Saturday, June 23, 2018

MITANDAO ISITUMIKE KUKWAMISHA SHUGHULI ZA SERIKALI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza mifumo ya utoaji huduma Serikali kwa njia ya mitandao isitumike kukwamisha shughuli za Serikali au mipango ya utoaji huduma kwa wananchi.

Amesema watakaobainika kuhujumu mifumo hiyo wachukuliwe hatua za kinidhamu na amesisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haitawavumilia watumishi wasio waadilifu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Juni 23, 2018) mara baada ya kuzindua mifumo tisa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dodoma.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2018 iliyotolewa na Umoja wa Afrika (AU) ni  “Mapambano dhidi ya Rushwa kwa kushirikisha wadau na kujenga uongozi bora ili kufikia Malengo ya Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na Malengo ya Maendeleo Endelevu”.

Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watumishi wa Umma wote nchini, wananchi, Sekta Binafsi, Sekta ya Umma, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kisiasa na Wadau mbalimbali,  kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa.

“Hii ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo Malengo ya Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika (AU) na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030 ya Umoja wa Mataifa  ambayo yamehimizwa na Kaulimbiu ya mwaka huu,”.

Pia Waziri Mkuu amewaagiza Watendaji  Wakuu wa Taasisi zinazosimamia mifumo hiyo pamoja na maafisa waliopewa dhamana ya kuwahudumia wananchi kupitia mifumo hiyo, wahakikisha wanailinda na kuitumia vema ili iweze kuwa na tija na manufaa yaliyokusudiwa.

Mifumo hiyo aliyoizundua inahusu utoaji Huduma Serikalini ambayo ni Mfumo wa Usajili wa Vizazi na Vifo, Mfumo wa Taarifa za Kitabibu, Mfumo wa Taarifa za Ununuzi, Mfumo wa Kumbukumbu za Kielektroniki na Mfumo wa Ofisi Mtandao.

Mingine ni Mfumo wa Ankara Pepe na Ulipaji wa Serikali, Mfumo wa Utoaji Huduma za Serikali Kupitia Simu za Mikononi, Mfumo wa Barua Pepe wa Serikali na Mfumo wa Vibali vya Kusafiri.

Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali la kutumia mifumo ya TEHAMA ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku.

“Hivyo basi, mtakubaliana nami kuwa, Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kutekeleza kwa vitendo azma ya kuwapatia wananchi hususani wa vijijini huduma bora na kwa wakati,” amesema.

Kwa upande wa wananchi,Waziri Mkuu amewataka  waendelee kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejipambanua kwa vitendo pamoja na kuwa na dhamira ya dhati ya kutoa huduma bora kwa wananchi wake.

Uzinduzi huo umehudhuliwa na waziri wa nchi, ofisi ya raisi menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Bw. George Mkuchika, waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji Charles Mwijage, naibu waziri Ujenzi, Uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye, na naibu waziri wa nchi OR-TAMISEMI Josephat Kakunda, wabunge, muwakilishi wa benki ya dunia, makatibu wakuu, watendaji na viongozi wa taasisi za umma.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.