NA. MWANDISHI WETU
Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel imezindua mfumo wa mtandao wa 4G wenye uwezo wa kutoa huduma za mitandao kwa kasi zaidi tofauti na ilivyokuwa awali na kurahisisha huduma kwa wateja wake nchini.
Akizindua mtandao huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki hii leo Novemba 14, 2019 katika hafla iliyoandaliwa na kampuni hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Dodoma Hotel amesema, mbali na utoaji wa huduma , mtanao huo utasaidia kuchochea shughuli za kimaendeleo kwa kuzingatia mchango wa sekta ya mawaasiliano katika uzalishaji.
Aliongezea kuwa, hatua hiyo imeonesha namna kampuni hiyo ilivyoweza kutambua mabadiliko ya kisayansi na teknolojia ikiwa ni pamoja na kuwafikia watanzania kwa wingi na urahisi zaidi katika huduma ya mawasilino.
“Hii imedhihirisha kuwa, mmeweza kuyaelewa mahitaji ya Watanzania wa kizazi hiki, na ndo maana leo mmezindua rasmi mtandao huu wenye kasi zaidi kuendelea kuboresha wamasilino hapa nchini,”alisisema Waziri Kairuki
Aidha aliwapongeza kwa hatua hiyo na kuwahakikishia kuwa, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa kutambua umuhimu wa sekta ya uwekezaji nchini.
Sambamba na hilo aliikumbusha Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzidi kusimamia maadili na matumizi sahihi ya mitandao kwa kuzingatia ongezeko la mitandao yenye kasi zaidi inachochea watu kufanya vitendo visivyofaa kwa matumizi yasiyofaa.
“Tusimamieni na kuhakikisha utaratibu na maadili yetu kama Watanzania yanazidi kuimarishwa na kudumishwa siku zote na huo ndiyo uzalendo kwani waswahili wanasema jasiri haachi asili na niwasihii tushikamane katika kulifanikisha hili”alisisitiza Kairuki
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu ya Airtel Tanzania Bw. George Mathen alieleza kuwa wameendelea kufanya maboresha hayo ili kuhakikisha wanatoa huduma stahiki zenye kuzingatia ubora ili kuendelea kuwa mtandao wenye uhakika na unaotoa huduma kwa ufanisi nchini.
Naye Mbunge wa Temeke Mhe. Abdallah Mtolea alisema kuwa,hatua ya kampuni hiyo kuzindua mtandao wenye kasi zaidi katika utoaji wa huduma kwa Watanzania utasaidia kuondoa changamoto za ukosefu wa mtandao wa uhakika katika maeneo mengi na kupongeza jitihada hizo zinazofanya na Airtel Tanzania.
“Nimefurahishwa kwa hatua hii, maana awali mlikuwa mnafanya vizuri ila uwepo wa mtandao wa 4G utaongeza kasi zaidi katika kutoa huduma zenu na kuendelea kuwafikiwa Watanzania wengi na huduma nzuri zaidi ili kuendelea kuwa na mchango katika shughuli za kiuchumi na kijamii,”alisema Mhe. Mtolea
=MWISHO=
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.