* Miradi mipya ya kisekta yatarajiwa kuzalisha ajira mpya 15,491
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania inaongoza kwa uwekezaji katika Afrika Mashariki na imeweza kuvutia uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.18, ikifuatiwa na Uganda dola za Marekani bilioni 0.7 na Kenya dola za Marekani bilioni 0.67.
“Kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuvutia uwekezaji nchini, hali ya uwekezaji imeimarika ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonesha kuwa Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 4, 2019) Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020 kwenye mkutano wa 15 wa Bunge.
Amesema Taarifa ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) ya mwaka 2018 inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) imebainisha kiasi hicho kikubwa cha uwekezaji.
“Taarifa nyingine ya“The Africa Investment Index (AII) 2018” inaonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 13 kati ya nchi 54 za Afrika katika kutoa fursa za masoko na vivutio vya uwekezaji.”
Vilevile, Waziri Mkuu amesema kuwa taarifa ya “Where to Invest in Africa” ya mwaka 2018, nayo imeonesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya saba kati ya nchi 52 zinazovutia zaidi kwa uwekezaji barani Afrika.
Kutokana na uwekezaji huo mkubwa, Waziri Mkuu amewataka Watanzania wachangamkie fursa zinazojitokeza kutokana na ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kijamii na pia uwekezaji wa sekta ya umma kwenye miundombinu kwa kuthubutu kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo kutekeleza mapendekezo ya Mpango Kazi Jumuishi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini. Pia itakamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji na Sheria ya Uwekezaji.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema uhamasishaji wa miradi ya kisekta ndani na nje ya nchi, umefanikisha kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali za kimkakati na unatarajia kuwekeza mitaji ya jumla ya dola za Marekani bilioni 1.84 na kuzalisha ajira mpya 15,491.
“Hadi kufikia Februari, 2019 jumla ya miradi mipya 145 ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Kati ya miradi hiyo, miradi 104 sawa na asilimia 72 inamilikiwa na wawekezaji wa ndani; miradi 38 sawa na asilimia 26 inamilikiwa na wawekezaji kutoka nje na miradi mitatu sawa na asilimia 2.01 ni ya ubia,” amesema.
Akizungumzia kuhusu zoezi la utoaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali imekusanya shilingi bilioni 9.9 tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo Desemba, 2018.
“Hadi tarehe 10 Machi 2019, jumla ya vitambulisho 496,221 sawa na asilimia 74 vilikuwa vimegawiwa kwa wajasiriamali wadogo katika mikoa yote nchini.” Amesema hatua hiyo ilichukuliwa ikiwa ni kutambua umuhimu wa wajasiriamali wadogo nchini katika kuchangia pato la Taifa na kukuza uchumi
“Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa vitambulisho 670,000 kwa ajili ya wajasiriamali wadogo ambao mitaji yao haizidi shilingi milioni nne. Lengo la kutoa vitambulisho hivyo vyenye kugharimu shilingi 20,000 kwa kila kimoja ni kuwatambua, kuwaandalia maeneo ya kufanya biashara bila usumbufu wowote na kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza mapato ya ndani,” amesema.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.