Tuesday, April 9, 2019

WAZIRI MKUU: MIFUKO YA PLASTIKI MWISHO JUNI MOSI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia Juni mosi mwaka huu, itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote na matumizi yake yatakoma ifikapo Mei 31, 2019.

“Hivi karibuni nimemwagiza Waziri anayesimamia masuala ya mazingira ikiwemo kuzungumza na wadau mbalimbali, ikiwemo wenye viwanda vya kutengeneza mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuhakikisha jambo hili linatekelezwa kwa haraka.”

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 9, 2019) Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

“Kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadilisha teknolojia, wauzaji kuondoa mzigo uliopo, Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hili kuwa na nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii ili kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki,” amesema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua kwamba kuna baadhi ya bidhaa lazima zifungwe kwenye vifungashio vya plastiki na kwamba vifungashio kwa bidhaa hizo havitapigwa marufuku.

“Kwa msingi huo, katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, yatatolewa maelezo ya kina kuhusu katazo la vifungashio vya aina hii, hasa katika maeneo ya uzalishaji viwanda, sekta ya afya, na kilimo,” amesema.

Amesema ana imani kuwa utaratibu huo pamoja na kutunza mazingira, utatoa fursa ya kutengeneza ajira nyingi husasan za watu wa chini kupitia utengenezaji wa mifuko mbadala ya plastiki pamoja na kutumia kikamilifu fursa ya viwanda vya karatasi vilivyopo nchini ikiwemo cha Mgololo.

Amesema matumizi ya plastiki nchini yameendelea kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo vya mifugo kwa kula plastiki, kuziba kwa mifereji, uchafuzi wa mazingira na kushindikana kwa kuozesha taka kwenye vituo vya kukusanya taka. 

Bunge lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/- kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2019/2020. Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 62,596,168,581/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile, Bunge liliidhinisha sh. 124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo 116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 7,609,511,600/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.