Friday, January 4, 2019

BARABARA YA MBINGA-MBAMBA BAY KUKAMILIKA 2021*Waziri Mkuu akagua ujenzi, aridhishwa na kasi ya mkandarasi


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga kwenda Mbamba bey yenye urefu wa kilomita 69 itakayogharimu sh. bilioni 129.3.

Amekagua barabara hiyo leo (Ijumaa, Januari 4, 2019) wakati akielekea wilayani Mbinga akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Ruvuma.

Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo wa barabara inayojengwa na kampuni ya Chico ya nchini China, ambapo ameuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kusimamia vizuri mradi huo.

“Kazi hii inafanywa kwa uhogari mkubwa, naipongeza kampuni ya Chico kwa hatua waliyoifikia na ninaamini kwamba barabara hii inayotarajiwa kukamilika Januari 2021 itakamilika mapema zaidi.”

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi na mkoa kwa ujumla kwani itarahisisha usafiri kwa watu pamoja na usafirishaji wa mizigo.

Amesema pia barabara hiyo itakuza sekta ya utalii na uvuvi katika mkoa wa Ruvuma kwa sababu itawezesha watalii na wafanyabiashara kufika kwa urahisi katika wilaya ya Nyasa ambako ni kuingo cha biashara kati ya nchi jirani na mikoa inayopitiwa na ziwa Nyasa.

Mkuu huyo wa mkoa ametumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwapelekea fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ya hospitali, vituo vya afya, shule, nishati na maji.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.