Saturday, April 6, 2019

VIJANA WAPONGEZA SERIKALI KUWAJENGEA UWEZO KUHUSU KILIMO CHA KITALU NYUMBA


NA.MWANDISHI WETU
Wanufaika wa programu ya kukuza ujuzi eneo la kilimo cha kisasa kupitia teknolojia ya kitalu nyumba “green house” wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwawezesha katika masuala ya kilimo hicho na kujikwamua kiuchumi.
Pongezi hizo wamezitoa hii leo Aprili 06, 2019 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipotembelea kukagua utekelezaji wa Programu ya ukuzaji ujuzi kwa vijana katika Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma.
Katika kupongeza jitihada hizo wanufaika wa programu ya kilimo hicho walibainisha mafanikio ikiwemo, kupata ujuzi wa kilimo cha mazao mbalimbali, kujikwamua kiuchumi ikiwa ni sehemu ya kujipatia vipato halali pamoja na kusaidia upatikanaji wa ajira kwa vijana wanaowezeshwa elimu hiyo.
Mtaalam kutoka kampuni ya Holly green Bw. Octovian Lasway alieleza kuwa, zaidi ya vijana 100 wamenufaika na elimu ya kilimo cha kitalu nyumba katika Wilaya hiyo na kusaidia kuondokana na changamoto za ukosefu wa ajira nchini.
“Programu hii imekuja wakati sahihi na imesaidia kundi kubwa la vijana kwa kuzingatia mafanikio yatokanayo na kilimo hiki cha kisasa kinacholeta tija kwa kuwa na mazao bora na kuongeza kipato kwa wananchi,”alisisitiza Octovian.
Akitoa maelezo kwa wanufaika hao, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe.Anthony Mavunde alieleza jitihada za Serikali katika kufikia kundi kubwa la vijana katika kuwawezesha na kuwajengea uwezo wa masuala ya ukuzaji ujuzi ili kuendelea kuongeza tija na kujikwamua kiuchumi kwa kuzingatia falsafa ya uchumi wa viwanda.
“Mradi umekusudiwa kutekelezwa kwenye Halmashauri zote 185 Tanzania Bara ambapo awamu ya kwanza itafikiwa mikoa 12 na Halmashauri 83 kwa lengo la kuwezesha vijana kuwa na ujuzi pamoja na stadi za maisha  ili kufikia malengo tuliyojiwekea kama Serikali,”alieleza Mavunde
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ajira wa ofisi hiyo Bw.Ally Msaki alieleza kuwa, mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati ya Serikali katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na kuboresha kipato kwa watanzania.
“Mpango huu unalenga kufikia vijana 18800 nchi nzima ambapo kila Halmashauri itafikia vijana 100 na hadi sasa tumefikia halmashauri za mkoa 10, ikiwemo;Dodoma, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Lindi, Mwanza, Simiyu, Geita, Shinyanga na Kagera,”alieleza Msaki
Naye Makamu mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Nagma Giga alifurahishwa na utendaji na bidii ya vijana hao na kuwaasa kuendelea kutumia  ujuzi huo kwa vijana wengine nchini.
Naye Naibu Waziri wa Ofisi hiyo anayeshughulikia Watu Wenye Ulemavu Mhe.Stella Ikupa aliwataka vijana kutodharau kilimo kwa kuzingatia mchango wake katika kujikwamua kimaisha.
“Maisha hayapo kwenye karamu peke yake bali jembe linauwezo wa kuwatoa na kuwakwamua kiuchumi endapo kutakuwa na umakini na kujitoa kwa bidii,”alisisitiza Ikupa.
Kwa upande wake mwanagenzi Bw.Festo Ezikiel aliendelea kuipongeza serikali kuendelea kuwaamii na kuwajengea uwezo wa kilio cha kisasa cha kutumia kitalu nyumba.
“Tunaipongeza Serikali kutuamii na kutupa ujuzi kuhusu kilimo hiki nasi tunaahidi kushirikisha vijana wengine waliopo katika maeneo yetu ili kujikwamua kiuchumi,”alisema Ezekiel
=MWISHO=


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.