Monday, April 15, 2019

TANZANIA YAKWANZA DUNIANI KUENDESHA MAFUNZO YA DHANA YA AFYA MOJA KWA NGAZI YA STASHAHADA NA ASTASHAHADA.

Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa mafunzo ya  Afya Moja katika kuwafundisha wanafunzi wa ngazi ya Stashahada na  Astashahada, mjini Morogoro tarehe 13 Aprili,

Na. OWM, MOROGORO.

Mtandao wa Afya moja kwa nchi za Afrika mashariki, Kati na Magharibi (OHCEA) umeendesha mafunzo ya Dhana ya Afya moja kwa wanafunzi wa ngazi ya Stashahada na Astashahada  kutoka vyuo vya kwenye sekta za Afya ya Binadamu, Mifungo, Wanyamapori na Mazingira. Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Duniani kufundisha Dhana hiyo katika ngazi hizo za taaluma,  kwa kuwa nchi nyingine  duniani hufundisha tu kwa ngazi ya Shahada na Shahada ya Uzamivu masuala ya  Afya moja.

Dhana ya Afya moja ambayo ni ushirikishwaji wa pamoja  sekta ya Afya ya Binadamu, Wanyamapori, Mifugo, Kilimo na  mazingira katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yatokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu ama kinyume chake. Wataalamu hao wamepata mafunzo hayo kwakuwa wapo karibu sana na jamii na  pindi utokeapo mlipuko wa ugonjwa ndio huwa kikosi kazi cha  kwanza na mstari wa mbele  kuwa eneo la tukio katika kufuatilia  na kukabili milipuko, kabla ya wataalamu wengine kushiriki kikamilifu.

Akiongea wakati wa kufunga Warsha ya kufanya tathmini ya namna wakufunzi wanavyotumia mitaala ya Afya Moja katika kuwafundisha wanafunzi wao wa ngazi ya Stashahada na  Astashahada, tarehe 13 Aprili, Mjini Morogoro, Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe alifafanua kuwa mafunzo hayo yanajenga kikosi kazi imara chenye kuchagiza shughuli za Afya moja hapa nchini.

“Katika kuimarisha Afya ya Binadamu pamoja na Afya ya mifugo na wanyamapori, kwa kutumia Dhana ya Afya moja, ninafarijika kwa  jitihada hizi za kuwajengea uwezo Wataalamu wa sekta za Afya katika ngazi ya Stashahada na Astashahada pamoja na wakufunzi wao, kwa kuwa tunaandaa rasilimali watu ya kuweza kuwa na uwezo wa kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa kwa Dhana ya Afya moja. Alisema Matamwe.

Wakiongea kwa nyakati tofauti waratibu wa mafunzo hayo  Profesa; Japheti Killewo na Profesa. Robinson Mdegela walifafanua kuwa tayari mitaala ya Afya moja kwa ngazi ya stashahada na astashahada imekamilika, lakini wakati taratibu za kuingiza  masuala ya Afya moja zitakamilika hivi karibuni katika mitaala ya ngazi  ya stashahada na Astashahada wameamua kufanya mafunzo hayo ili wakufunzi kujifunza kwa vitendo juu ya kufundisha masuala ya Afya moja lakini pia na kuwaandaa wanafunzi watakao fundishwa  kwa kutumia mitaala hiyo.

Aidha waratibu hao walibainisha kuwa wanafunzi hao wakiweza kuielewa vizuri dhana ya Afya moja watatumika vyema kuielimisha jamii juu ya masuala ya Afya Moja,  na nchi yetu itaweza kuzuia maambukizi ya magonjwa ya mlipuko hususani yale yatokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu na pia kupunguza usugu wa madawa kwa sababu wataweza kuongeza ushirikiano, mawasiliano na uratibu baina ya sekta husika.

Mafunzo hayo  yaliyowajumuisha zaidi ya wanafunzi 210, wa ngazi ya astashahada na ngazi ya cheti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili, SUA, Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Morogoro, Chuo cha Afya cha Kilosa, Chuo cha Wanyamapori Pasiansi na Chuo cha Wanyamapori Mweka,

Aidha,  wakufunzi zaidi ya 30 wameshiriki kutoka Chuo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine, Vyuo vya Afya Lindi, Mafinga, Kilosa, Mtwara, Singida, Kagemu, Mirembe, Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Morogoro, Temeke, Tengeru, Buhuri, pamoja na Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori , Pasiansi na Mweka.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Chuo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili  na Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine kwa kushirikiana na USAID, kupitia vyuo vikikuu vya  MINNESOTA na Tufs vya nchini Marekani
MWISHO.


Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akisistiza jambo wakati wa kufunga Warsha ya kufanya tathmini ya namna wakufunzi wanavyotumia mitaala ya Afya Moja katika kuwafundisha wanafunzi wao wa ngazi ya Stashahada na  Astashahada, mjini Morogoro tarehe 13 Aprili.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa mafunzo ya  Afya Moja katika kuwafundisha wanafunzi wa ngazi ya Stashahada na  Astashahada, mjini Morogoro tarehe 13 Aprili.
Baadhi ya Waratibu wa Warsha ya kufanya tathmini ya namna wakufunzi wanavyotumia mitaala ya Afya Moja katika kuwafundisha wanafunzi wao wa ngazi ya Stashahada na  Astashahada, mjini Morogoro tarehe 13 Aprili, kulia ni Mratibu kutoka  Chuo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili,  Profesa Japhet Killewo na kushoto ni Mratibu kutoka Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine, Profesa. Robinson Mdegela, katikati ni Rasi wa Ndaki ya Tiba za Wanyama na Sayansi za Afya Chuo kikuu Sokoine.  
Baadhi ya wanafunzi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe (hayupo pichani) wakati wa kufunga Warsha ya kufanya tathmini ya namna wakufunzi wanavyotumia mitaala ya Afya Moja katika kuwafundisha wanafunzi wao wa ngazi ya Stashahada na  Astashahada, mjini Morogoro tarehe 13 Aprili.
Mratibu kutoka  Chuo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili,  Profesa Japhet Killewo akisisitiza jambo wakati wa kufunga Warsha ya kufanya tathmini ya namna wakufunzi wanavyotumia mitaala ya Afya Moja katika kuwafundisha wanafunzi wao wa ngazi ya Stashahada na  Astashahada, mjini Morogoro tarehe 13 Aprili.
Mratibu kutoka Chuo Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine,  Profesa Robinson Mdegela akisisitiza jambo wakati wa kufunga Warsha ya kufanya tathmini ya namna wakufunzi wanavyotumia mitaala ya Afya Moja katika kuwafundisha wanafunzi wao wa ngazi ya Stashahada na  Astashahada, mjini Morogoro tarehe 13 Aprili
Baadhi ya wanafunzi wa ngazi ya Stashahada na  Astashahada wa sekta za Afya ya Binadamu , wanyamapori, mifugo, kilimo na Mazingira wakifuatilia warsha ya kufunga mafunzo hayo ya  Afya Moja, mjini Morogoro tarehe 13 Aprili.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.