Tuesday, April 30, 2019

WAZIRI MKUU: SERIKALI IMETOA SH. BILIONI 118 KUIMARISHA MAWASILIANO


*Ahimiza wananchi walinde minara ya mawasiliano popote pale ilipo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema tangu Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote uanzishwe, Serikali imechangia shilingi bilioni 118 ili kuimarisha huduma za mawasiliano ambapo wakazi zaidi ya milioni tano kwenye kata 703 zenye vijiji 2,501 wameweza kufikiwa.

Ametoa kauli hiyo hilo leo (Jumanne, Aprili 30, 2019) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Dodoma waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya miaka 10 ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mwl. Nyerere, jijini Dodoma.

“Ninayo furaha kubwa moyoni mwangu, ninaposhuhudia mfuko huu ukitimiza miaka 10 huku sehemu kubwa ya nchi yetu ikiwa na mawasiliano ya uhakika. Napenda niwakikishie kwamba Serikali itaendelea kupeleka mawasiliano kwenye sehemu zilizobakia hapa nchini ili wananchi wote waweze kunufaika na uwepo wa mawasiliano,” amesema.

Amesema Serikali inatambua mchango wa watoa huduma za mawasiliano katika kufikisha huduma hiyo sehemu mbalimbali, kwani kwa sasa kuna baadhi ya minara imejengwa kwa ushirikiano baina ya kampuni za simu. “Nitoe rai kwa wananchi wahakikisha mnailinda minara ya mawasiliano, na tena mhakikishe popote ilipo inalindwa kwa mguvu zote ili tusirudishe nyuma juhudi za maendeleo,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ameipongeza Bodi na menejimenti ya mfuko huo kwa kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule zaidi ya 500 nchini pamoja na kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 800.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye alisema mfuko huo umejenga vituo 10 vya TEHAMA huko Zanzibar (Pemba na Unguja) ili viwe ni vituo vya mafunzo ya TEHAMA.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter Ulanga alisema mpaka sasa takribani asilimia 94 ya Watanzania wanapata huduma za mawasiliano mijini na vijijini.

“Kama unavyotambua kwa ukubwa wa nchi yetu, bado kuna maeneo yenye changamoto za mawasiliano. Mfuko umekwishaainisha jumla ya kata 234 ambazo zabuni yake inatarajiwa kutangazwa Mei 2019,” amesema.

Alisema Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote pamoja na kupeleka huduma za mawasiliano vijijini umeweza kuanzisha matumizi ya TEHAMA katika shule za msingi na sekondari nchini ikiwa ni utekelezaji wa majukumu yake kama yalivyoainishwa katika sheria iliyoanzisha mfuko huo.

“Katika kipindi cha miaka 10, Mfuko umeweza kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za Serikali. Kupitia mradi wake wa kuunganisha shule na mtandao wa Internet, mfuko huo umepeleka vifaa hivyo kwenye shule za serikali 503, ambapo kila shule ilipata kompyuta tano. Aidha, printa zaidi ya 150 zimeweza kutolewa katika shule za umma za msingi na sekondari, alisema Mhandisi Ulanga.
         
Alisema kupitia mradi wa kuunganisha shule za umma na mtandao wa internet, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano na kampuni ya Satelaiti ya Avanti Communications, imeweza kuunganisha shule 301 na mtandao wa internet.

Aidha, Mhandisi Ulanga alisema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa kushirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia umeweza kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 583 katika mwaka wa fedha 2017/2018 wa shule za umma kwa ajili ya kuufanya mradi wa kupeleka vifaa vya tehama uwe endelevu.

“Lengo hasa la mafunzo haya ni kutoa elimu ya kutatua matatizo ya awali katika vifaa mbalimbali vya TEHAMA, ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa vifaa vinavyopelekwa shuleni na kuboresha namna ya kuandaa na kufundisha masomo mbalimbali. Mwaka huu wa fedha 2018/2019 tumetoa mafunzo kwa idadi hiyo hiyo ya walimu,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kufanikisha mafunzo hayo.

(mwisho) 



EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.