Wednesday, January 16, 2019

WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO 14 KUHARAKISHA UJENZI WA MJI WA SERIKALI

*Awataka Makatibu Wakuu wasimamie upandaji miti, maua

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa mji wa Serikali na kutoa maagizo 14 ambayo yataharakisha kukamilika kwa kazi hiyo.

Ametoa maagizo hayo jana (Alhamisi, Januari 16, 2019) mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Ihumwa lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, Waziri Mkuu alisema pamoja na spidi anayoihimiza, bado wakandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora unaotakiwa (quality).

“Kazi ya ujenzi ikamilike tarehe 31 Januari 2019 kwa kasi na viwango vyenye ubora; mifumo ya ICT, umeme na maji izingatiwe wakati wa ujenzi na zile sites zenye upungufu wa nguvu kazi, vijana waongezwe na kazi ifanyike mchana na usiku,” alisema.

Aliwataka waratibu wa zoezi la Serikali kuhamia Dodoma wakiwemo Wizara husika na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe kuwa wakandarasi ambao hawajalipwa hususan vikosi vya ujenzi wanaojenga jengo la Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wanalipwa.

Waziri Mkuu aliwataka Makatibu Wakuu wote wasimamie upandaji miti, maua (hata landscaping) kwenye maeneo waliyopewa hasa katika kipindi hiki cha mvua ili mandhari za ofisi zianze kuvutia.

“Wizara zifanye usafi ndani na nje wakati ujenzi ukiendelea. Wizara kwa kushirikiana na TFS (Wakala wa Misitu) waendelee na zoezi la upandaji miti na wataalam wa bustani wahusishwe mapema wakati huu wa ujenzi. Lakini ninawaagiza Makatibu Wakuu wasimamie kwa karibu suala hili kwa sababu eneo kubwa liko chini ya ofisi zao, hawa wakandarasi wakimaliza ujenzi watabomoa mabati na kusafisha eneo la ujenzi tu,” alisema

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wahakikishe wanafungua ofisi ya muda katika Mji wa Serikali ili kurahisisha usimamizi wa miundombinu inayowahusu.

Ametumia fursa hiyo kuwataka Wakala wa Majengo nchini (TBA) wawasilishe taarifa ya maendeleo ya ujenzi kwa kila Wizara kwa kila hatua inayoendelea.

Alisema ununuzi wa vifaa vya ujenzi kwenye wizara mbalimbali hususan wakati wa ukamilishaji ujenzi, havina budi kununuliwa mapema na vile vinavyounganishwa kama vile chuma za kenchi vifanyike kwenye eneo la ujenzi (sites) ili vikaguliwe na TBA.

Kuhusu majengo ya ofisi ambayo kasi yake inasuasua kama vile TAMISEMI, Madini na baadhi ya sites za Mzinga Holdings, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wachukue hatua stahiki kusimamia ujenzi na kushauri ipasavyo.

Amesema wakandarasi kama Mzinga, SUMA JKT na NHC waangalie namna ya kuwapa ajira za kudumu hususan zinazohusiana na ujenzi mafundi wanaoshiriki shughuli za ujenzi Ihumwa.

Pia aliwataka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Wizara husika wahakikishe barabara za mji wa Serikali zinatengenezwa angalau kwa kiwango cha changarawe ili zipitike kwa urahisi katika kipindi cha mpito wakati taratibu za kudumu za kuweka lami zikiendelea.

Ili kuokoa muda, Waziri Mkuu aliwataka wakandarasi wahakikishe kazi zisizo za masharti kama vile kusuka nondo zitekelezwe kwa pamoja wakati wa shughuli za ujenzi wa ujumla zikiendelea.

Akihitimisha, Waziri Mkuu alisema Ofisi ya Waziri Mkuu ipatiwe taarifa ya idadi ya ajira iliyotengenezwa kutokana na ujenzi wa mji wa Serikali hususan za wale ambao hawana ajira za kudumu kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi huo.

Waziri Mkuu ameahidi kurudi Ihumwa Januari 31, mwaka huu ili akapokee funguo za ofisi za wizara zote.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi huo, Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma, Bw. Meshack Bandawe alisema ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni umegharimu sh. bilioni 3.6 na uko kwenye hatua za mwisho.

“Jiji la Dodoma lina ziada ya maji ya lita za ujazo milioni 13.5, na kwa upande wa umeme, kuna ziada ya megawati 20 kwa sababu uwezo wa kuzalisha umeme ni megawati 48 na zinazotumika hadi sasa ni megawati 28 tu,” alisema.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.