Friday, April 27, 2018

VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WATAKIWA KUWA MAKINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamewataka viongozi wa vyama vya siasa wajitahidi kuwa makini na namna wanavyoendesha vyama vyao kwa sababu wananchi wanaowaongoza ni wa vyama vyote.

Pia amewaasa viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa waendelee kushikamana ili waweze kulifikisha Taifa mahali ambapo Watanzania wanapatarajia ikiwa ni pamoja na kupunguza umaskini.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Aprili 27, 2018) wakati akizungumza na Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa katika ukumbi wa mikutano wa Waziri Mkuu ulioko Mlimwa jijini Dodoma.

“Viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa wajitahidi kuwa makini na namna ambavyo wanaendesha siasa katika vyama vyao, wananchi wanaowaongoza ni wa vyama vyote hivyo tupeleke ujumbe ambao utawaongoza kujileta maendeleo.”

Waziri Mkuu amesema kuwa mazungumzo yaliyofanyika leo baina ya Serikali na viongozi hao yameonesha nia ya pamoja ya kuendeleza ushirikiano. Pia amesema wana wajibu wa kuendeleza historia nzuri kwani siasa ni moja ya nyenzo zinazochochea  maendeleo.

Akijibu ombi la viongozi hao kuhusu changamoto ya upatikanaji wa fedha za kuendesha shughuli za baraza hilo ikiwemo mikutano, Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali  itafanyia kazi maombi hayo ili waweze kutimiza majukumu yao kama ilivyokusudiwa.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.