Saturday, January 19, 2019

MHE. MAVUNDE AWATAKA KAZI SACCOS KUWA NA MIRADI YENYE TIJA

 NA; Mwandishi Wetu - Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana) Mhe. Anthony Mavunde ameutaka uongozi wa Kazi SACCOS kubuni miradi yenye tija ili kuboresha mfuko wao na kuleta manufaa kwa wanachama wake.
Ametoa rai hiyo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Wanachama wa SACCOS hiyo uliofanyika Januari 19, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za TAKWIMU Jijini Dodoma.
Ameutaka uongozi wa chama hicho kubuni miradi ya kimkakati inayotekelezeka na kuendana na mazingira, na hali ya kiuchumi ya eneo husika.
“Ni vyema uongozi kuangalia fursa za kiuchumi zilizopo Dodoma ili kuanzisha miradi itakayoendana na hali halisi ya kiuchumi pamoja na kukikwamua chama chenu kuendelea kuwa na tija,” alisisitiza Mavunde.
Lengo la mkutano hilo lilikuwa ni kupeana taarifa za uendeshaji wa chama, kufanya uchaguzi wa viongozi wapya katika bodi ya uongozi na kamati ya usimamizi pamoja na kujadili namna bora ya kuendelea kuboresha Chama hicho ili kuendelea kuwa na tija kwa wanachama wake.
Aidha aliwatoa hofu wanachama kwa kueleza kuwa, uwepo wa vyama hivi ni kisheria na kikanuni za utumishi wa umma na kuwataka kuviheshimu ili kuendelea kuwa wanachama hai.
“Ieleweke kuwa ukiwa katika chama hiki, bado upo katika utaratibu na kanuni za utumishi wako hivyo muendelee kufanya vyema katika chama ili kujipatia heshima ndani na nje ya ofisi yako,” alisema Mavunde.
Aliwapongeza viongozi pamoja na wanachama wote kwa mchango wanaoutoa kwa ofisi yake kuzingatia mchango wa Chama kwa watumishi wote.
“Ninashawishika na kuona mchango wenu kwetu kama ofisi, kwani mmechangia kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wetu, ambao vinginevyo wangeshindwa kutoa huduma bora yenye tija kwa wadau wetu kutokana na changamoto za kifedha huwenda ingechangia kuwaingiza katika matendo ya utovu wa nidhamu kama vile rushwa”,alisisitiza Mavunde.
Pia aliwataka viongozi wa Ofisi yake kuendelea kuunga mkono jitihada hizo ambazo chama kimezionesha hususani uanzishwaji wa miradi ikiwemo ikiwemo kuwekeza katika viwanda.
Naye Bw. Omari Sama mwenyekiti wa chama hicho aliunga mkono maagizo hayo kwa kuanzisha miradi endelevu itakayoleta maendeleo ya kiuchumi kwenye chama, kuongeza wanachama na kukifanya chama hiko kitambulike zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa ofisi hiyo, Bw. Peter Kalonga aliuasa uongozi mpya kuendelea kutoa elimu ya ushirika kwa wanachama ili kuweza kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Anthony Mavunde (wa nne kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe waliohudhuria Mkutano Mkuu Wanachama wa Kazi SACCOS Januari 19, 2019.Jijini Dodoma.EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.