Tuesday, January 8, 2019

OFISI YA WAZIRI MKUU YATOA MAFUNZO KWA MAMA WADOGO MKOANI TABORA

OWM (KVAU) - Tabora
 
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inaratibu mafunzo maalum kwa mama wadogo yanayolenga kuwawezesha kujitambua na kujithamini.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Uyui iliyopo Mkoani Tabora ambapo mama wadogo takribani 45 wamefundishwa mada mbalimbali ikiwemo Ujasiriamali, kilimo biashara, taratibu za kuunda vikundi vya uzalishaji mali, fursa za uwezeshaji wa vijana kiuchumi, malezi bora na familia, afya na lishe.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Uyui Mhe. Gift Msuya amesema kuwa Serikali inatambua tatizo la mimba za utotoni na imeonesha dhairi ufuatiliaji wa suala hilo kwa kuwachukulia hatua za kisheria wanaohusika na vitendo hivyo.
“Takribani asilimia 45 ya mabinti wanaoandikishwa kujiunga na kidato cha kwanza wanashindwa kumaliza kidato cha nne kutokana na changamoto za mimba za utotoni, ndoa za utotoni na umbali wa kupata huduma ya elimu.” alisema Msuya
Aidha, Msuya alieleza kuwa Halmashauri yake imeanzisha kampeni ya “Nishike Mkono, Boresha Elimu Uyui” inayolenga kuwainua watoto wa kike kwa kuwaboreshea mazingira ya elimu yatakayo wawezesha kupata elimu bora.     
Aliongeza kuwa Mkoa wa Tabora umekuwa ukitekeleza kwa vitendo Mpango wa Kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/18 – 2021/22 ambapo miongoni mwa mikakati ya mpango huo ni kupunguza kiwango cha mimba kwa vijana wa kike.
Pia alitoa rai kwa vijana walioshiriki mafunzo hayo, wakawe mabalozi wazuri kwa kufikisha elimu kwa vijana wenzao ili wafahamu njia za kuepuka mimba zisizo tarajiwa na waweze kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Bw. Julius Tweneshe alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu inaratibu programu ya mama wadogo kitaifa inayokusudia kuwawezesha kupata mbinu na stadi za kujitambua, kuthubutu, kufanya maamuzi sahihi na kujiwekea malengo katika maisha yao.
“Tutatumia mafunzo haya kuhakikisha vijana wanachangamkia fursa za kiuchumi kupitia vikundi vya uzalishaji mali ambavyo vitawasaidia kujipatia kipato na kuweza kutunza watoto wao.” alisema Tweneshe  
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Tabora Bw. Baraka Mackona aliweza kuishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu kwa kuandaa mpango wa mafunzo hayo ya mama wadogo kwa kuanza na Halmashauri ya Uyui na Kaliua.
“Tumeanza na halmashauri hizi mbili kutokana na ukubwa wa tatizo, hivyo kuwajengea uwezo vijana wa kike kutachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hili la mimba za utotoni.” alisema Mackona


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.