa Kitaifa wa Uanagenzi na Mwongozo wa Kitaifa wa Mafunzo ya Vitendo kwa wahitimu kwa lengo la kuweka utaratibu wa utoaji wa mafunzo hayo kwa wadau wote ili waweze kuajirika. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itatoa mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi kwa vijana 10,500 katika fani mbalimbali. Ninazishukuru kampuni binafsi ambazo zinaendelea kutoa nafasi za mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika nyanja mbalimbali ili tuweze kukuza ujuzi wa rasilimali watu ya taifa.

 


Ajira


33.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kuratibu juhudi za kukuza ajira nchini. Hadi kufikia Februari 2018, jumla ya ajira 482,601 katika sekta rasmi zimezalishwa nchini. Kati ya ajira hizo, ajira 345,547, sawa na asilimia 72 zimezalishwa kutokana na shughuli za umma ikiwemo miradi ya maendeleo ya Serikali kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na miradi ya TASAF; na ajira 137,054 sawa na asilimia 28 zimezalishwa katika sekta binafsi.

34.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaandaa mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba Watanzania wazawa wanashiriki na kunufaika na miradi mikubwa ya kitaifa. Vikao kati ya Serikali na wafanyabiashara vimefanyika ili kuwaandaa kuwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuratibu masuala ya ukuzaji ajira nchini ikiwa ni pamoja na kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Ajira ili iendane na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.

 

Masuala ya Kazi na Wafanyakazi


35.        Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo tija, ufanisi na mahusiano mema mahali pa kazi, Serikali inasimamia Sheria Na.6 ya Ajira na Mahusiano Kazini na Sheria Na.7 ya Taasisi za Kazi. Sheria hizo zinalenga kuhakikisha haki na wajibu kwa mfanyakazi na mwajiri vinapatikana. Ili kufikia azma hiyo, Serikali imehimiza kuanzishwa kwa mabaraza ya wafanyakazi, kufunga mikataba ya hali bora pamoja na kufanya kaguzi mbalimbali mahali pa kazi ili kujiridhisha kuwa viwango vya kazi vinazingatiwa. 

36.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Julai 2017 hadi Februari 2018, jumla ya kaguzi 102,860 zimefanyika katika maeneo mbalimbali ya kazi nchi nzima. Sambamba na kaguzi hizo, elimu kuhusu sheria za kazi, wajibu na majukumu ya wajumbe wa baraza kwa waajiri na wafanyakazi kupitia vyama vyao ilitolewa. Jumla ya waajiri 640 na wafanyakazi 3,624 walipatiwa elimu hiyo. Aidha, mabaraza 441 ya wafanyakazi yaliundwa na 46 yalihuishwa upya.

37.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ilipokea na kusajili migogoro ya kikazi 6,113 ambapo migogoro 4,816 sawa na asilimia 79, ilitatuliwa kwa njia ya usuluhishi na uamuzi. Katika mwaka 2017/2018, utafiti kuhusu sekta na vyanzo vinavyoongoza kwa migogoro ya kikazi umefanyika. Sekta ya usafirishaji iliongoza kwa kuwa na migogoro 547; ulinzi binafsi 512; viwanda 434; elimu 420; huduma za hoteli 399 na taasisi za umma 321. Aidha, aina ya vyanzo vinavyoongoza kusababisha migogoro ya kazi ni kuachishwa kazi bila kufuata taratibu sahihi; madai mbalimbali na kuvunjwa kwa mikataba isivyokuwa halali. Utafiti huu utaisaidia Serikali kwa kushirikiana na waajiri na vyama vya wafanyakazi kuweka mipango ya pamoja na kuzuia migogoro sehemu za kazi kabla haijatokea.

38.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi na kuendeleza mijadala yenye tija ili kupunguza migogoro mahali pa kazi. Serikali pia itaendelea kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ikiwa ni pamoja na kufanya kaguzi, kusajili, kusuluhisha na kuamua migogoro katika maeneo ya kazi. Aidha, itashirikiana kwa karibu na vyama vya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kufanya majadiliano ya mara kwa mara kwa lengo la kuongeza tija na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

SEKTA BINAFSI


39.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa letu. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuboresha miundombinu wezeshi kama vile reli, barabara, umeme na maji. Hatua nyingine ni kupunguza na kufuta baadhi ya kodi zinazoathiri ufanisi wa sekta binafsi; kuhuisha sera na sheria pamoja na kuimarisha majadiliano yenye manufaa baina ya sekta ya umma na sekta binafsi. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Februari 2018, jumla ya miradi 175 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.4 ilisajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC). Miradi hiyo inatarajiwa kutoa fursa za ajira 20,178.

40.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuimarisha majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kwa nia ya kuondoa changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta binafsi. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imefanya mikutano minne na wawakilishi wa sekta binafsi. Miongoni mwa mikutano hiyo, ni ule uliofanyika tarehe 19 Machi, 2018 ambao uliongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo kwa Wizara na Taasisi za umma kukutana na wawakilishi wa sekta binafsi ili kutatua kwa haraka changamoto zilizobainishwa katika mkutano huo. Serikali inawahakikishia wafanyabiashara na sekta binafsi kwamba inawathamini na itaendelea kushirikiana nao kutatua changamoto zinazowakabili ili kujenga uchumi wa viwanda.

SEKTA YA HIFADHI YA JAMII


41.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii ikiwemo kutungwa kwa sheria inayounganisha Mifuko ya Pensheni ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF na kuunda mfuko mmoja kwa ajili ya watumishi wa umma unaojulikana kama Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma. Sheria hiyo pia, imefanya marekebisho kwenye Sheria ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii ili kuufanya Mfuko huo uhudumie wafanyakazi wa sekta binafsi pamoja na kutoa huduma ya hifadhi ya jamii katika sekta isiyo rasmi.

42.        Mheshimiwa Naibu Spika, kutungwa kwa sheria hiyo kutasaidia kuondoa changamoto iliyotokana na wingi wa mifuko ya hifadhi ya jamii inayolipa mafao yanayotofautiana kwa watumishi wa umma wenye masharti ya kazi yanayofanana. Vilevile, sheria hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya baadhi ya mifuko kutokuwa endelevu kutokana na idadi ndogo ya wanachama, ushindani usiokuwa na tija na gharama kubwa za uendeshaji. Sheria imeweka kipindi cha mpito cha miezi sita kitakachoanza tarehe ya kuanza kutumika kwa sheria hiyo. Lengo ni kuwezesha maandalizi ya utekelezaji wake kufanyika pasipo kuathiri shughuli na huduma muhimu kwa wanachama wa mifuko iliyounganishwa ikiwa ni pamoja na kupokea mafao yao.

Napenda kuwataarifu Watanzania kupitia Bunge hili kwamba tayari Mheshimiwa Rais amesaini muswada huo kuwa sheria ya nchi. Utekelezaji wa sheria hii utaboresha mafao ya wafanyakazi.
                                                                                         
43.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itakamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003 na hivyo kuandaa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ambayo itakuwa jumuishi. Lengo la Serikali ni kuwezesha huduma za hifadhi ya jamii kuwafikia wananchi wengi zaidi hususan waliopo katika sekta isiyo rasmi na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

 

Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu


44.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuimarisha uratibu na utekelezaji wa Sheria Na. 9 ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010, kwa kuhakikisha upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imeunda kamati za watu wenye ulemavu katika mikoa 12 ya Geita, Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Njombe, Pwani, Singida, Rukwa, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Ufuatiliaji unaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa mikoa mingine nayo inaunda kamati hizo.

45.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa vifaa saidizi kwa jamii ya watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kufanya shughuli zao bila utegemezi. Baadhi ya vifaa vilivyotolewa ni viti mwendo 240, bajaji 6, magongo ya kutembelea 350, kofia pana 128, fimbo nyeupe 175, miwani maalum kwa wenye uoni hafifu 70, shime sikio 20, vyerehani 8, vifaa vya kukuzia maandishi 65, mafuta maalum ya kukinga ngozi dhidi ya mionzi ya jua 35, viti maalum vya kuogea 50 na nyenzo nyingine za kujimudu. Vilevile, Serikali imeendelea kuviboresha vyuo vya watu wenye ulemavu vya Yombo, Dar es Salaam na Sabasaba, Singida. Serikali pia inakamilisha uanzishwaji wa kanzidata ya wahitimu wenye ulemavu kutoka vyuo mbalimbali nchini ili iwe rahisi kuwaunganisha na fursa za ajira zinazopatikana kwenye sekta binafsi na umma.

46.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto kwa kutoa elimu ya ulinzi na usalama kwa watoa huduma katika vituo vinavyolea watoto wenye ulemavu wa ngozi kwenye mikoa ya Shinyanga, Mara, Tabora, Simiyu, Tanga, Mwanza, Kigoma na Singida. Lengo la utoaji elimu ni kuwajengea uelewa na kuwapa mbinu watoa huduma waendelee kuimarisha ulinzi kwa watoto pamoja na kuwahimiza wazazi, walezi na jamii waone umuhimu wa kulea watoto hao kwenye ngazi ya familia.

47.        Mheshimiwa Naibu Spika, Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishwaji wa Mfuko wa Taifa wa Maendeleo wa Watu wenye Ulemavu. Serikali pia itaendelea na zoezi la kuanzisha madawati ya watu wenye ulemavu na kuhamasisha sekta binafsi na umma kuweka miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Aidha, Serikali itahimiza waajiri wote nchini kuajiri watu wenye ulemavu wenye sifa kwenye nafasi mbalimbali na pia kutoa matangazo ya ajira yanayohamasisha wenye ulemavu kuomba nafasi zinazotangazwa. Vilevile, itahamasisha na kuelimisha jamii kuhusu mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu ikiwemo kuwaheshimu, kuwatambua, kuwathamini na kutowanyanyapaa.

SEKTA ZA UZALISHAJI


Kilimo

Hali ya Upatikanaji wa Chakula


48.        Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuimarika. Katika msimu wa 2016/2017 na 2017/2018, uzalishaji ulifikia tani milioni 15.9 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.3 ya chakula kwa kipindi hicho. Kutokana na uzalishaji huo, nchi ilikuwa na ziada ya tani milioni 2.6 za mazao yote ya chakula na hivyo, kujitosheleza kwa asilimia 120. Aidha, hadi kufikia Januari, 2018 Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ulikuwa umenunua jumla ya tani 26,038 za mahindi na akiba ya chakula iliyopo ghalani ni tani 92,074.

Mazao ya Biashara na Kuimarisha Ushirika


49.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeamua kuweka mkazo maalum wa kuyaendeleza kwa kasi mazao matano ya biashara ambayo ni chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku. Lengo ni kuongeza mapato ya wakulima, kuwa chanzo cha kuaminika cha malighafi katika uchumi wa viwanda, na kuendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira na fedha za kigeni. Uamuzi wa kuongeza usimamizi katika uzalishaji wa mazao hayo makuu ya biashara unatokana na ukweli kwamba, kwa kipindi kirefu uzalishaji ulishuka kutokana na changamoto kadhaa. Miongoni mwa changamoto hizo ni kupungua tija katika uzalishaji, baadhi ya wakulima kuacha kulima mazao hayo kutokana na kukata tamaa kwa sababu mbalimbali zikiwemo vyama vya ushirika kutotekeleza vema wajibu wao, wizi, dhuluma na pia ushiriki mdogo wa maafisa kilimo katika kusimamia kilimo cha kitaalamu.

50.        Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine za kushuka uzalishaji wa mazao hayo ni huduma zisizoridhisha za ugani na utafiti, ukosefu wa pembejeo bora, utitiri wa tozo na wingi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika. Kwa mfano, uzalishaji wa zao la pamba ulipungua kutoka tani 456,814 mwaka 2013/2014, hadi tani 282,809 mwaka 2015/2016. Kwa upande wa tumbaku, uzalishaji katika kipindi cha miaka minne ulishuka kutoka tani 126,624 mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani 60,929 mwaka 2015/2016.

51.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua za kuimarisha utawala bora kwenye vyama vya ushirika kwa kusimamia chaguzi za vyama 2,537, chaguzi za viongozi wa bodi za vyama vya ushirika 532 na kufanya kaguzi katika vyama vya ushirika 2,896 vikiwemo vyama vikuu. Kazi za kusimamia vyama vya ushirika zinaendelea. Pamoja na hatua hiyo, Serikali inasimamia uendelezaji wa mazao hayo moja kwa moja kupitia maafisa kilimo na Bodi za Mazao. Hatua nyingine ni kufuta baadhi ya tozo zilizokuwa kero katika mazao makuu ya biashara pamoja na kuhakikisha kwamba mauzo yanafanyika kwa njia ya wazi na inayoleta ushindani.

52.        Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali kusimamia mazao makuu ya biashara, tayari tumeanza kuona matokeo chanya kwa kuongezeka uzalishaji wake. Kwa mfano, hadi mwezi Machi 2018, uzalishaji wa mazao ya asili ya biashara ulifikia tani 804,025. Uzalishaji huu unaashiria ongezeko la mavuno ikilinganishwa na mwaka 2016/2017. Ongezeko hilo la uzalishaji wa mazao ya biashara linakwenda sambamba na kuimarika kwa mwenendo wa bei za mazao hayo hususan korosho na kahawa.

53.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuimarisha vyama vya msingi vya ushirika vya mazao ya kilimo na masoko vinavyozalisha mazao ya kimkakati ya biashara ya pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku.

Serikali inalenga kuimarisha masoko ya mazao hayo kwa kuhamasisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo mazao hayo yatazalishwa na kuuzwa kupitia vyama vya ushirika kwa njia ya minada. Pamoja na hatua hizo, Soko la Bidhaa ambalo limeshaanzishwa, litasaidia sana kuimarisha masoko ya mazao kwani yatakuwa yanauzwa kwa njia ya ushindani mkubwa huku wakulima wanaozalisha kwa ubora wakinufaika na bei ya juu zaidi.

Pembejeo za Kilimo


54.      Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imerahisisha upatikanaji wa mbolea kwa wakulima baada ya kuanza kuagiza mbolea kwa kutumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja. Hadi kufikia mwezi Machi 2018, upatikanaji wa mbolea hapa nchini ulikuwa tani 310,674, sawa na asilimia 64 ya mahitaji ya tani 485,000 kwa mwaka. Kwa upande wa mbegu bora za kilimo, upatikanaji umefikia tani 51,700, sawa na asilimia 86.2 ya mahitaji ya tani 60,000 kwa mwaka. Kwa mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuboresha Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa pamoja ili uendelee kuleta ufanisi na tija iliyokusudiwa.

Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo


55.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imekamilisha maandalizi ya awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo. Programu hiyo itatekelezwa kwa miaka 10 katika vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaweka mkazo katika kutekeleza malengo makuu ya programu hiyo. Msukumo utawekwa kwenye kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo ya kipaumbele kwa kuimarisha upatikanaji na matumizi ya pembejeo na zana za kilimo; kuimarisha huduma za ugani; kuimarisha kilimo cha umwagiliaji; kuimarisha huduma za utafiti wa mazao ya kilimo na kuhakikisha matokeo ya utafiti yanawafikia wakulima; kuweka na kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi ya kilimo; kuimarisha usindikaji wa mazao ya kilimo na kuwezesha upatikanaji wa masoko ya mazao.

56.        Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tumeamua kwa dhati kusimamia kwa karibu sekta ya kilimo ambayo ndiyo inaajiri Watanzania wengi. Tutahakikisha kuwa mkulima ananufaika na kilimo chake kwa kuwafikishia wakulima pembejeo ikiwemo mbolea na mbegu kwa wakati; kuimarisha miundombinu ya kilimo na kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika. Pia, Serikali itatoa kipaumbele katika kufungamanisha sekta ya kilimo na viwanda kwa lengo la kuongeza thamani na faida kwenye shughuli za kilimo.

 

Mifugo


57.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba mifugo bora na ya kisasa ni fursa kubwa ya kupunguza umaskini hapa nchini. Hata hivyo, ili mifugo hiyo iweze kuleta matokeo makubwa, hususan upatikanaji wa soko la uhakika ndani na nje ya nchi, hapana budi mifugo itambuliwe bayana. Kutokana na mahitaji hayo ya utambuzi, Serikali inatekeleza zoezi la utambuzi wa mifugo kwa njia ya chapa ya moto ambapo hadi Februari 2018, ng’ombe 16,408,022 wamepigwa chapa. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 94.4 ya ng’ombe 17,390,090 waliotegemewa kupigwa chapa. Zoezi hili ni endelevu na ninawaomba wadau watoe ushirikiano wa kutosha kwa Serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Maliasili na Utalii


58.        Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa sekta ya maliasili na utalii katika ukuaji wa Pato la Taifa na kuongeza ajira, Serikali inaongeza juhudi za kulinda rasilimali za Taifa ikiwemo misitu, wanyamapori, malikale, ufugaji nyuki, uvuvi, pamoja na kuhakikisha rasilimali hizo zinanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo. Serikali pia imechukua hatua za kuimarisha mifumo ya kukusanya mapato katika sekta hizo, kupambana na ujangili, kuzuia upotevu wa mazao ya misitu na kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji na hifadhi.

Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeanza mapitio ya Sera za Taifa za Utalii, Misitu na Ufugaji Nyuki ili ziendane na mazingira ya sasa na kuimarisha zaidi ulinzi wa rasilimali hizo.

59.        Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta ya utalii, idadi ya watalii walioingia nchini mwaka 2017 imeongezeka hadi kufikia watalii milioni 1.33 ikilinganishwa na watalii milioni 1.28 mwaka 2016. Pia, mapato yameongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.19 mwaka 2017 ikilinganishwa na  Dola za Marekani bilioni 2.13 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia sita. Takwimu hizo zinabainisha kwamba, sekta ya utalii ina fursa kubwa ya kulipatia taifa fedha za kigeni na kuzalisha ajira kwa wingi.

Tutaendelea kuimarisha sekta hii kwa kuvutia wawekezaji zaidi na kuimarisha miundombinu ya maeneo ya utalii pamoja na kuhamasisha utalii wa ndani, utalii wa mambo ya kale na kihistoria katika miji ya zamani ikiwemo Bagamoyo, Kilwa na Mikindani.

Viwanda


60.         Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kwamba kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga uchumi wa Taifa unaotegemea viwanda. Hadi kufikia mwezi Februari 2018, viwanda vipya 3,306 vimeanzishwa. Aidha, Serikali inahamasisha uwekezaji katika viwanda kwa kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kodi kwa wawekezaji mahiri; kuendeleza na kuboresha miundombimu wezeshi kama vile barabara, reli, bandari, umeme na maji. Pia, kuhuisha sera,   sheria na kanuni pamoja na kufuatilia utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa na kuchukua hatua stahiki kwa wamiliki walioenda kinyume na mikataba ya mauzo. Vilevile, Mikoa na Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutenga maeneo ya uwekezaji wa viwanda.

61.         Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya hifadhi ya jamii inashiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo, pamoja na miradi mingine, NSSF na PPF kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wanatekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa sukari mkoani Morogoro. Lengo la Mradi huo ni kuzalisha tani 250,000 za sukari na umeme MW 40. Mradi huo unatekelezwa katika shamba la Mkulazi lililopo Ngerengere lenye ukubwa wa hekta 63,000 na shamba la gereza la Mbigiri lenye ukubwa wa ekari 12,000 lililopo Dakawa.

Hadi sasa ekari 2,000 za mashamba ya miwa zimetayarishwa katika eneo la Mkulazi na ekari 1,100 zimepandwa miwa. Lengo la Serikali ni kukamilisha awamu ya kwanza ya ufungaji wa mitambo ya kiwanda cha Mbigiri ifikapo mwezi Desemba, 2018 ili uzalishaji uanze mwaka 2019. Miradi hii itakapokamilika itazalisha zaidi ya ajira 100,000. Aidha, tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huu mwezi Juni, 2017 ajira za moja kwa moja 780 na ajira zisizo za moja kwa moja  24,000 ikijumuisha wakulima wadogo wa mbegu na kilimo cha nje zimezalishwa.

62.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itatoa kipaumbele katika kutekeleza miradi ya kielelezo, uanzishwaji wa kanda maalum za kiuchumi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda. Vilevile, Serikali itaweka msisitizo katika kubuni mikakati ya uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vidogo na vya kati.

 

Madini


63.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeimarisha usimamizi katika sekta ya madini ili kuiwezesha sekta hiyo kuchangia kikamilifu katika uchumi wa nchi, kuongeza mapato ya Serikali na kuzalisha ajira. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kukusanya taarifa za uzalishaji wa madini, kuimarisha ukaguzi wa uzalishaji na mauzo kwenye migodi mikubwa na midogo na kufuatilia ukusanyaji wa maduhuli. Zoezi la ukaguzi limewezesha kukamatwa kwa madini yaliyokuwa yakitoroshwa yenye thamani ya Dola za Marekani takriban 898,523 na shilingi milioni 557.

64.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Februari, 2018 maduhuli ya Serikali yaliyokusanywa kutoka sekta ya madini yalifikia shilingi bilioni 180.4. Pamoja na mambo mengine, mafanikio hayo yametokana na usimamizi makini katika sekta ya madini na uamuzi wa Serikali kufungua soko la Tanzanite nchini. Aidha, Serikali imeimarisha soko la madini nchini kwa kuhakikisha kuwa madini yanauzwa kwa ushindani.

65.        Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba, tarehe 20 Septemba 2017, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alielekeza ujengwe ukuta katika eneo linalozunguka mgodi wa Tanzanite uliopo Mererani ili kuimarisha ulinzi na kudhibiti utoroshaji wa madini hayo.

Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa ujenzi wa ukuta huo wenye mzunguko wa kilomita 24.5 umekamilika. Nitumie fursa hii, kuwapongeza viongozi na watendaji wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

66.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kujenga uwezo wa wazawa ili washiriki kikamilifu katika sekta ya madini. Uwezeshaji huo utakwenda pamoja na utoaji mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu teknolojia mbadala ya uchenjuaji dhahabu kwa lengo la kupunguza athari za mazingira na maafa katika maeneo ya migodi. Aidha, Serikali itakamilisha taratibu za kumpata mwekezaji atakayejenga mitambo ya kuchenjua madini nchini.

HUDUMA ZA KIUCHUMI


Ardhi


67.        Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa rasilimali ya ardhi kama kitovu cha uzalishaji mali, Serikali inachuka hatua madhubuti za kuiendeleza. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza Mpango Kabambe wa Majiji, Manispaa na Miji; udhibiti wa migogoro baina ya watumiaji wa ardhi na uimarishaji wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi nchini. Napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba Mipango Kabambe ya Manispaa za Iringa, Singida na Mji wa Kibaha imekamilika na mipango mingine 20 ipo katika hatua mbalimbali za uandaaji.  Hadi sasa, michoro 1,110 ya mipango miji iliidhinishwa kati ya 1,148 iliyopokelewa kutoka Halmashauri za miji mbalimbali.

Natoa wito kwa wananchi wote nchini wanapofanya shughuli za maendeleo kuzingatia mipango kabambe inayoandaliwa na mamlaka za upangaji miji.

68.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na changamoto ya migogoro ya ardhi miongoni mwa watumiaji ikiwemo migogoro ya mipaka ya vijiji, wakulima na wafugaji, wanavijiji na hifadhi na mapori ya akiba. Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kuunda timu ya kisekta ya kushughulikia migogoro ya ardhi ambayo imetembelea Mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Morogoro na Tabora na kufanya majadiliano na wadau 1,106. Hatua mbalimbali za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinaendelea kuchukuliwa.

Nishati         


69.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua thabiti kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya  uchumi wa viwanda. Hatua zilizochukuliwa zinalenga kuongeza uzalishaji, kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa umeme na kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme vijijini na mijini. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya Kinyerezi I (MW 185), Kinyerezi II (MW 240) na Mradi wa Umeme wa Maji wa Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) utakaozalisha MW 2,100.

70.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imepanua na kuboresha miundombinu ya kusafirisha umeme kwa kutekeleza miradi mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na: Mradi wa Rufiji - Chalinze - Dodoma wenye msongo wa kV 400; Mradi wa Singida – Arusha – Namanga wenye msongo wa kV 400; na Mradi wa Makambako – Songea wenye msongo wa kV 220. Utekelezaji wa miradi hii umeongeza hali ya upatikanaji umeme nchini kufikia asilimia 67.5. Aidha, uunganishaji umeme kwa watumiaji umefikia asilimia 49.5.

71.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza awamu ya tatu ya Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) ambao umepangwa kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji 7,873 ambavyo havijapata umeme nchini. Kati ya hivyo, vijiji 7,697 vimepangwa kupatiwa umeme wa Gridi ya Taifa na vijiji 176 pamoja na visiwa vitapatiwa umeme nje ya gridi kwani ndiyo njia muafaka ya kuvipatia umeme kwa sasa. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaongeza fedha za mfuko wa REA ili kuhakikisha vijiji vilivyosalia pamoja na taasisi zinazotoa huduma za kijamii vijijini zinapata umeme. Serikali pia, itaendeleza miradi ya kuunganisha Gridi ya Taifa na gridi za nchi jirani za Zambia, Kenya, Burundi na Rwanda.

Bomba la Mafuta (Hoima – Tanga)


72.        Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 5 Agosti 2017, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni waliweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga.  Uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo kwa upande wa Uganda ulifanyika katika eneo la Hoima tarehe 11 Novemba, 2017. Bomba hilo la kusafirisha mafuta ghafi litakuwa na urefu wa kilometa 1,445 ambapo kilometa 1,115 zitajengwa Tanzania. Mradi huo utakuwa na manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili ambapo ajira takriban 10,000 zitazalishwa wakati wa ujenzi na ajira zaidi ya 1,000 wakati wa uendeshaji wake.

 

Barabara


73.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuboresha mtandao wa barabara nchini. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Februari 2018, ujenzi wa Km. 776.45 za barabara kuu kwa kiwango cha lami umekamilika na Km. 1,760 zinaendelea kujengwa. Aidha, barabara zenye urefu wa Km. 17,054 zimekarabatiwa katika kipindi hicho. Vilevile, ujenzi wa madaraja ya Kilombero na Kavuu umekamilika na ujenzi wa madaraja ya Sibiti, Mto Mara, Lukuledi, Ruhuhu, Momba na Mlalakuwa unaendelea. Madaraja mengine 996 katika maeneo mbalimbali nchini yamekarabatiwa.

74.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Hadi kufikia Februari 2018, ujenzi wa barabara ya juu katika eneo la TAZARA ulifikia asilimia 70 na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo (Ubungo Interchange) umeanza. Aidha, maandalizi ya Awamu ya Pili hadi ya Nne ya Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka yanaendelea. Katika mwaka 2018/2019, Serikali imepanga kujenga kilometa 597 za barabara kuu na za mikoa kwa kiwango cha lami na kilometa 72 za kiwango cha lami zitakarabatiwa.

Barabara za Vijijini na Mijini


75.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tanzania Rural and Urban Roads Agency – TARURA) kwa lengo la kurahisisha huduma za usafirishaji na kuongeza kasi ya wananchi kujiletea maendeleo. TARURA imepewa jukumu la kusimamia ujenzi na matengenezo ya mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 108,946.2 za vijijini na mijini. Katika mwaka 2017/2018, TARURA imesimamia matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 4,183.3, madaraja 35, makalavati makubwa 43 na madogo 364 na drift nne. Napenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa TARURA kuwaelimisha wananchi, viongozi na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu majukumu na mfumo wa utendaji kazi wake.

Reli


76.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) itakayokuwa na urefu wa Km. 1,219. Hadi sasa, ujenzi wa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye Km. 300 umeanza na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2019. Aidha, tarehe 14 Machi 2018, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande cha kutoka Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa kilomita 422. Ujenzi wa reli hii utasaidia kukuza sekta nyingine za kiuchumi kama vile kilimo, viwanda, madini, utalii pamoja na kutoa fursa nyingi za ajira. Utekelezaji wa mradi huu unakadiriwa kutoa ajira 30,000 za moja kwa moja na nyingine 600,000 zisizo za moja kwa moja.

Bandari


77.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa majini. Uboreshaji huo utaanza na Gati Na. 1 – 7; kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia meli na eneo la kugeuzia meli; kuimarisha mtandao wa reli bandarini pamoja na kujenga gati maalumu la kuhudumia meli za magari. Vilevile, Mamlaka ya Bandari Tanzania imefungua ofisi katika baadhi ya nchi jirani kwa lengo la kuongeza urahisi wa kutoa huduma. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea na uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Aidha, Serikali itatekeleza mradi wa dirisha moja la forodha (Tanzania Electronic Single Window System-eSWS) ili kuwaweka pamoja wadau wote wa kuondosha shehena bandarini na mipakani. Kukamilika kwa mradi huo, kutarahisisha na kupunguza muda na gharama za utoaji na upitishaji wa shehena bandarini.

 

Mawasiliano


78.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kutekeleza Awamu ya Tatu ya mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa miundombinu ya itifaki (Internet Protocol – Multiplier Label Switching) pamoja na ujenzi wa kituo cha kuhifadhi data ambacho hadi sasa mifumo ya taasisi 27 imeunganishwa ukiwemo mfumo wa ukusanyaji mapato wa TRA. Kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kutaongeza usalama, usiri wa data, kujikinga na majanga na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali na muingiliano wa mifumo katika Kituo cha Data cha Taifa na vituo vingine vitakavyojengwa nchini.

79.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kufikisha huduma ya mawasiliano vijijini ambapo vijiji 1,921 vimepatiwa huduma hiyo. Aidha, Serikali imeimarisha huduma za simu na intaneti katika taasisi za umma zikiwemo shule, vituo vya afya, vituo vya polisi na ofisi za posta. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kupanua matumizi yake hadi katika ngazi ya wilaya. Vilevile, kuendelea kusimamia kampuni za simu nchini ili ziweze kutoa kumbukumbu sahihi kwa lengo la kukokotoa mapato yatokanayo na malipo ya huduma za simu za kitaifa na kimataifa.

HUDUMA ZA JAMII

 

Elimu


80.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetekeleza kwa mafanikio mpango wa utoaji wa elimu ya awali na elimumsingi bila malipo. Tangu kuanza kwa mpango huo, Serikali imekuwa inapeleka kwa wakati na moja kwa moja shuleni fedha zote za ruzuku ya elimumsingi. Kiasi cha shilingi bilioni 20.8 kinapelekwa kila mwezi kwa shule zote za msingi na sekondari nchini, ikijumuisha fedha za posho maalum kwa Walimu Wakuu, Waratibu wa Elimu Kata na Wakuu wa Shule.

81.        Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji mzuri wa mpango wa elimumsingi bila malipo umechangia kuimarika kwa mahudhurio ya wanafunzi darasani; kuongezeka kwa ubora wa elimu inayotolewa shuleni kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi. Kwa mfano, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza imeongezeka kutoka 1,568,378 mwaka 2015 hadi 2,120,667 mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 35.2. Kwa mwaka huu, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza ni 2,078,379. Vilevile, wanafunzi waliofaulu mtihani wa kuhitimu darasa la saba na kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 448,826 mwaka 2015 hadi wanafunzi 538,826 mwaka 2016; na mwaka 2017 wanafunzi 562,695 wamechaguliwa kuingia sekondari.

82.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imejenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari ikiwemo ukarabati wa shule za sekondari kongwe 89 ili kuboresha mazingira ya shule na kuinua ubora wa elimu. Aidha, Serikali imenunua na kusambaza vifaa vya maabara vyenye thamani ya shilingi bilioni 16.9 kwa shule za sekondari 1,696 kwa ajili ya kuimarisha ujifunzaji wa masomo ya sayansi kwa nadharia na vitendo. Vilevile, walimu 3,347 wa masomo ya sayansi na hisabati na mafundi sanifu wa maabara 386 wameajiriwa. 

83.        Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutoa kipaumbele kwenye elimu, imeleta hamasa kubwa kwa wananchi kuchangia maendeleo ya elimu. Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia kwa hiari maendeleo ya elimu kupitia Ofisi za Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri. Aidha, naziagiza Halmashauri zote nchini kuratibu na kusimamia ipasavyo michango ya hiari ya elimu inayotolewa na wananchi na matumizi yake, hususan kwa kuanzisha Mfuko Maalum wa Elimu katika Halmashauri husika ambao utasimamiwa na Bodi.

84.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 365 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 483 mwaka 2017. Hatua hiyo imewezesha idadi ya wanaonufaika na mikopo hiyo kuongezeka kutoka wanafunzi 98,300 mwaka 2015 hadi wanafunzi 119,435 mwaka 2017/2018. Serikali pia inaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya vyuo vya elimu ya juu nchini ili kuboresha mazingira ya vyuo hivyo na kuviwezesha kuzalisha wataalam mahiri wanaoweza kujiajiri au kuajiriwa katika soko la ajira. Natoa wito kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu na wadau wa elimu kufanya tathmini na kuboresha mfumo wa ufundishaji wa wanafunzi wa elimu ya juu nchini ili kuwapatia mbinu zitakazowawezesha kujiajiri.

85.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu wa mwaka 2017 hadi 2021 pamoja na mpango kazi wake unaolenga kutekeleza vipaumbele vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Utekelezaji wa mpango huo wa sekta ya elimu utasaidia kuongeza idadi ya wataalam wenye ujuzi wa kati na wa juu ifikapo mwaka 2021. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya pili ya ukarabati wa shule kongwe, kujenga ofisi za udhibiti ubora katika wilaya mbalimbali nchini, kununua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari na kujenga vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari.

 

Maji


Huduma ya Maji Vijijini


86.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini kwa kujenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji. Katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla ya miradi 71 imekamilishwa vijijini na mingine 366 inaendelea kutekelezwa. Utekelezaji wa miradi hiyo, umewezesha kuongezeka idadi ya wananchi wanaopata maji vijijini. Pia, Serikali imepanga kubadilisha mitambo inayotumia nishati ya dizeli kusukuma maji na kufunga mitambo inayotumia nishati ya jua ili kuwapunguzia wananchi gharama za uendeshaji na matengenezo.

87.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2018/2019, Serikali itakamilisha ujenzi wa miradi  ya maji 387 kwenye Halmashauri mbalimbali nchini na kuanza miradi mipya ya maji vijijini; kutekeleza miradi ya maji vijijini katika maeneo kame na yenye shida kubwa ya maji; kuendelea na ujenzi na ukarabati wa mabwawa pamoja na upanuzi wa miundombinu ya maji kutoka kwenye mabwawa na visima vilivyochimbwa. Vilevile, Serikali itaendelea na ujenzi wa miradi mikubwa ya maji katika maeneo ya Tabora, Kigoma na Same - Mwanga- Korogwe.

Huduma ya Maji Mijini


88.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Serikali imejenga, kupanua na kukarabati miradi ya maji katika maeneo mbalimbali mijini ili kufikia malengo yaliyowekwa. Juhudi hizo zimewezesha hali ya upatikanaji wa maji kwenye miji mikuu ya mikoa kufikia wastani wa asilimia 78. Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo yanayohudumiwa na DAWASA, upatikanaji wa maji umefikia asilimia 75. Aidha, upatikanaji wa maji katika miji mikuu ya wilaya, miji midogo na maeneo yanayohudumiwa na miradi ya kitaifa umefikia asilimia 60. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kukamilisha miradi mingi ya maji iliyopo.

 

Afya


Utoaji wa Chanjo


89.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasimamia shughuli za utoaji wa chanjo nchini ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa kitaifa na kimataifa yanafikiwa.  Hadi sasa, Tanzania imefikia kiwango cha juu cha asilimia 97 ya utoaji wa chanjo ya pentavalent kwa watoto inayokinga magonjwa ya kifaduro, dondakoo, pepopunda, homa ya ini na mafua. Kutokana na kufikia kiwango hicho, mwezi Desemba 2017, Serikali ya Tanzania ilipongezwa na Shirika la Afya Duniani kwa hatua hiyo kubwa. Lengo la Shirika la Afya Duniani ni kila nchi kufikia kiwango cha uchanjaji wa asilimia 90.

90.        Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na usimamizi madhubuti wa Serikali katika utoaji wa chanjo. Niwapongeze sana viongozi na watendaji wa sekta ya afya pamoja na mamlaka zote zinazohamasisha na kutoa huduma za chanjo hapa nchini.

Upatikanaji wa Dawa, Vifaa na Vifaa Tiba


91.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya. Bajeti kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi imeongezwa kutoka shilingi bilioni 252 mwaka 2016/2017 na kufikia shilingi bilioni 269 mwaka 2017/2018. Kutokana na ongezeko hilo, upatikanaji wa aina 135 ya dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini umeimarika na kufikia asilimia 89.6.

 

Huduma za Tiba za Kibingwa


92.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya kibingwa nchini. Huduma zilizoimarishwa ni pamoja na upandikizaji wa figo na vifaa vya kuongeza usikivu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, upasuaji kwa kutumia tundu dogo na kufungua kifua katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Vilevile, Serikali imeimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambapo dawa zinapatikana na muda wa kupata huduma ya mionzi ya saratani umepungua. Kutokana na maboresho hayo, idadi ya wagonjwa waliopewa rufaa ya matibabu nje ya nchi imepungua kutoka wagonjwa 304 mwaka 2016/2017 na kufikia 103 mwaka 2017/2018. Hatua hiyo imesaidia kupunguza gharama kubwa ambazo Serikali ingetumia kuwapeleka wagonjwa hao nje ya nchi.

ULINZI NA USALAMA


93.        Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya mipaka ya nchi yetu ni salama. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kuliimarisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kutoa mafunzo na mazoezi ya kijeshi, kulipatia vifaa, zana, mitambo bora na ya kisasa pamoja na kuweka na kuimarisha miundombinu muhimu na ya kimkakati ili kuliwezesha jeshi kutekeleza jukumu lake la ulinzi wa mipaka ya nchi yetu. Vilevile, Serikali imeweka alama za mipakani ili kuimarisha ulinzi na kulinda vema mipaka ya nchi. Aidha, Jeshi la Wananchi linashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, mamlaka za kiraia na mataifa mengine kupambana na matishio mapya ya kiusalama yakiwemo ugaidi, uharamia, uhamiaji haramu, biashara haramu za dawa za kulevya na usafirishaji haramu wa binadamu.

94.        Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi letu limeendelea kudumisha ushirikiano na nchi nyingine duniani kupitia mafunzo ya pamoja na operesheni za kikanda na kimataifa chini ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Katika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani, tarehe 7 Desemba 2017 nchi yetu ilipoteza askari 15 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kutokea kwa askari wetu wanaolinda amani. Kwa mara nyingine, naomba kuungana na Mheshimiwa Rais na Watanzania wote kuzipa pole familia za mashujaa hawa waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi wa amani. Licha ya changamoto zinazojitokeza, Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani kwenye nchi mbalimbali duniani ili kuendelea kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi pamoja na kuyaongezea majeshi yetu uzoefu na mbinu za kisasa  za ulinzi wa amani.

95.        Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa usalama wa raia, Serikali imelipatia Jeshi la Polisi vitendea kazi muhimu ikiwemo vifaa vya kisasa vya mawasiliano na uchunguzi ili liweze kupambana na ujambazi na matukio mengine ya kihalifu nchini. Aidha, imejenga Kituo cha Kisasa cha Mawasiliano (Call Centre) Dar es Salaam ambacho kinawezesha wananchi kutoa taarifa ya matukio hayo kwa urahisi. Pia Serikali imehamasisha jamii kushiriki katika ulinzi wao na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kuwapatia taarifa za wahalifu na uhalifu. Natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola ili kudhibiti matukio ya kihalifu nchini.

96.        Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi wa Uhamiaji Mtandao (e-immigration) ambapo mwezi Januari 2018, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Pasi Mpya ya Kusafiria ya Kielektroniki ya Kimataifa ya Afrika Mashariki. Kuzinduliwa kwa pasi hii kutapunguza vikwazo vya kusafiri mipakani baina ya raia wa nchi wanachama, kuimarisha mahusiano na kuchochea shughuli za kiuchumi miongoni mwa raia wa Jumuiya hii. Natoa rai kwa Watanzania kuanza kutumia pasi hii na kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, ajira na elimu zinazopatika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

97.        Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua hiyo, Serikali imedhibiti wimbi la wakimbizi na wahamiaji haramu wanaoingia nchini kwa sababu mbalimbali. Aidha, ofisi tisa mpya za uhamiaji zimefunguliwa katika wilaya za Gairo, Iramba, Kakonko, Kilosa, Kiteto, Manyoni, Mvomero, Siha na Songwe kwa lengo la kuongeza udhibiti wa wahamiaji haramu. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa uhamiaji mtandao. 

 

BUNGE


98.        Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, kumekuwa na mikutano mitatu ya Bunge ambapo masuala mbalimbali yalijadiliwa na kutolewa ufafanuzi na Serikali. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Mkutano huu wa Bajeti utakuwa unahitimisha idadi ya mikutano minne ya Bunge kwa mwaka huu wa fedha unaoishia Juni, 2018. Katika mikutano mitatu iliyopita, maswali ya msingi 359 na maswali ya nyongeza 1,002 yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, katika utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, maswali ya msingi 17 pamoja na mawili ya nyongeza yaliulizwa na kujibiwa. Miswada 15 ya Sheria ya Serikali iliwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.

99.        Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Bunge liliratibu na kusimamia shughuli za vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, kutoa huduma za hansard, utafiti, utawala na kutoa mafunzo kwa Waheshimiwa wabunge na watumishi wa Ofisi ya Bunge. Pia, Bunge lilijadili na kuridhia Maazimio matano yanayohusu utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.

MAHAKAMA


100.     Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kuongeza ufanisi wa utendaji wa mhimili wa Mahakama nchini. Katika mwaka 2017/2018, Mahakama imesikiliza na kukamilisha mashauri 494,525 kati ya 513,329, sawa na asilimia 96.3 ya mashauri yote katika ngazi zote za Mahakama. Hatua hii imesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri katika mahakama zetu. Hali kadhalika, katika kipindi hicho Serikali imekamilisha ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Kigoma na Mara. Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa Mahakama za Wilaya na za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini.

 

MASUALA MTAMBUKA


Mfumo wa Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali


101.     Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali ilizindua Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Shughuli za Serikali. Mfumo huo unalenga kuongeza ufanisi katika uratibu wa shughuli za Serikali na kuiwezesha Serikali kufanya tathmini ya utoaji huduma kwa wananchi na mipango ya maendeleo. Mfumo huo umeanza kufanya kazi ambapo kwa sasa Wizara zote zinawasilisha utekelezaji wa shughuli zao kupitia mfumo huo. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaimarisha matumizi ya mfumo huo hasa katika ngazi za Mikoa na Halmashauri na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.

 

Hifadhi ya Mazingira


102.     Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza jukumu la usimamizi na uhifadhi wa mazingira nchini. Katika mwaka 2017/2018, Serikali imeongeza hamasa na ushirikishwaji mkubwa wa wananchi katika suala la usafi, utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika maeneo yote ikiwemo makazi yao. Hatua hiyo imetokana na ushiriki mkubwa wa viongozi wa kitaifa, mikoa na watendaji wa ngazi zote katika shughuli za usafi na uhifadhi wa mazingira.

103.     Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuimarisha ukaguzi wa masuala ya hifadhi ya mazingira nchini, Serikali imeongeza idadi ya Wakaguzi wa Mazingira kutoka 62 hadi kufikia 512. Aidha, kaguzi 380 zimefanyika kwenye viwanda kwa lengo la kufanya tathmini za mazingira pamoja na kutoa elimu na uelewa kuhusu uendeshaji endelevu wa viwanda unaozingatia utunzaji bora wa mazingira.

104.     Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika Mkutano wa Kumi wa Bunge hili, napenda kusisitiza kwamba halmashauri zote nchini ziweke mpango mahsusi wa kuhifadhi mazingira unaojumuisha kupanda na kutunza miti. Serikali itaweka utaratibu wa upimaji wa utendaji wa wakuu wote wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri unaozingatia uendelezaji na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao.

 

Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya


105.     Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imeimarisha utendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kuipatia wataalamu, vifaa na kuongezea fedha. Aidha, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, imefanyiwa marekebisho ili kuondoa mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji wake. Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, ilikamata jumla ya watuhumiwa 11,071 na kati yao, watuhumiwa 3,486 ni wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambao walifikishwa mahakamani. Watuhumiwa wengi waliokamatwa, walijihusisha na dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi na heroine.

106.     Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hicho, jumla ya tani moja na kilo 561.28 za dawa aina ya heroin zilikamatwa. Kati ya hizo, kilo 196.28 zilikamatwa kwenye eneo la maji ya Tanzania na nchi kavu na tani moja na kilo 365 zilikamatwa kwenye bahari kuu kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa na kuteketezwa. Aidha, kilo 5.2 za cocaine, tani 47.7 za bangi na tani 7.4 za mirungi zilikamatwa. Mamlaka pia ilikamata lita 304,513 za vimiminika vya kemikali bashirifu na kilo 22,143 za kemikali bashirifu yabisi. Katika operesheni za uteketezaji wa mashamba ya bangi na mirungi, ekari 572.75 za bangi na ekari 64.5 za mirungi ziliteketezwa.

107.     Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeimarisha huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kutumia methadone katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mwananyamala na Temeke jijini Dar es Salaam.

Vilevile, Serikali imeanzisha vituo vipya vya tiba hiyo ili kuwafikia waathirika wengi zaidi nchini ambapo kliniki saidizi za kutibu waathirika wa dawa za kulevya zimeanzishwa katika hospitali za rufaa za mikoa ya Mbeya na Mwanza. Hadi kufikia Januari 2018, zaidi ya watumiaji 5,560 walikuwa wakipatiwa huduma za tiba ya methadone katika vituo mbalimbali nchini. Serikali pia imekuwa ikisimamia uanzishwaji wa nyumba za upataji nafuu (Sober House) ambazo hadi sasa idadi yake ni 22. Aidha, mwezi Februari 2018, Serikali ilizindua mwongozo wa uendeshaji wa sober houses unaolenga kuwawezesha wamiliki wa nyumba hizo kuwasaidia waathirika hao ipasavyo.

108.     Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Machi 2018, nchi yetu ilishiriki katika Mkutano wa 61 wa Kimataifa wa Commission for Narcotic Drugs (CND) uliofanyika Vienna, Austria na kushirikisha zaidi ya nchi 150. Katika mkutano huo, Tanzania ilitambuliwa kama nchi ya mfano katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya barani Afrika na kupewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Vyombo vinavyopambana na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani (HONLEA) kutoka Afrika, utakaofanyika Septemba 2018. Mkutano huo utatoa fursa kwa wataalam nchini kubadilishana taarifa, uzoefu, kujenga mahusiano na kujifunza mbinu zinazotumiwa na nchi nyingine katika kukabiliana na dawa za kulevya.

109.     Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa viongozi na watendaji kuwaelimisha vijana kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya. Aidha, wananchi waendelee kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kutoa taarifa kuhusu wanaojihusisha na dawa hizo. Pia ni vema wazazi, walezi na jamii kuwa karibu na vijana wetu na kufuatilia nyendo zao ili kuwaepusha kuingia kwenye mkumbo wa matumizi ya dawa za kulevya.

Vita dhidi ya Rushwa


110.     Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kupambana na rushwa pamoja na ufisadi. Katika kipindi cha mwezi Julai 2017 hadi Machi 2018, jumla ya majalada 325 yalifanyiwa uchunguzi na TAKUKURU na kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo majalada 214 kati ya hayo yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani.

Aidha, kesi 727 ziliendeshwa mahakamani na kesi 219 ziliamuliwa na watuhumiwa 138 walipatikana na hatia na kuhukumiwa. Kutokana na operesheni zilizofanywa na TAKUKURU katika maeneo ya ukusanyaji mapato, uzuiaji wa malipo hewa na ukaguzi wa miradi ya maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 58.4 ziliokolewa na kurejeshwa Serikalini.

111.     Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU pia imefuatilia miradi ya maendeleo 195 yenye thamani ya shilingi bilioni 154.1 katika sekta za elimu, afya, maji na ujenzi ili kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kama zilivyokusudiwa na thamani ya fedha inapatikana. Katika ufuatiliaji huo, miradi 73 yenye thamani ya shilingi bilioni 30.9 ilibainika kuwa na kasoro katika utekelezaji wake. TAKUKURU imetoa mapendekezo ambayo yanafanyiwa kazi na Serikali na tayari hatua za kinidhamu na kisheria zimechukuliwa kwa wahusika.

 

Mapambano Dhidi ya UKIMWI


112.     Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika jamiii. Ili kutekeleza azma hiyo, Mpango wa Kuzuia Maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto umepewa kipaumbele. Aidha, elimu ya UKIMWI imetolewa kupitia vyombo vya habari, majarida na vipeperushi. Vilevile, elimu imetolewa kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu rika pamoja na kuwashirikisha viongozi na watu mashuhuri, viongozi wa dini, sekta binafsi na kutekeleza programu za kupambana na UKIMWI mahali pa kazi.

Kutokana na juhudi hizo, matokeo ya utafiti uliofanyika katika ngazi ya kaya kuanzia mwezi Oktoba 2016 hadi Agosti 2017 yanaonesha kuwa wastani wa kitaifa wa maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ni asilimia 4.7. Aidha, utafiti huo umebainisha kwamba kiwango cha maambukizi mapya ya VVU kwa mwaka ni asilimia 0.27.

113.     Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatoa huduma kwa wananchi wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) nchini. Hadi kufikia Septemba 2017, WAVIU 972,127 sawa na asilimia 70 ya WAVIU wote walikuwa wanapatiwa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV’s). Katika mwaka 2017/2018, Serikali kwa kushirikiana na wadau wamechangia zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwenye Mfuko Maalum wa UKIMWI ili kupunguza utegemezi kutoka kwa wafadhili. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nne wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023. Vilevile, kampeni maalum za kushawishi wanaume kushiriki katika kupima afya zao na vijana kujitambua zitaendeshwa.

 

Uratibu wa Maafa


114.     Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuratibu shughuli za usimamizi wa maafa nchini kwa kuzuia, kupunguza madhara na  kujiandaa kukabiliana na maafa pindi yanapotokea. Aidha, mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa taarifa za tahadhari za awali ili kupunguza madhara ya maafa umeboreshwa. Serikali pia imekamilisha kusimika mashine 36 za kisasa za kufuatilia taarifa za hali ya hewa katika wilaya mbalimbali nchini pamoja na kuwaongezea uwezo wataalamu wa hali ya hewa. Jitihada hizi zimeongeza uhakika wa utabiri wa hali hewa nchini kufikia asilimia 87.

115.     Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeimarisha ushirikiano katika masuala ya usimamizi wa maafa kupitia Umoja wa Afrika na jumuiya za SADC, EAC na IGAD. Ushirikiano huo, umewezesha nchi wanachama kubadilishana taarifa za kuandaa utabiri wa hali ya hewa na matumizi yake katika kupunguza madhara ya maafa. Vilevile, nchi hizo zinabadilishana uzoefu pamoja na kutoa mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa wataalam wa nchi wanachama. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa na Wilaya na kuratibu shughuli za kupunguza madhara ya maafa na misaada ya kibinadamu.

Mbio za Mwenge wa Uhuru


116.     Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliratibu mbio za Mwenge wa Uhuru kwa lengo la kukuza mshikamano na kuhimiza shughuli za maendeleo. Katika mbio hizo ambazo kilele chake kilikuwa tarehe 14 Oktoba 2017 Mjini Magharibi Zanzibar, miradi 1,512 yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.06 iliwekewa mawe ya  msingi na kuzinduliwa. Kati ya miradi hiyo, miradi 150 yenye thamani ya shilingi bilioni 568.8 ilikuwa ya viwanda.  Uzinduzi wa mbio za mwenge kwa mwaka 2018 ulifanyika mkoani Geita tarehe 2 Aprili 2018 na kilele chake kitafanyika mkoani Tanga, tarehe 14 Oktoba 2018. Ninawasihi wananchi kushiriki kwa wingi wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwani zinalenga kuleta umoja na mshikamano kwa wananchi pamoja na kuhimiza shughuli za maendeleo.

MAHUSIANO YA KIMATAIFA


117.     Mheshimiwa Naibu Spika,  jukumu la kuimarisha mahusiano na mataifa mengine duniani, mashirika ya kimataifa na washirika wetu wa maendeleo limeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali katika kutekeleza Sera yetu ya Mambo ya Nje. Katika kufanikisha jukumu hilo kwa ufanisi, Serikali inafanya mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ili iweze kukidhi mahitaji na matakwa ya sasa ya Tanzania katika kushughulikia siasa za kimataifa na diplomasia pamoja na masuala ya mtangamano wa kikanda na kuendeleza Umoja wa Afrika.

118.     Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji na watalii; kutafuta fursa za mafunzo; kuendelea kuwashirikisha Watanzania waishio ughaibuni kuchangia katika maendeleo ya nchi yao pamoja na kutafuta ajira na masoko ya bidhaa za Tanzania nje. Aidha, Serikali itaimarisha sera ya ujirani mwema kwa lengo la kukuza mahusiano na kufungua milango ya ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya kitaifa ya kipaumbele hususan, reli, barabara, nishati na biashara na majirani zetu.

Vilevile, Serikali itatoa msukumo kwa Mabalozi kutumia ushawishi wao kuitangaza vyema miradi ya kipaumbele na vivutio mbalimbali vilivyopo nchini na kutangaza lugha ya Kiswahili ambayo ikitumika vizuri inaweza kuwa chanzo cha ajira kwa Watanzania.

HITIMISHO


119.     Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanashuhudia mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi cha takriban miaka miwili na nusu tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iingie madarakani. Mafanikio hayo yanatoa matumaini kwa Watanzania kwamba yale yaliyoahidiwa ndani ya kipindi cha miaka mitano yatatekelezwa.

120.     Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia malengo ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali pamoja na mambo mengine, itaweka mkazo katika kudhibiti upotevu wa mapato; kuimarisha mfumo wa kukusanya mapato hususan kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na kudhibiti matumizi ya fedha na rasilimali nyinginezo za umma. Aidha, msukumo utawekwa katika kuhimiza uwajibikaji wa watendaji wa Serikali na kuimarisha ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.

121.     Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wakati anazindua Bunge lako Tukufu tarehe 20 Novemba 2015, pamoja na mambo mengine aliweka wazi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi wa viwanda kwa lengo la kutengeneza ajira nyingi kwa Watanzania.

Ili kufikia azma hiyo, Serikali itaendelea kufanya yafuatayo:

Mosi:              Kuimarisha na kudumisha amani, utulivu, mshikamano na umoja wa kitaifa uliopo ili kuleta maendeleo endelevu;

Pili:             Kuboresha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na utoaji huduma;

Tatu:              Kujenga miundombinu muhimu ikiwemo reli, bandari, viwanja vya ndege, barabara na madaraja;

Nne:            Kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa nishati ya uhakika sambamba na kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi, mashamba na maeneo ya makazi na  viwanda;

Tano:              Kusimamia viongozi na watendaji wote ili kuondoa urasimu usio wa lazima pamoja na kuwahudumia wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote; na

Sita:               Kusimamia kikamilifu rasilimali zilizopo ili zitumike kwenye maeneo yanayochochea ukuaji uchumi na utoaji huduma bora kwa wananchi.

122.     Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa kila mwananchi kuendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu uaminifu na kupiga vita rushwa.

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2018/2019


122.     Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2018/2019, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini yake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Arobaini na  Tatu, Milioni Mia Sita Kumi na Nane, Mia Saba Sitini na Mbili  Elfu na Mia Sita Tisini na Nane (Shilingi 143,618,762,698). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sabini na Nne, Milioni Mia Tano Ishirini na Saba, Mia Tatu Ishirini na Moja Elfu na Mia Sita Tisini na Nane (Shilingi 74,527,321,698) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Sitini na Tisa, Milioni Tisini na Moja, Mia Nne Arobaini na Moja Elfu (Shilingi 69,091,441,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

123.     Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, naliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Tano, Milioni Mia Tano Ishirini na Moja, na Mia moja Elfu (Shilingi 125,521,100,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Moja Kumi na Saba, Milioni Mia Mbili na Tano, Mia Nne Themanini na Saba Elfu (Shilingi 117,205,487,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Nane, Milioni Mia Tatu Kumi na Tano, Mia Sita Kumi na Tatu Elfu (Shilingi 8,315,613,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.

124.     Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.