Na. OWM,
KAGERA
Serikali
kupitia uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa
kushirikiana na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja
na wadau wa maendeleo; WHO, FAO, USAID, HRH2030, na USAID Global Health Supply Chain Programu, imefanikiwa
kufanya zoezi la kupima utayari wa kukabili ugonjwa wa Ebola katika mkoa wa
Kagera katika wilaya tatu za mkoa huo kwa kuhusisha watoa huduma za Afya katika wilaya hizo
za Bukoba mjini, Misenyi na Ngara.
Zoezi
hilo limefanikiwa kuwaimarisha watumishi hao katika maeneo maalum ikiwemo ya uratibu,
utambuzi na ufuatiliaji wa wagonjwa iwapo tagundulika, matibabu ya wagonjwa,
uchukuaji na usafirishaji wa sampuli na kuthibitisha maabukizi pamoja kuimarisha
mifumo ya utambuzi wa masuala ya Afya kwa kila abiria wanaopita kwenye mipaka
ya mkoa wa Kagera.
Akiongea
kuhusu kuhitimishwa kwa zoezi hilo jana tarehe 3 Agosti, 2019, mkoani Kagera, Mkurugenzi Msaidizi
(Utafiti na Mipango), Idara ya Menejimenti ya Maafa, ofisi
ya Waziri Mkuu, Bashiru Taratibu, ameeleza kuwa watumishi wa sekta ya Afya katika
maeneo yote ambayo zoezi hilo limefanyika wameweza kuimarishwa katika suala la uratibu hususani katika kuhakikisha kuwa
rasilimali zote zinazohitajika pindi ikigundulika kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola
zinapatikana kwa wakati na kwa kutosheleza mahitaji pamoja na kutumika kwa
usahihi.
Aidha,
Mratibu wa zoezi hilo toka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na
Watoto, ambaye pia ni Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dharura na Maafa, Dkt. Faraja Msemwa amefafanua kuwa timu
ya wataalamu wa sekta za Afya na Uratibu
wa Shughuli za serikali, kutoka Wizarani, Idara na Mashirika ya Kimataifa, wamefanikiwa kuendesha zoezi
hilo kwa watoa huduma wa Afya kwa wilaya tatu za mkoa huo hususan zilizopo mipakani.
“Zoezi
letu tumefanikiwa kulihitimisha mkoani
hapa kwa kufanya zoezi la kupima utayari wa kukabili ugonjwa wa Ebola kwa
watoa huduma wa Afya kwa vituo vya Afya vya
Nshambya, Kabyaile, Kabanga, Bunazi pamoja na Hospitali ya Rufaa ya mkoa
ya Bukoba. Tunaamini zoezi hili limeboresha utayari wa watoa
huduma za afya hapa mkoani Kagera katika kukabili ugonjwa wa Ebloa” alisema Dkt. Msemwa
Kwa
upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Marco Mbata amefafanua kuwa kufanyika
kwa zoezi hilo mkoani humo kumewawezesha kujua maeneo gani ya kuboresha wakati
wa kukabili mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na watumishi wameelewa
kwa vitendo wapo tayari kukabili ugonjwa huo.
“Tunashukuru
vifaa tunavyo vya kutumia wakati wa kujikinga iwapo atatokea mgonjwa wa Ebola,
hivyo kupitia zoezi hili tumeongeza uelewa wa kujikinga wenyewe, kuwakinga
watu walio karibu na mgonjwa pamoja na jamii nzima. Tumeweza kujifunza jinsi ya
kumpokea mgonjwa, kuchukua vipimo hakika zoezi hili limetujenga ” alisisitiza Mbata.
Naye
Mratibu wa Vituo vya Mipakani, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee
na Watoto, Remedius Kakuru amebainisha
kuwa kupitia zoezi hilo limeboresha utendaji wa maafisa Afya wa mipakani kwa
kuzingatia kuwa tayari serikali imenunua
vifaa vya kisasa muhimu vinavyo hitajika kwa ajili ya utambuzi wa abiria mwenye
maambukizi ya ugonjwa wa Ebola ikiwemo Vipima joto la mwili “thermal scanners". Vifaa hivyo vina uwezo wa kupima joto la mwili la abiria
wanao pita katika mipaka ya Tanzania vina uwezo wa kupima joto la mwili kwa
kuwa ndiyo kiashiria kikuu kimojawapo
kwa mgonjwa mwenye maabukizi ya Ebola .
Kwa
upande wake Afisa anayeshughulika na
Magonjwa ya Mlipuko kutoka Shirika la Afya Duniani, hapa nchini, Anthony Kazoka
alieleza kuwa Shirika la Afya Duniani linaendelea kushirikiana na serikalai ya
Tanzania katika kulinda Afya za watu wake kwa kutoa utaalamu katika zoezi hilo kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo
zimo hatarini kupata mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Hivyo kwa kufanyika zoezi hilo kwa mafanikio kutasaidia Tanzania kuwa
salama na kuwa chanzo cha kuiweka Dunia salama kwa kutambua maabukizi ya
ugonjwa huo mapema iwapo yatatokea.
Kufuatia
nchi ya jirani (DRC) kuendelea kukabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola tangu
Agosti mwaka 2018. Tanzania imeendelea kuchukua tahadhari za ugonjwa huo kwa
kupima utayari wa Watoa huduma za Afya kwa mikoa ya mipakani ukiwemo mkoa wa
Kagera. Mkoa huo ambao unapakana na nchi ya Uganda ambayo inapakana na DRC lakini pia imekuwa na wagonjwa kadhaa wa Ebola.
Zoezi
hilo linaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo ambao ni WHO,
FAO, USAID, HRH2030, na USAID Global Health Supply Chain Programu. Zoezi hilo
limefanyika kwa muda wa wiki moja ambapo limekamilika tarehe 3 Agosti mwaka
2019, kwa kufanyika katika vituo vya
kutolea huduma za afya na maeneo ya mipaka ya mkoani wa Kagera.
MWISHO.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.