Saturday, August 3, 2019

WAZIRI MKUU ATAKA BENKI ZIWAHUDUMIE WANUNUZI WA PAMBA KESHO JUMAPILI


*Nia yake ni wakulima waanze kulipwa Jumatatu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka benki zilizoko kwenye mikoa inayolima pamba zihakikishe kuwa kesho Jumapili zinatoa huduma kwa wateja ili wanunuzi wa pamba wakamilishe taratibu za mikopo.

“Kesho mabenki yanayotoa huduma Jumapili ni vema yafanye kazi, ili wanunuzi wa pamba waje wakamilishe taratibu zote za makaratasi na Jumatatu wapate hela ya kuanzia kazi. Hata mkifunga saa 6 mchana, wao wabakie hadi saa 10 ili mradi wakamilishe taratibu zote,” amesema.

Ametoa wito huo leo mchana (Jumamosi, Agosti 3, 2019) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa nane inayolima pamba ya Mara, Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga, Singida na Tabora pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB.

Waziri Mkuu amesema kikao kilichofanyika jana (Ijumaa, Agosti 2, 2019) baina ya Benki Kuu, wanunuzi wa pamba na wamiliki wa mabenki kimeafiki kuanza kutoa mikopo kwa wanunuzi ili waanze kununua pamba kuanzia keshokutwa (Jumatatu, Agosti 4, 2019).  

Amesema kazi ya kununua pamba ikianza, ilipwe kwanza iliyokusanywa ili ianze kusombwa na iweze kupisha nafasi kwa pamba mpya itakayoendelea kununuliwa na kupelekwa kwenye maghala.

Amemtaka pia Mwenyekiti wa Wanunuzi, Bw. Christopher Gachuma ahakikishe anaweka ufuatiliaji ili kujua kujua ni kiasi gani cha pamba kimenunuliwa kutoka kwa nani na wapi. “Endeleeni na uratibu wa ununuzi mjue nani amenunua nini, wapi na kwa gharama ipi.”

Pia amewataka wataalamu wa Wizara wa Kilimo waende mikoani, watu wa mabenki na Benki Kuu washirikiane na taasisi ambata kama Bodi ya Pamba, Tume ya Ushirika na AMCOS ziratibu vizuri kila mwananchi anayepeleka pamba na wahakikishe analipwa.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka wanunuzi wa pamba na wafanyabiashara wote wajenge viwanda hapa nchini ili kupata suluhisho la kudumu la soko la pamba. “Natoa wito kwa wafanyabiashara nchini wajenge viwanda vya kusokota nyuzi na kutengeneza nguo.
Amesema hivi sasa nchini, kuna viwanda viwili tu vya kusokota nyuzi ambapo kimoja kiko Dar es Salaam na kingine kiko Shinyanga ambavyo uwezo wake ni mdogo. “Leo tumenunua pamba lakini tutaanza kupata changamoto ya usafirishaji wa kuipelekea nje ya nchi kuiuza. Tukiwa na viwanda hapa ndani, tatizo la soko halitakuwepo.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Mabenki, Bw. Abdulmajjid Nsekela, aliwahakikishia wakuu wa mikoa yote na wanunuzi waliokuwa wakishiriki mkutano huo kutoka kwenye mikoa yao kwamba fedha itapatikana kuanzia Jumatatu (keshokutwa).

“Napenda kuwahakikishia kuwa kwenye kikao cha jana, benki zote zimeridhia kwamba zitatoa mikopo kwa wanunuzi. Tulikubaliana kwamba wanunzi wote walioomba mikopo waje haraka kuchukua fedha zao, waliopata lakini wakawa hawajachukua mikopo waje pia kuchukua.

“Mabenki yako tayari kutoa fedha hizo, na tutasimamia ili kuhakikisha fedha zinatolewa kwa wakati na wanunuzi wanapata hela,” alisema mbele ya Waziri Mkuu.

Naye Mwenyekiti wa Wanunuzi wa Pamba, Bw. Christopher Gachuma alisema wanunuzi wako tayari kununua pamba ili itoke mikononi mwa wakulima iende kwa ginners (wenye vinu vya kuchambua pamba.

“Kuanzia wiki ijayo, tutajitahidi kununua pamba kwa haraka na kwenye maeneo yasiyo na wanunuzi tutakutana na kujipanga ili tuwafiie wote. Ila kwenye mikoa ya pembezoni kama Katavi, ambako hakuna ginneries, tunaomba upendeleo maalum sababu ya umbali uliopo.”

Naye Waziri wa Kilimo, Bw. Japhet Hasunga amesisitiza kuwa wanunuzi wanaoenda kununua pamba wilaya za Meatu, Igunga na Singida wawe makini na wapeleke kwenye ginneries maalum za kuchambua mbegu na siyo za kusindika mafuta.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Bw. Selemani Jafo ameiomba Benki Kuu ya Tanzania (BoT) isimamie kwa karibu makubaliano ya kikao cha jana ili utekelezaji wake  uende kwa haraka zaidi.

“Ningeshauri Mwenyekiti wa Wanunuzi afuatilie wafanyabiashara wake, ili wakipata hiyo fedha, waende wakatimize malengo yaliyokusudiwa. Na Wakuu wa Mikoa mkutane na wanunuzi wa mikoa yenu kila baada ya siku mbili, ili muweze kubaini kwa haraka changamoto zinazowapata na kuzisuluhisha kwa haraka,” alisema.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.