Thursday, August 8, 2019

WAZIRI MKUU AKERWA NA UPANDAJI WA BILI YA MAJI MASWA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekerwa na kitendo cha Mamlaka ya Maji wilayani Maswa kupandisha bili ya maji kutoka sh 5,000 hadi sh. 28,000 jambo ambalo amesema halikubaliki na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka akutane na wahusika leo.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Agosti 8, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kumalija, wilayani Maswa mara baada ya kutembelea ghala la pamba la Chama cha Msingi cha Kumalija.

“Haiwezekani bili ikapanda kwa kiasi hicho. Hapo utakuwa unamsaidia mwananchi myonge au utakuwa unamnyonga. Bili haiwezi kupandishwa kwa asilimia kubwa kiasi hicho yaani imetoka shilingi elfu tano hadi shilingi elfu ishirini na nane.”

Waziri Mkuu alisema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo upandishaji huo wa bili hauna tija kwa wananchi wanyonge.

Wakati huo huo,Waziri Mkuu alisema Serikali imetoa sh. milioni 440 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la upasuaji, ukarabati wa wodi na duka la dawa, upanuzi wa wodi ya watoto na ujenzi wa wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa, ambapo ujenzi wake unaendelea.

Alisema mbali na fedha hizo, pia Serikali imepeleka sh. milioni 881 wilayani Maswa ambapo kati yake sh. milioni 481 ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa kituo vya afya cha Malampaka, kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya kituo cha afya cha Mwabayanda.

Akizungumza kuhusu elimu msingi bila malipo, Waziri Mkuu alisema kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 Serikali imepeleka wilayani Maswa jumla ya sh. bilioni 2.1, kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa Maofisa Elimu wa kata na Walimu Wakuu katika shule 28 za msingi.

Pia Waziri Mkuu alisema Serikali kuanzia mwaka 2016 hadi 2019  imepeleka wilayani Maswa jumla ya sh. bilioni 2.7 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule katika shule 16 za Sekondari.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.