Monday, June 18, 2018

KILIMO CHA PAMBA KUNOGESHA MAPINDUZI YA VIWANDA

*Ni kutokana na juhudi za Serikali za kuhamasisha kilimo cha pamba 


 ZAO la pamba ni miongoni mwa mazao makubwa ya biashara yaliyokuwa yakiliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni na kuchangia kukuza uchumi wa wananchi miaka ya 1970.

Kwenye miaka ya 1970 kulisheheni vyama vingi vya ushirika wa zao la Pamba na viwanda vya kuchambua nyuzi na kukamua mafuta, ambavyo vilibadili  hali halisi ya kipato cha wananchi wa eneo linalolimwa zao hilo na kulifanya kujulikana kama dhahabu nyeupe.
Kilimo hicho kilianza kudorora miaka ya hivi karibuni kutokana na kulegalega kwa vyama vya ushirika na matokeo yake pamba iliuzwa ikiwa chafu bila kuzingatia ubora  na madaraja yaliyopo.
Kutokana na sababu hizo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, iliamua kufufua zao hilo ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi ya viwanda vya nguo na mafuta yatokanayo na mbegu za pamba zinapatikana pamoja na kuinua uchumi wa wakulima nchini.
Katika kufanikisha suala hilo Serikali ilianza kwa kuwaagiza viongozi wa mikoa yote inayolima pamba kuhakikisha wanawahamasisha wakulima kufufua mashamba yao na ilihakikisha inafuatilia jambo hilo kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba, ugawaji wa pembejeo hadi utafutaji wa masoko.

Baada ya kutoa agizo hilo ambalo lilifanyiwa kazi na tayari mafanikio yameanza kuonekana katika msimu wa mwaka huu, kwa wakulima  kuanza kuvuna na kuuza kwa mafanikio.

Akizungumzia kuhusu hali ya zao hilo mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella, anasema msimu wa mwaka huu umekuwa na mafanikio makubwa kutokana na hamasa iliyotolewa na viongozi wakuu wa Serikali.

Bw. Mongella anasema kutokana na hamasa hiyo, mwaka huu wanatarajia kupata mavuno makubwa kutoka katika kilimo  hicho kwa sababu wakulima wengi wamelima na baadhi yao tayari wameshaanza kuvuna.

Anasema Rais Dk. Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, walitoa maelekezo mahususi na walifanya ufuatiliaji wa karibu wa kilimo cha mazao makuu matano ya biashara nchini, likiwamo na zao la pamba.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya zao hilo jijini Mwanza hivi karibuni, Bw. Mongella amesema zao la pamba litasaidia kufufua viwanda vya mafuta ya kula, nguo pamoja na kuongeza ajira.

Amesema baada ya Rais Dkt. Magufuli kuhamasisha kilimo cha zao hilo, ambacho kilianza kusuasua nchini, viongozi waliitikia na kuwahimiza wakulima wachangamkie fursa hiyo, ambao walikubali.

“Tunashukuru kwa hamasa na miongozo iliyotolewa na viongozi wetu kwa sababu iliongeza ari kwa wakulima kulima zao la pamba kwa wingi na mwamko kwa wananchi kulima mazao mengine, likiwamo la mpunga,” anasema.

Hata hivyo, kiongozi huyo ameishukuru Serikali kwa kuagiza pamba itakayovunwa iuzwe kupitia minada itakayosimamiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) katika kila eneo, jambo ambalo limesaidia  kufufuka kwa vyama hivyo.

“Tunashukuru kwa maelekezo na miongozo iliyokuwa inatolewa na viongozi wetu wakuu. Sasa AMCOS zetu zimefufuka na huu ni mwanzo tu mapinduzi makubwa katika biashara ya zao la pamba na yajayo yanafurahisha zaidi,” anasisitiza Bw. Mongella.

Bw. Mongella anatarajia kuwahamasisha wakulima wote wa mkoa huo pamoja na wafugaji na wavuvi wajiunge katika AMCOS zilizoko katika maeneo yao, ili kuweza kuirahisishia Serikali kufanyanao kazi.

Mkuu huyo wa mkoa pia anatumia fursa hiyo kuwapongeza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maofisa Kilimo kuanzia ngazi ya wilaya hadi kijiji na wakulima kwa kuhakikisha kilimo cha zao la pamba kinapata mafanikio.

Bw.Mongella anaamini ushirikiano wao kupitia vikosi kazi mbalimbali vilivyoundwa kuanzia ngazi ya mkoa ambapo alikuwa Mwenyekiti watendaji hao walitoa ushirikiano mkubwa ulichangia mafanikio ya zao hilo.

Hata hivyo, Bw. Mongella amewashauri wakulima watumie taasisi za kifedha kuhifadhi fedha zao na wajijengee nidhamu ya matumizi, ambayo itawapa fursa ya kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo, ikiwa pamoja kujenga nyumba bora.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza, Bw. Juma Sweda anasema anaishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kulifufua zao hilo pamoja na kuwahamasisha wananchi kulima na kutoa maelekezo ya uuzwaji wake.
“Naishukuru Serikali kwani baada ya kuwahamasisha ufufuaji wa kilimo cha zao la pamba nasi tuliungana na wananchi kuhakikisha maelekezo hayo tunayatekeleza kwa vitendo, lengo letu kubwa ni kuona zao hili linarudi kama zamani.

‘’Mbali na kuwahamasisha wananchi kulima zao la pamba, pia Watumishi wa Halmashauri  nao wamelima jumla ya ekari 306 za zao la pamba kwenye kijiji cha Ikoma katika Kata ya Kijima. Mashamba yaliongeza hamasa kwa wananchi,’’ anasema Sweda.

Bw. Sweda anasema kabla ya wakulima kuanza kuanda mashamba ya kilimo cha pamba, Wilaya ya Misungwi yenye vjjiji 113 ilitoa mafunzo kwa wakulima wawili kila kijiji, ambao wameshirikiana na vikosi kazi vya vijiji husika na Maafisa Ugani kusimamia kilimo cha zao hilo.

Anasema kwa sasa wapo katika hatua ya uvunaji na uuzaji, ambapo wamejipanga kukagua kikamilifu ili kuona zoezi hilo linaenda vizuri na pamba yote inayopokelewa na vyama vya ushirika ni ile iliyo katika ubora unaohitajika.

Anasema baada ya Serikali kuhamasisha kilimo cha zao la pamba kwa mikoa yote inayolima zao hilo, pia iliagiza kuanzishwa kwa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) katika maeneo yote, ambapo AMCOS 50 zilianzishwa wilayani Misungwi.

Bw. Sweda anasema AMCOS zimesaidia kuimarisha ubora wa pamba, ambapo viongozi wake hukagua pamba kabla ya kuipokea na iwapo mkulima atabainika kupeleka pamba chafu hulazimika kuisafisha kwanza kwa kutenga safi pembeni kabla ya kupima na kulipwa. 

Mkuu huyo wa Wilaya anaongeza kuwa, mbali na kukagua usafi na ubora wa pamba ili kuhakikisha hakuna pamba chafu inayouzwa, pia wanasimamia zoezi la malipo kwa wakulima na kwamba wanaouza wote wanalipwa hapo hapo na ni marufuku mnunuzi kumkopa mkulima.

Pia, anasema wilaya yao imeanzisha mikakati mbalimbali ya kutoa motisha kwa Maafisa Kilimo na wakulima waliofanya vizuri, ambapo hutoa zawadi za pikipiki kwa mkulima na afisa aliyeongoza katika kata yake.

Anaongeza kuwa Maafisa Kilimo Wasaidizi wapo nchini Brazil kwa mafunzo ya miezi mitatu, ambapo wanajifunza namna ya kilimo bora cha zao la pamba. Viongozi hao ambao ni John Choto, Haika Kimambo na Bahati Mchele walichaguliwa kuhudhuria mafunzo hayo baada ya kuonyesha jitihada kubwa katika kusimamia zao hilo.

Mkuu huyo wa wilaya anasema wilaya ina Maafisa Ugani 90 ambao wamesambazwa kuanzia wilayani hadi vijiji, lengo likiwa ni kupata nafasi ya kusimamia vizuri na kwa ukaribu zao la pamba.

Anasema wilaya ina jumla ya kata 27 ambapo Maafisa Kilimo wake wote walipatiwa pikipiki ili ziwawezeshe kuwafikia wakulima kwa urahisi na kuwahudumia kwa wakati lakini atakayeshindwa kuwajibika atanyang’wanywa pikipiki.

Sambamba na hayo, Bw. Sweda aliwashauri wakulima kutumia vizuri fedha wanazozipata baada ya kuuza mazao yao. Anasema ni vema wakatumia fedha hizo kujiletea maendeleo katika familia zao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bora za kisasa na kuwaendeleza watoto wao kielimu.

Anasema kwa sasa wapo katika hatua ya uvunaji na uuzaji, ambapo wamejipanga kukagua kikamilifu ili kuona zoezi hilo linaenda vizuri na pamba yote inayopokelewa na vyama vya Ushirika ni ile iliyo katika ubora unaohitajika.

Anasema viongozi wa Vyama vya Msingi vya AMCOS, hukagua pamba kabla ya kuipokea na iwapo mkulima atabainika kupeleka pamba chafu hulazimika kuisafisha kwanza kwa kutenga safi na chafu ndipo hupima na kulipwa.

Mkuu huyo wa wilaya anaongeza kuwa zao la pamba mbali ya kuwapatia wakulima kipato, pia litaimarisha hali ya usalama wa chakula kwa sababu fedha watakayoipata baada ya kuuza pamba itawawezesha kumudu ununuzi wa mahitaji mengine katika familia na hawatouza vyakula walivyonavyo.

Hata hivyo, Bw. Sweda aliwaomba wadau wa sekta binafsi wasaidie katika kuliongezea thamani zao hilo kwa kufanya uwekezaji mkubwa wa viwanda vya nyuzi, nguo na vya kukamua mafuta ya pamba badala ya kuuza malighafi.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Kata ya Mondo, Bw. Sebastian Mbandi anasema mafanikio ya zao hilo kwa mwaka huu ni makubwa ukilinganisha na miaka iliyopita, hata hivyo wameshindwa kufika lengo walilojiwekea kutokana na mazao mengi kushambuliwa na wadudu aina ya thrips.

Bw. Mbandi anasema walitarajia kuvuna wastani wa tani 1.5 kwa ekari moja lakini kutokana na changamoto ya ugonjwa iliyosababishwa na mdudu huyo wanatarajia kuvuna wastani wa kilo 800 kwa ekari hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia wakulima kwa kuwatafutia dawa itakayowawezesha kupambana na thrips msimu ujao.

Kwa upande wao, wakulima wakizungumza kwa nyakati tofauti, walitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dk. Magufuli kwa kuhamasisha wananchi walime zao la pamba, ambapo nao waliitikia wito huo na sasa wameanza kuona mafanikio.

Miongoni mwa wakulima hao ni pamoja na Bw. Hoja Ngole mkazi wa Kijiji cha Mondo ambaye amelima ekari sita na tayari ameshavuna na ameenda kuuza na anatarajia kutumia fedha atakazozipata kwa kujenga nyumba ya kisasa.

Bw. Ngole na mkewe Bibi Sara waliahidi kuongeza ukubwa wa shamba katika msimu ujao na wamewaomba wananchi wengine kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo kwa kuwa ni mkombozi wa maisha yao.   ’’Tumehamasika kuongeza ukubwa wa shamba baada ya Waziri Mkuu kututembelea na tunataka akija tena akute tumebadilika, tuwe na nyumba bora,’’ anasema. 
Mkulima mwingine,mkazi wa kijiji cha Mondo Bw. Michael Masalamunda ambaye alikuwa amepeleka pamba yake katika kituo cha mauzo cha Mwanimo AMCOS amesema anatarajia kutumia fedha atakazozipata baada ya mauzo hayo kwa kuongeza mtaji wa biashara ya ng’ombe.

Bw. Masalamunda naye amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuwahamasisha walime zao la pamba pamoja na na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye naye aliwahamasisha na kufuatilia maendeleo ya zao hilo.
Mkulima huyo anaishukuru Serikali kwa kuagiza mauzo ya zao hilo yasimamiwe na vyama vya ushirika kwa sababu vimewezesha wakulima kuwa na soko la uhakika la pamba yao na wakiuza tu wanalipwa fedha zao hakuna anayekopwa. “Mimi leo nakuja kuuza kwa awamu ya pili na fedha zote nimelipwa.”

Naye mkulima mwingine, mkazi wa kijiji cha Maganzo Bw. Swalala Nteminyanda anaiomba Serikali kuwatafutia dawa nzuri itakayoweza kuwaangamiza wadudu aina ya thrips ambao wameonyesha usugu baada ya kupuliziwa dawa mbalimbali bila ya kufa.

Nteminyanda pia anawashauri wakulima wenzie wafuate maelekezo yanayotolewa na Maafisa ugani wanaowatembelea katika mashamba yao ili waweze kupata mavuno mengi na yenye viwango vya ubora vinavyotakiwa. Mkulima huyo amelima ekari saba na anatarajia kujenga nyumba bora kwa fedha atakazozipata.

Kwa upande waowanunuzi wa zao hilo wanaishukuru  Serikari kwa kuweka mfumo mzuri wa ununuzi wa zao hilo, ambalo kwa mwaka huu linauzwa kupitia katika minada inayosimamiwa na AMCOS.

Miongoni mwa wanunuzi hao ni pamoja Meneja Mkuu wa Kampuni ya NGS Investment LTD, Bw. Emmanuel Dandu alipokuwa akizungumzia kuhusu kuanza kwa uchambuaji wa pamba kwa msimu wa mwaka huu.

Bw. Dandu ambaye kampuni yao ya NGS Investment LTD, licha ya kujishughulisha na biashara nyingine, pia inamiliki kiwanda cha kuchambua pamba cha Majahida kilichopo wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, ambayo tayari imeshaanza zoezi ya uchambuaji pamba.

Anasema pamba inayochambuliwa katika kiwanda hicho wanainunua kupitia AMCOS walizopangiwa, ambapo alipongeza mfumo huo kwa sababu unawawezesha kupata malighafi kwa urahisi na kwa wakati.

“Wanunuzi wote tunanunua pamba kupitia AMCOS. Serikali imeweka mfumo mzuri unaotuwezesha wote kununua pamba kadiri ya uwezo wetu. AMCOS zimeagizwa kuuza pamba kwa wanunuzi wote bila ya ubaguzi, tofauti na miaka ya nyuma” anasema Bw. Dandu.
  
Anasema awali kabla pamba haijaanza kuuzwa kupitia AMCOS suala la ubora lilikuwa halizingatiwi sana na wakulima kwani  pamba yake ikikataliwa na kampuni moja alikuwa na uhuru wa kuipeleka kwenye kampuni nyingine jambo ambalo lilichangia kuishusha thamani.

Hata hivyo, wanunuzi hao wanaiomba Serikali kuziwezesha AMCOS kuwa na maghala makubwa na ya kisasa ya kuhifadhia pamba, lengo likiwa ni kuhakikisha pamba inahifadhiwa kwenye maeneo salama na kuifanya isipoteze ubora.

Mbali na maombi hayo, pia wameiomba Serikali kuwajengea uwezo viongozi wa Ushirika ili waweze kutekeleza majuku yao kikamilifu na pia isaidie kutoa elimu kwa wanachama juu ya umuhimu na faida za AMCOS ili wakulima wengi waweze kujiunga.

Akizungumzia kuhusu uwezo wa kiwanda hicho, anasema kina uwezo wa kuchambua tani 40,000 za pamba kwa mwaka, lakini wanalazimika kuchambua wastani wa tani tano  hadi 12 kutokana na changamoto ya upatikanaji wa pamba ya kutosha pamoja na changamoto ya umeme wa uhakika.

Pia anaiomba Serikali iwasaidie wakulima kwa kuwapatia pembejeo kwa wakati pamoja na kuwapa elimu ya mara kwa mara juu ya kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha zao la pamba, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa wakati ili waweze kujiongezea tija.

Anasema kwa sasa kiwanda hicho kina jumla ya wafanyakazi 300, ambao kati yao 62 ni waajiriwa wa kudumu na waliosalia ni vibarua. 

Bw. Dandu anasema marobota yanayotengenezwa kiwandani hapo yanakuwa na uzito wa kilo 200 hadi 220, huku wateja wao wakubwa ni Cotton Distributors Inc (CDI) ya nchini Uswisi, Saurashtra Cotton and Agro Product PVT LTD ya nchini India.

Wengine ni Awatac Impex PTE LTD ya nchini Singapore pamoja na viwanda vya nguo vya ndani ya nchi kikiwemo cha Mwatex cha jijini Mwanza. Alisema matarajio ya kampuni hiyo ni kuanzisha kiwanda cha kutengeza nyuzi ili kuongezea thamani ya pamba kabla ya kuiuza.

Aidha, Meneja huyo anasema mbegu zinazopatikana baada ya pamba hiyo kuchambuliwa zinapelekwa moja kwa moja katika kiwanda cha kukamua mafuta ya kula na mashudu huuzwa kama chakula cha mifugo na mabaki yanayopatikana baada ya mafuta kuchujwa, anasema yanatumika kwa kutengeneza sabuni za kufulia, ambazo wanaziuza kwa wananchi. 


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.