Tuesday, April 9, 2019

KITENGO CHA WATU WENYE ULEMAVU KUIMARISHWA: WAZIRI IKUPA


NA.MWANDISHI WETU
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu Wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha kitengo kinachoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu ili kuendana na mahitaji halisi nchini.
Ameyasema hayo hii leo Aprili 09, 2019 alipokuwa akijibu hoja Bungeni Dodoma ikiwa ni moja ya hoja iliyotolewa kuhusu uboreshwaji wa kitengo hicho ili kuendelea kuongeza nguvu katika kushughulikia mahitaji ya kundi hilo.
Naibu Waziri alieleza kuwa Ofisi yake imejipanga kuhakikisha inaboresha kitengo hicho kwa kuendelea kuwajengea uwezo watumishi na kuongeza watumishi watakaohudumia makundi hayo.
“Serikali imeoa ipo haja ya kuwajengea uwezo watumishi wa kitengo hiki wanaosimamia na kuratibu masuala ya watu wenye ulemavu ili kuongeza nguvu na kuboresha utendaji,”alisema Ikupa
Aliongezea kuwa, umuhimu wa kuongeza watumishi utasaidia kuendana na mahitaji halisi ya kundi hilo na kupunguza changamoto zilizopo kwa sasa.
Katika kuendelea kuboresha utekelezaji wa masuala hayo Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuandaa mazingira wezeshi ikiwemo kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa kwa Watu Wenye Ulemavu utakaosaidia kushughulikia masuala  ya ruzuku za vyama vya watu wenye ulemavu, kuwezesha programu za elimu na mafunzo, kuwezesha huduma za utengamavu kwa watu wenye ulemavu pamoja na kutumika katika tafiti mbalimbali.
“Kwa mwaka wa Fedha 2019/2020 jumla ya shilingi Milioni 103 zimetengwa kwa ajili ya Mfuko huo ambazo zitakuwa ni mbegu kwa mfuko hivyo ni vyema sasa kukawa na wadau wataochangia kutunisha mfuko huu,”alisisitiza Ikupa

Aidha, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa mamlaka mbalimbali kuhusu ujenzi wa miundombinu rafiki inayoendana na makundi ya watu wenye mahitaji maalum nchini ili kuondokana na changamoto za uwepo wa miundombinu isiyoendana na mahitaji halisi kwa kundi hilo.
”Suala la Miundombinu ni la kila mtu hivyo basi ni vyema tukahakikisha kunakuwa na ujenzi unaozingatia uhitaji wa wenye ulemavu ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza”, alisisitiza Ikupa

=MWISHO=


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.