Tuesday, June 5, 2018

WAZIRI MKUU AWASISITIZA WABUNGE WADUMISHE MSHIKAMANO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasisitiza wabunge waendelee kudumisha  mshikamano ili Tanzania iendelee kuwa nchi tulivu na yenye amani.

Amesema mshikamano na upendo walionao wabunge hao ni vema wakauendeleza ili waweze kutekeleza shughuli zao za kuishauri Serikali.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumanne, Juni 5, 2018) katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma wakati wa futari aliyowaandalia wabunge. Futari hiyo ilihudhuriwa na wabunge wa vyama vyote.

"Mshikamano na upendo huu tuliouonesha kuanzia mwanzo wa mkutano wa Bunge naomba tuudumishe ili tuweze kuishauri vizuri Serikali na tufikie malengo tuliyojiwekea,” alisema. 

Naye,Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alitoa neno   la shukurani kwa niaba ya wabunge wote alimshukuru Waziri Mkuu kwa heshima aliyowapa.

"Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, hii heshima uliyotupa ni kubwa, kualikwa na wewe si jambo dogo si kila mtu anaweza kupata nafasi hii," alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mgogoni, Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf ambaye alisoma dua alisema watu wanatakiwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai aliowapa.

“Kuna wenzetu tulioshirikiana nao kwenye mfungo wa Ramadhani mwaka uliopita lakini leo hatunao sababu wametangulia mbele ya haki, hivyo sisi tunatakiwa tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai aliotupa,” alisisitiza.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.