Monday, October 28, 2019

KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MKAKATI WA AJIRA NA UWEZESHAJI VIKUNDI VYA VIJANA

Na; Mwandishi Wetu
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mikakati iliyoweka katika kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na uwezeshwaji kiuchumi kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana “Youth Development Fund” na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya vijana katika Mkoa wa Morogoro, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga ameipongeza Serikali kwa mikakati iliyokuja nayo katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwajengea mazingira wezeshi na yanayowahamasisha kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
“Matokeo ya utekelezaji wa mikakati hiyo tumeona kwa kiasi kikubwa imewawezesha vijana kutambua taratibu rasmi za kupata mikopo yenye riba nafuu na ambayo imewasaidia kuazisha miradi ya kiuchumi,” alisema Mheshimiwa Giga.
Aliongeza kuwa Serikali iendelee kutenga bajeti zaidi ya uwezeshwaji wa vikundi vya vijana kwa kuwa vina tija na vinapunguza tatizo la ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa.
Sambamba na hayo Kamati hiyo iliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutoa maelekezo katika halmashauri zote kuelimisha vijana zaidi ili waweze kutambua taratibu za kupata mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana na asilimia 10 ya mikopo ambayo utolewa kwa Vijana 4%, Wanawake 4% na Wenye Ulemavu 2% kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.
Akitoa maelezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde ameihakikishia Kamati ya Bunge kwamba Serikali itaendelea kuviwezesha kiuchumi vikundi vya vijana katika mkakati wa kuhamasisha vijana kujiajiri lakini pia kuwajengea uwezo wa kiuchumi vijana ili nao pia washiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa uchumi wa viwanda ambapo matarajio ni kwamba ifikapo mwaka 2025 zaidi ya asilimia 40 ya nguvukazi iwe imeajiriwa kwenye sekta ya viwanda.
“Serikali iliazisha mfuko wa maendeleo ya vijana na programu mbalimbali ili kuwawezesha wananchi hususan vijana kuweza kupata mahitaji ya mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazo waingizia kipato,” alisema Mavunde
Akitolea mfano mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vijana kutumia teknolojia ya kitalu nyumba ni mkakati mzuri ambao Serikali imekuja nao katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo.
Aidha, Naibu Waziri Mavunde aliwahamasisha vijana kuandaa maandiko ambayo yataelezea shughuli zenye tija wanazotaka kuzifanya katika kujileta maendeleo ili waweze kupata mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri itakayowasaidia kuendesha shughuli zao.  
Kwa nyakati tofauti vijana wa Mkoa wa Morogoro wameishukuru Serikali kwa uwezeshaji kupitia Mfuko wa maendeleo ya vijana na kuomba kuwezeshwa zaidi ili kukidhi matarajio yao ya uanzishwaji wa viwanda katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tano katika uchumi wa viwanda.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.