Monday, June 11, 2018

WANAMISUNGWI TUMIENI VIZURI FEDHA ZA PAMBA-DC


MKUU wa wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, Bw. Juma Sweda amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanatumia vizuri fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya zao la pamba.

Amesema ni vema wakatumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo katika familia zao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bora na za kisasa na wawaendelea watoto kielimu.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 11, 2018) wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua shughuli za uvunaji na uuzaji wa zao la pamba. Ziara hiyo imefanyika kwenye vijiji vitatu vya kata ya Mondo wilayani hapa.

Bw. Sweda amesema wananchi wengi walihamasika kulima zao la pamba baada ya Serikali kuhamasisha walime na kuahidi kulifuatilia kuanzia hatua za utayarishaji wa mashamba hadi utafutaji wa masoko.
“Naishukuru Serikali kwani baada ya kuhamasisha ufufuaji wa kilimo cha zao la pamba nasi tuliungana na wananchi kuhakikisha maelekezo hayo tunayatekeleza kwa vitendo, lengo letu kubwa ni kuona zao hilo linarudi kama zamani,” amesema.

Amesema kwa sasa wapo katika hatua ya uvunaji na uuzaji, ambapo wamejipanga kukagua kikamilifu ili kuona zoezi hilo linaenda vizuri na pamba yote inayopokelewa na vyama vya Ushirika ni ile iliyo katika ubora unaohitajika.

Amesema viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) hukagua pamba kabla ya kuipokea na iwapo mkulima atabainika kupeleka pamba chafu hulazimika kuisafisha kwanza kwa kutenga safi na chafu ndipo hupima na kulipwa. 

Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa, mbali na kukagua usafi, pia wanasimamia zoezi la malipo kwa wakulima na kuhakikisha kwamba wanaouza pamba wote wanalipwa hapo hapo na ni marufuku mnunuzi kumkopa mkulima.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Kata ya Mondo, Bw. Sebastian Mbandi amesema mafanikio ya zao hilo kwa mwaka huu ni makubwa ukilinganisha na miaka iliyipita, hata hivyo wameshindwa kufikia malengo waliyojiwekea kutokana na mazao mengi kushambuliwa na wadudu aina ya thrips.

Bw. Mbandi amesema walitarajia kuvuna wastani wa tani 1.5 kwa ekari moja lakini kutokana na changamoto ya ugonjwa iliyosababishwa na mdudu huyo wanatarajia kuvuna wastani wa kilo 800 kwa ekari. 

Kwa upande wao, wakulima ambao walizungumza kwa nyakati tofauti, walitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kuhamasisha wananchi walime zao la pamba, ambapo nao waliitikia wito huo na sasa wameanza kuona mafanikio.

Miongoni mwa wakulima hao ni pamoja na Bw. Hoja Ngole mkazi wa Kijiji cha Mondo ambaye amelima ekari sita na tayari ameshavuna na leo ameenda kuuza na anatarajia kutumia fedha atakazozipata kwa kujenga nyumba ya kisasa.

Bw. Ngole na mkewe Bibi Sara wameahidi kuongeza ukubwa wa shamba katika msimu ujao na wamewaomba wananchi wengine kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo kwa kuwa ni mkombozi wa maisha yao.

Naye,mkulima mwingine Bw. Michael Masalamunda ambaye alikuwa amepeleka pamba yake katika kituo cha mauzo cha Mwanimo AMCOS amesema anatarajia kutumia fedha atakazozipata baada ya mauzo hayo kwa kuongeza mtaji wa biashara ya ng’ombe.

Bw. Masalamunda naye amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuwahamasisha walime zao la pamba pamona na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye naye aliwahamasisha na kufuatilia maendeleo ya zao hilo.
Pia ameishukuru Serikali kwa kuagiza mauzo ya zao hilo yasimamiwe na vyama vya Ushirika kwa sababu vimewezesha wakulima kuwa na soko la uhakika la pamba yao na wakiuza tu wanalipwa fedha zao hakuna anayekopwa. “Mimi leo nakuja kuuza kwa awamu ya pili na fedha zote nimelipwa,”.


Attachments are


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.