Wednesday, April 4, 2018

MAJALIWA: SERIKALI YAAJIRI WAKAGUZI WA MAZINGIRA 450

Asema Serikali imeimarisha mifumo ya taarifa za ardhi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeongeza idadi ya Wakaguzi wa Mazingira kutoka 62 hadi kufikia 512 ili kuimarisha ukaguzi wa masuala ya hifadhi ya mazingira nchini.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) Bungeni mjini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019 kwenye mkutano wa 11 wa Bunge.

Amesema katika mwaka wa fedha uliopita, jumla ya kaguzi 380 zimefanyika kwenye viwanda kwa lengo la kufanya tathmini za mazingira pamoja na kutoa elimu na uelewa kuhusu uendeshaji endelevu wa viwanda unaozingatia utunzaji bora wa mazingira.

“Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa Kumi wa Bunge hili, halmashauri zote nchini zinapaswa ziweke mpango mahsusi wa kuhifadhi mazingira unaojumuisha kupanda na kutunza miti. Serikali itaweka utaratibu wa upimaji wa utendaji wa wakuu wote wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri unaozingatia uendelezaji na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao,” alisisitiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali inachukua hatua madhubuti za kuendeleza ardhi kutokana na umuhimu wake kama kitovu cha uzalishaji mali.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni kutekeleza mpango kabambe wa majiji, manispaa na miji; kudhibiti migogoro baina ya watumiaji wa ardhi na kuimarisha mfumo unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi nchini.

“Napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba Mipango Kabambe ya Manispaa za Iringa, Singida na Mji wa Kibaha imekamilika na mipango mingine 20 ipo katika hatua mbalimbali za uandaaji. Hadi sasa, michoro 1,110 ya mipango miji imeshaidhinishwa kati ya 1,148 iliyopokelewa kutoka Halmashauri za miji mbalimbali,” alisema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wote wanapofanya shughuli za maendeleo, wazingatie mipango kabambe inayoandaliwa na mamlaka za upangaji miji kwenye maeneo yao husika.


Alisema Serikali imechukua hatua kadhaa za kukabiliana na changamoto ya migogoro ya ardhi miongoni mwa watumiaji ikiwemo migogoro ya mipaka ya vijiji, wakulima na wafugaji, wanavijiji na hifadhi na mapori ya akiba.

“Moja ya hatua zilizochukuliwa ni kuunda timu ya kisekta ya kushughulikia migogoro ya ardhi ambayo imetembelea mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Morogoro na Tabora na kufanya majadiliano na wadau 1,106. Hatua mbalimbali za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinaendelea kuchukuliwa.”

Kuhusu utendaji wa bandari nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ili kuifanya Tanzania iwe kitovu cha usafiri wa majini. Alisema uboreshaji huo utaanza na gati namba moja hadi saba; kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia meli na eneo la kugeuzia meli; kuimarisha mtandao wa reli bandarini pamoja na kujenga gati maalumu la kuhudumia meli za magari.

“Vilevile, Mamlaka ya Bandari Tanzania imefungua ofisi katika baadhi ya nchi jirani kwa lengo la kuongeza urahisi wa kutoa huduma. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea na uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara,” alisema.

“Serikali itatekeleza mradi wa dirisha moja la forodha (Tanzania Electronic Single Window System-eSWS) ili kuwaweka pamoja wadau wote wa kuondosha shehena bandarini na mipakani. Kukamilika kwa mradi huo, kutarahisisha na kupunguza muda na gharama za utoaji na upitishaji wa shehena bandarini,” alisema Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umejumuisha ujenzi wa mtandao wa miundombinu ya itifaki (Internet Protocol – Multiplier Label Switching) pamoja na ujenzi wa kituo cha kuhifadhi data ambacho hadi sasa mifumo ya taasisi 27 imeunganishwa ukiwemo mfumo wa ukusanyaji mapato wa TRA.

“Kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kutaongeza usalama, usiri wa data, kujikinga na majanga na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali na muingiliano wa mifumo katika Kituo cha Data cha Taifa na vituo vingine vitakavyojengwa nchini,” alisema.

Kuhusu huduma ya mawasiliano vijijini, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ambapo vijiji 1,921 vimepatiwa huduma hiyo. “Serikali imeimarisha huduma za simu na intaneti katika taasisi za umma zikiwemo shule, vituo vya afya, vituo vya polisi na ofisi za posta.

“Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kupanua matumizi yake hadi katika ngazi ya wilaya na kuzisimamia kampuni za simu nchini ili ziweze kutoa kumbukumbu sahihi kwa lengo la kukokotoa mapato yatokanayo na malipo ya huduma za simu za kitaifa na kimataifa,” alisema.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.