Tuesday, November 5, 2019

WAZIRI MKUU ASHIRIKI MAZISHI YA MWENYEKITI WA CCM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameshiriki katika mazishi ya mwanasiasa mkongwe na Mwenyekiti wa zamani wa CCM wa wilaya ya Ruangwa, Bw. Kaspar Selemani Mmuya yaliyofanyika kwenye Kitongoji cha Mtakuja, kijiji cha Nangumbu wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Akizungumza katika  mazishi hayo, Waziri Mkuu amesema marehemu  Bw. Mmuya enzi za uhai wake alitoa ushirikiano mzuri kwa viongozi na wananchi wa Ruangwa kwa ujumla na wakati wote alikuwa tayari  kutoa ushauri katika masuala ya siasa na uongozi.

Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, ameshiriki katika mazishi ya mwanasiasa huyo mkongwe yaliyofanyika leo (Jumanne, Novemba 5, 2019). Amesema marehemu alikuwa kiongozi makini na mwenye kupenda ushirikiano.

“Marehemu alikuwa kiongiozi wangu na mshauri wa masuala ya siasa na kijamii wakati wote nilipomuomba au yeye mwenyewe alipoona iko haja ya kufanya hivyo. Wakati wote wa uhai wake alikuwa tayari kusikiliza na kushauri, “ alisisitiza Waziri Mkuu .

Mazishi hayo pia yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nchi OWM - Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana,  Anthony Mavunde, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Lindi, Fadhili Juma, Viongozi wa chama cha Walimu Tanzania wa Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Ruangwa  pamoja na viongozi wa Serikali na vyama vya Siasa.

Mapema leo asubuhi Mheshimiwa Majaliwa alishiriki katika kikao cha Bunge  kwenye ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.