*Ataka fedha wanazopata
zitumike kujenga miradi mikubwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka
Asasi za Kiraia ziendelee kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi.
“Nitoe rai
kwenu wana AZAKI, muendelee kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla ili Serikali iweze kujenga
miradi mikubwa ya kijamii,” amesema.
Ametoa wito huo leo jioni (Jumatatu, Novemba 4,
2019) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na washiriki wa Maonesho
ya Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini yaliyoanza leo kwenye uwanja wa
Jamhuri jijini Dodoma. Maonesho hayo yatafikia kilele chake Ijumaa, Novemba 8,
mwaka huu.
Amesema Serikali
inatambua na kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya Kiserikali katika
kusukuma gurudumu la maendeleo nchini kama vile kuwajengea uwezo viongozi wa Serikali
za Mitaa wakiwemo Madiwani, viongozi wa vijiji na mitaa ili watambue majukumu
yao.
“Niwatoe hofu
tu kwamba Serikali inatambua mchango wenu wa kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli
mbalimbali za maendeleo; kujiongezea kipato na kupata ujuzi; utoaji wa huduma za
kijamii hususan elimu, afya, upatikanaji wa maji, huduma za kisheria na huduma
za mikopo midogo.
“Pia tunatambua
mchango wa AZAKI wa kuleta teknolojia mpya na rahisi kwa wananchi pale mnapoona
kuna uhitaji. Pia mnaisaidia Serikali kupinga mila potofu na kandamizi hasa kwa
makundi yenye mahitaji maalum,” amesema.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzitaka AZAKI nchini zizingatie sheria
iliyofanyiwa marekebisho ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24/2002 na kanuni
zake, ambayo ilipitishwa na Bunge kupitia Sheria Na. 3/2019 na kusisitiza
kwamba marekebisho hayo yalilenga kuboresha sekta hiyo.
“Nipende kuwahakikishia wana-AZAKI kuwa marekebisho
hayo yalilenga kuboresha sekta ya NGOs na siyo kuyabana mashirika yasiyo ya
Kiserikali kama ambavyo imekuwa ikipotoshwa na baadhi ya watu. Marekebisho hayo
yalizingatia misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,”
amesema.
Kuhusu mapato ya AZAKI, Waziri Mkuu amesema fedha wanazopata
zinaweza kufanya miradi mikubwa ambayo itawanufaisha wananchi na akawasihi
wazitumie kwenye ujenzi wa miradi mikubwa inayoonekana badala ya kuendesha
semina na warsha.
“Tunajua fedha mnazopata zinaweza kusaidia kwenye
miradi hii. Kwa mfano, kuanzia Januari hadi Septemba, mwaka huu, tulifanya
mapitio ya ufadhili wa fedha mnazopata. Na katika upekuzi uliofanyika kwenye
taasisi 92, ilibainika kwamba zilipokea jumla ya sh. bilioni 261.059 ambazo
zimeingia kwenye AZAKI hizi.”
“Vilevile, mwaka 2016 hadi 2017, tuliangalia mapato
ya NGOs 51, tukagundua kuwa katika kipindi cha miaka miwili, zimepokea jumla ya
shilingi trilioni 2.5. Kama fedha hizi zote zingeratibiwa vizuri kwa kupunguza
matumizi yasiyo na umuhimu ni lazima tungefika mbali. Tutumie vizuri fedha hizi
za ufadhili kwa miradi inayoonekana,” amesisitiza.
Akizungumzia
kuhusu ajira kwa vijana, Waziri Mkuu amesema vijana ni kundi lenye umuhimu mkubwa katika kutekeleza shughuli mbalimbali
za maendeleo licha ya kuwa wanakabiliwa na uhaba wa ajira.
Amesema Sensa
ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonesha asilimia 35 ya Watanzania wote ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35. Kwa
mujibu wa matokeo ya utafiti wa nguvukazi ya Taifa wa mwaka 2014, vijana
wamebainika kuwa ndio kundi kubwa la nguvukazi ya Taifa ambao ni asilimia 56 ya
nguvukazi yote nchini.
“Kila
mwaka, kumekuwa na ongezeko la vijana wanaoingia kwenye soko la ajira. Kwa
mfano, taarifa ya hali ya ajira ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa mwaka 2019
inaonesha kuwa asilimia 11.8 ya nguvukazi ya vijana duniani ambao ni takriban
vijana million 59.1 hawana kazi,” amesema.
Mapema, Waziri wa
Nchi (OR-TAMISEMI), Bw. Suleiman Jafo alizishukuru asasi zote za kiraia ambazo
zinafanya kazi Tanzania kwa sababu zinawahudumia wananchi kwa karibu zaidi. “Ninazishukuru
NGOs zote kwa kusaidia kutoa elimu kwa wananchi. GTunazishukuru kwa kazi kubwa
mnayoifanya Tanzania nzima kwa kushirikiana na Ofsi ya Rais TAMISEMI,”
Akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na washiriki wa maonesho hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alisema mwaka huu, wizara yake
imesajili mashirika yasiyo ya Kiserikali 617 ikilinganishwa na mashirika 385 yaliyosajiliwa
mwaka 2017.
“Kati ya hayo mashirika 617, mashirika 44 ni ya ngazi
ya kimataifa; 551 ni ngazi ya kitaifa, saba ni katika ngazi ya mikoa na
mashirika 15 ni katika ngazi ya wilaya. Hadi kufikia Oktoba, 30, 2019,
tumeshasajili mashirika 19,318” alisema.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.