Friday, June 8, 2018

WAZIRI MKUU AZINDUA MAABARA YA KUPIMA MADINI

*Ni ya kwanza Afrika, inauwezo wa kutambua aina za madini na yalikotoka
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua maabara ya kisasa ya na ya kwanza barani Afrika yenye uwezo wa kupima na kutambua aina mbalimbali za madini.

Amesema maabara hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya umiliki wa madini na kudhibiti utoroshwaji wa madini mbalimbali kati ya nchi moja na nyingine.

Maabara hiyo imefunguliwa leo (Ijumaa, Juni 8, 2018) katika Kituo cha Madini na Jiosayansi  cha Afrika  (AMGC) kilichopo Kunduchi jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema uzinduzi wa maabara hiyo utawezesha wataalamu kutambua aina za madini na nchi yanakotoka, hivyo kuondoa migogoro ya umiliki wake. 

“Maabara hii litatuweza kulinda madini yetu na kufanya biashara ya madini vizuri. Pia hii ni fursa nzuri kwa nchi za Afrika kutumia maabara hii kupima madini yao na kubaini yalikotoka,” amesema.

Hata hivyo Waziri Mkuu amewataka viongozi wa kituo hicho kuhakikisha wanaziwesha nchi wanachama kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya madini pindi zinapohitaji.

Pia Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kusaidia katika ununuzi wa vifaa vya maabara hiyo pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu watakaoiendesha.

Waziri Mkuu, pia ameiomba Serikali hiyo kutoa mafunzo hayo kwa Watanzania wengi zaidi ili kuongeza idadi ya wataalamu wa kuendesha maabara hiyo.

Pia, Waziri Mkuu amefungua Mkutano 38 wa Mawaziri wa Madini kutoka nchi Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu unaofanyika katika kituo cha AMGC.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ikiwa ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama zilizosheheni wanyama wa aina mbalimbali pamoja na fukwe za bahari.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.