WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameahidi kupokea kundi la watalii wasiopungua 300 ambao
wanatarajiwa kuwasili nchini Machi, mwaka huu.
Watalii
hao ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 wanaotarajiwa kuwasili
nchini katika mwaka 2019 chini ya mpango unaosimamiwa baina ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania na kampuni ya TouchRoad
International Holding Group ya China.
Ametoa
ahadi hiyo leo (Jumamosi, Januari 19, 2019) alipokutana na Mwenyekiti wa Touchroad Group, Bw. Liehui He na
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji Thomas Mihayo ofisini kwake Mlimwa, jijini
Dodoma.
Waziri Mkuu
amefikia uamuzi huo baada ya kuelezwa na Bw. He huyo kwamba kundi hilo la watalii
likiwa Djibouti litapokelewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo na likienda Zimbabwe,
litapokelewa na Rais wa nchi hiyo.
“Tanzania
imeamua kuweka mkakati wa kuongeza idadi ya watalii nchini kwa kuboresha miundombinu
ya usafiri na kukuza utalii kupitia vivutio vya vyakula vya asili, mavazi ya
asili, wanyama, fukwe za bahari na milima. Kwa hiyo, ujio wa kundi hili kubwa,
unatoa fursa mpya ya kutangaza vivutio vya nchi yetu,” amesema.
“Nitoe wito
kwa Watanzania wanaoishi maeneo ya jirani na vivutio vyetu, wachangamkie fursa
ya ujio wa watalii hawa katika maeneo mbalimbali. Wakifika Dar es Salaam, wanaweza
kwenda Kigoma kuona Ziwa Tanganyika, mbuga zilizoko Nyanda za Juu Kusini, Arusha
au vivutio vya Zanzibar. Tujiandae, tuwe tayari kuwauzia bidhaa mbalimbali,”
amesema.
Pia
amesema amefurahishwa na wazo lao la kuifanya Dar es Salaam iwe kitovu cha utalii (tourist
hub) kwa makundi ya watalii ambayo yatakuja Tanzania na baadaye kutoka Tanzania
kwenda Lusaka, Harare, Johannesburg na Djibouti.
Mwenyekiti
huyo ambaye aliwasili nchini juzi, ameambatana na ujumbe wa watu 31 ambao
unajumuisha waandishi wa habari, wasanii, wanamuziki na watu mashuhuri.
Akiwa Beijing,
China, wakati akishiriki mkutano wa Jukwaa la Biashara baina ya Tanzania na
China lililofanyika Septemba mwaka jana, Waziri Mkuu alikutana na uongozi wa
kampuni ya TouchRoad ambayo ilionesha nia ya kutangaza fursa za utalii zilizopo
hapa nchini.
Ziara ya Bw.
He ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa kati ya kampuni ya TouchRoad
na Bodi ya Utalii ya Tanzania, Novemba 2018.
Mapema, Bw. He alimweleza Waziri Mkuu nia ya kampuni hiyo kutekeleza
makubaliano yao ya kutangaza
vivutio vya utalii vya Tanzania katika soko la China ili kuvutia watalii
wapatao 10,000 waitembelee Tanzania katika mwaka 2019.
“Tumepanga kuleta
watalii 10,000 kwa mwaka huu wa 2019 na tumeweka lengo la kuongeza idadi hiyo
kwa asilimia 20 kila mwaka kwa muda wa miaka mitano. Pia tuna lengo la kuitumia
ndege ya ATCL ili ilete watalii moja kwa moja kutoka Shanghai, China,” alisema.
Akielezea
ujio wa kundi la kwanza la watalii, Bw. He alisema kundi hilo litakaa Djibouti
kwa siku moja, Tanzania siku nne (tatu za kulala) na Zimbabwe siku tatu (mbili
za kulala) na kisha kurejea China.
Alisema
wanapanga kila mwezi wawe na kundi kubwa la watalii ambao watakuwa wanafikia
Tanzania na kupelekwa nchi nyingine kwa sababu Wachina wengi hupenda kufanya
utalii kwa siku walau 10, lakini wapelekwe maeneo matatu au manne tofauti kuona
vivutio vya aina nyingine badala ya kukaa sehemu moja kwa kipindi chote hicho.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.