Friday, January 4, 2019

WAZIRI MKUU ACHUKIZWA NA TAARIFA YA KUZUIWA KWA NGUZO ZA UMEME


*Aitisha kikao na viongozi wa maeneo hayo pamoja na Mawaziri husika

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amemuita Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi pamoja na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote zinazozalisha nguzo za umeme katika mkoa huo kufika ofisini kwake ili waeleze sababu za kuzuia nguzo za hizo zisitoke. 

“Wanieleze kwa nini wanazuia nguzo,Wakati wananchi wanasubiri kuunganishiwa huduma ya nishati ya umeme wao wanazuia nguzo wanasubiri posho,  Wanaidai Serikali wakati ni  wao ni sehemu ya Serikali  Tutakutana ofisini kwangu Januari 7, saa tano kamili asubuhi.”

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Ijumaa, Januari 4, 2019) wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji Nyoni,  wilayani Mbinga akiwa katika siku ya tatu za ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma. Alisema jambo hilo linakwamisha zoezi la usambazaji umeme.

Aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walilalamikia kitendo cha kutofikishiwa huduma ya umeme katika maeneo yao kutokana na kukosekana kwa nguzo ambazo zimezuiwa kwa sababu ya wahusika wanaidai Serikali posho.

Waziri Mkuu alisema viongozi wengine watakaokuwepo kwenye kikao hicho ni pamoja na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Waziri wa nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, 
Wenyeviti wa halmashauri hizo zilizozuia nguzo ili wamueleze sababu za kuzuia nguzo hizo.

Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli iAlisema Serikali imedhamiria kusambaza huduma ya nishati ya umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo na wananchi hao wataunganishiwa umeme huo kwa gharama ya sh. 27,000 tu.

Pia Serikali imeondoa gharama za kulipia nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali na kwa vijiji ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola, jambo ambalo linalenga kufungua fursa za ajira na kukuza uchumi kwa wananchi na Taifa.

Serikali imefanya maamuzi hayo kwa sababu huduma hiyo ya umeme ni muhimu kwani mbali ya kutumika katika matumizi ya majumbani, pia kwa kusogezwa karibu na maeneo ya pembezoni itawezesha zahanati, shule ,viwanda na vituo vya afya kuwa na umeme.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.