Wednesday, November 6, 2019

WAZIRI MKUU AFIWA NA KAKA YAKE, AWASHUKURU WALIOJITOKEZA MAZISHINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewashukuru watu wote waliojitokeza katika mazishi ya kaka yake Mzee Bakari Majaliwa (78), aliyefariki juzi (Jumatatu, Novemba 04, 2019) nyumbani kwake katika kijiji cha Chimbila ‘B’wilayani Ruangwa, Lindi.

Ametoa shukrani hizo leo (Jumatano, Novemba 06, 2019) wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika kijijini Nandagala wilayani Ruangwa na amesema kwamba hayo ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kila mtu atapita kwenye njia hiyo.

“Tulikuwa 12 na sasa tumebaki watano, wanaume wawili na wanawake watatu. Msiba huu kwetu ni mkubwa umepunguza idadi ya watoto wa Mzee Majaliwa lakini hatuna namna ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu, wajibu wetu ni kuendelea kumuombea. Nawashukuru wote mlioacha shughuli zenu na kutukimbilia, familia imethamini sana ujio wenu jambao hili limetokea ghafla.” 

Waziri Mkuu pia amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa salamu za pole alizozitoa. “Jambo hili pia limemgusa Mheshimiwa Rais wetu ambaye ametutaka tuwe watulivu katika kipindi hiki kigumu na kwamba kila mmoja kwa dhehebu lake aendelee kumuombea marehemu ili Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema.”

Amesema alipata taarifa za msiba huo wakati akijiandaa kwenda wilayani Ruangwa kwa ajili ya kushiriki mazishi yamwanasiasa mkongwe na Mwenyekiti wa zamani wa CCM wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Kaspar Selemani Mmuya. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Generali, Venance Mabeyo akitoa salamu za pole kwa niaba ya Maafisa na Askari wa Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama amesema anajua uzito wa msiba pamoja na majonzi waliyonayo kwa kuondokewa na mpendwa wao na kwamba wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa ndiye anayetoa na anayetwaa. “Hakuna namna ya kurekebisha maamuzi ya Mwenyezi Mungu, tuendelee kumsindikiza kaka yetu kwa sala Mwenyezi Mungu ampokee kwa amani.”

Naye, Mwakilishi wa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Othman Kaporo amesema amewataka wananchi wajiandae na kifo kwa kufanya ibada. “Ni kawaida kwa binadamu kujisahau lakini Mwenyezi Mungu ametuwekea vitu vya kutukumbusha juu ya uwepo wake ikiwemo kifo, hivyo tuyatekeleze yale yalikuwa ya wajibu kuyatekeleza.”




EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.