Sunday, November 24, 2019

SEKTA ISIYO RASMI KUONGEZEWA TIJA-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali zote mbili (Jamhuri ya Muugano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) zinatambua mchango wa sekta isiyo rasmi, hivyo zimekuwa zikifanya juhudi mbalimbali kuendeleza na kuongeza tija katika sekta hiyo. 

Amesema katika kuhakikisha sekta hiyo inaendelea, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara kwa wajasiriamali wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuendelea kuwapatia vyeti vya uasili ambavyo vimetoa unafuu mkubwa wa kodi na tozo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Novemba 24, 2019)wakati akifunga Maonesho ya Wajasiriamali wa Tanzania kusherehekea miaka 20 ya uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Fumba, Zanzibar.

Amesema wanapohitimisha maonesho hayo sambamba na kusherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatakiwa wajitathmini kuona kama wametimiza malengo ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo. 

“Vilevile, tuendeleze ujirani mwema, kupanua na kuimarisha ushirikiano wa watu wa Afrika Mashariki ili kuharakisha ukuaji wa kiuchumi sanjari na kuboresha maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki kiuchumi, kisiasa na kijamii.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzungumzia kuhusu vikwazo visivyo vya kiforodha vinavyozorotesha wajasiriamali kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo amesema vimeendelea kutatuliwa kupitia majadiliano baina ya Tanzania na nyingine ndani ya Jumuiya hiyo kwa lengo la kuvipunguza na kuviondoa kabisa.

Waziri Mkuu amesema  kupitia majadiliano hayo, Serikali imefanikiwa kuratibu zoezi la uondoaji wa vikwazo vya biashara visivyo vya kiforodha 15kati ya 24vilivyoripotiwamwaka 2019 navikwazo tisa vilivyobakiahatua ya kuvipatia ufumbuzi inaendelea.

Hata hivyo,Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza mkakati wa kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha wajasiriamali wanachangamkia fursa za kibiashara zitokanazo na Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Waziri Mkuu amesema mkakati huo unahusisha zoezi la kufanya utafiti wa uelewa wa Watanzania kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki na matokeo ya utafiti huo yatatumika katika kutoa elimu kwa umma kulingana na mahitaji.

Katika kutatua changamoto ya mitaji kwa wajasiriamali, Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 ya kuweka mfumo wa kuvitambua, kuvisajili na kuviwezesha vikundi vyenye mwelekeo wa ushirika na ujasiriamali. 

Amesema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa taasisi za fedha na mifuko mbalimbali ya umma na binafsi kutoa mikopo kwa wajasiliamali kwa riba nafuu na ikiwezekana isiyo na riba.

“Katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Juni, 2019 mikopo yenye thamani ya sh.   bilioni 42.06 kwa vikundi11,487 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ilitolewa. Vilevile, mikopo hiyo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri imeendelea kuzingatia uwiano wa asilimia nne kwa vikundi vya wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.” 

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inahamasisha uundwaji wa vikundi vya wajasiriamali, kusimamia utoaji wa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi hivyo sambamba na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuwezesha wajasiriamali na wawekezaji wengine kufanya shughuli zao bila bughudha.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeanzisha mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa lengo la kutoa mitaji na huduma nyingine za kifedha zenye masharti nafuu kwa wananchi wa Unguja na Pemba. Mfuko huu umelenga wananchi wenye kipato kidogo ili waweze kuzalisha mali kwa kujiajiri na kupunguza umaskini.
Amesema hadi kufikia Juni 2019 kupitia mfuko huo mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 3.5 ilikuwa imetolewa na kuzifikia jumla ya Shehia 346. “Mfuko huu kupitia mradi wa mbogamboga na matunda umetoa mikopo 263 kwa wakulima wa mbogamboga na matunda 384 wa Pemba yenye thamani ya sh. milioni 60.6 na wakulima 384 wa Unguja yenye thamani ya sh. milioni 151.3.
Amesema Serikali imeendelea kufanya maonesho mbalimbali ya Wajasiriamali wa Sekta isiyo rasmi ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Maonesho hayo yametoa fursa kwa wajasiriamali kupata ujuzi, taarifa za masoko, teknolojia, mbinu na taratibu mbalimbali za kufanya biashara ili kukuza shughuli zao. 
Maonesho hayo yamewapatia wajasiriamali uthubutu wa kushiriki wao binafsi katika maonesho mengine kwenye nchi za Afrika Kusini, Malawi, Zambia, Sudan Kusini, Msumbiji na Marekani. Pia wameweza kufanya ziara katika nchi ya China ambako walijifunza na kununua mashine za kisasa kwa ajili ya kuboresha uzalishaji wa bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko la ndani na nje.EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.