Friday, June 8, 2018

WAZIRI MKUU ATAKA WANAOTOA TAARIFA ZA UONGO WADHIBITIWE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wawachukulie hatua kali wananchi wote wanaotumia vibaya namba za mawasiliano za jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu matukio ya majanga ya moto.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini kuendelea kutoa mafunzo kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na kupambana na majanga ya moto pindi yanapotokea katika maeneo yao.

Pia ameziagiza Halmashauri zote nchini kuwa na magari ya zimamoto pamoja na magari ya kubeba wagonjwa kwenye vituo vyote vya Zimamoto na Uokoaji katika maeneo yao.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Juni 8, 2018) wakati alipofanya ziara katika Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura ya Maafa pamoja na Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha mkoa wa Ilala.

Amesema ili kudhibiti wananchi wanaopiga simu za kuomba msaada wa kutaka kuokolewa, huku kukiwa hakuna tukio lolote la janga la moto lililotokea kwenye maeneo yao, ni vema watu hao wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,  Thobias Andengenye kumweleza baadhi ya changamoto zinazolikabili jeshi hilo kuwa ni pamoja na wananchi kupiga simu wakidai kuna ajali ya moto imetokea katika maeneo yao na baada watu wa uokoaji kufika wanabaini ni uongo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu aziagiza Halmashauri zote nchini kuwa na magari ya zimamoto pamoja na ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya kutoa huduma pindi majanga yanapotokea kwenye maeneo yao ili kuharakisha utoaji wa huduma za dharura.

Pia amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kila Mtanzania aweze kuwa na uelewa wa kutoa huduma za awali pindi majanga ya moto yanapotokea katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vya kuzima moto.

Waziri Mkuu ambaye alitembelea kituo cha Jeshi la Zimamoto cha Ilala amejionea magari ya kuzimia moto likiwemo la aina ya Bronto Sky Lift lenye uwezo wa kufika futi 54 na kuzunguka nyuzi 360. 

Alielezwa kuwa katika Bara la Afrika, magari ya aina hiyo yapo matatu tu, ambayo yapo nchini Tanzania, Misri na Afrika Kusini. Kwa upande wa Tanzania, gari hilo lilinunuliwa miaka 10 iliyopita kwa sh. bilioni 1.5. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitembelea Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura ya Maafa, ambapo aliwasisitiza viongozi wa kituo hicho kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara yatokanayo na kuishi kwenye maeneo hatarishi hususan mabondeni.

Waziri Mkuu alisema licha ya kuwapa elimu, pia wanatakiwa kuwashawishi wakazi wa maeneo hayo kuondoka kabla ya kutokea kwa maafa badala ya kusubiri majanga yatokee. Pia aliwataka wawe na mpango wa kuonesha eneo lenye maafa na kuujulisha umma.

Pia aliwataka watendaji wanaohusika na kamati za maafa waimarishe mawasiliano katika ngazi zote kuanzia ya kijiji hadi Taifa na wafanye kazi kwa ushirikiano ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi pindi maafa yanapotokea.

Awali, Waziri Mkuualitembelea Ofisi za Mpiga Chapa wa Serikali jijini Dar es salaam ambapo mbali na mambo mengine alijionea moja kati ya mitambo ya kwanza ya Mpiga  Chapa wa Serikali uitwao  Original Heidelberg wenye zaidi ya miaka 100 ambao bado unafanya kazi vizuri.  


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.