Thursday, October 17, 2019

WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA YA RUANGWA

*Akemea ujenzi mbovu wa kuta, aagiza zibomolewe na kurekebishwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi na kusema kwamba hajaridhishwa na baadhi ya majengo.

Amemwagiza Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Tengamaso Wilson abomoe kuta zenye hitilafu na kurekebisha kasoro zilizopo kwenye majengo hayo ikiwemo kutonyooka kwa kuta za majengo hayo.

Alitoa agizo hilo jana (Jumatano, Oktoba 16, 2019) wakati akikagua majengo ya hospitali hiyo, na kumweleza mhandisi huyo kwamba kuta zimepishana unene kwa sababu hakusimamia kazi yako ipasavyo. “Ukuta huu ni mbovu kwa sababu hukuwasimamia vizuri mafundi wako. Kuna mahali juu unaona ukuta ni mdogo na huku chini ni mnene.”

Majengo ambayo Waziri Mkuu aliyakagua na kuonesha kutoridhishwa nayo ni ya utawala, wagonjwa wa nje (OPD) na maabara. Majengo mengine yanayojengwa ni jengo la wazazi, la X-ray, la utoaji dawa na la kufulia nguo.

Alipouliza ni kwa nini kumetokea tofauti baina ya kuta hizo, Waziri Mkuu alijibiwa kwamba tatizo ni upigaji wa lipu. “Mhandisi wa Wilaya simamia hili, kagonge upya kuta za jengo hili na lile. Hatuwezi kuwa na jengo la Serikali la aina hii. Tukitoa fedha ya Serikali ni lazima mjiridhishe kama kilichojengwa ndicho sahihi.”

“Tunahitaji majengo yote yawe smart, hata ujenzi wake nao uwe smart. Usikubali kutoa certificate kama kazi haijakamilika. Kama kuna kazi haujaridhika nayo, usikubali certificate itoke. Zile sentimeta 30 ni lazima zirekebishwe la sivyo, itaonekana huku uliweka matofali mengi kuliko upande ule,” alisisitiza.

Akiwa hospitalini hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba katika awamu ya kwanza, Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe majengo saba ya kipaumbele ambayo ni jengo la wazazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, la X-ray, la utoaji dawa, la kufulia nguo na la utawala.

Ujenzi wa hospitali hiyo unafanyika kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa ‘Force Account’ ambapo Halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri mafundi wa kujenga majengo yaliyoelekezwa wakisimamiwa na wataalam wa halmashauri na kamati mbalimbali. 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemwagiza mweka hazina wa Halmashauri hiyo, Bw. Frank Chonya ajiridhishe na kazi za ujenzi zinazofanyika kabla hajaamua kutoa fedha za malipo.

“Mweka hazina, wakati wote ukiambiwa kuwa certificate imeletwa ni lazima uende ukakague mradi na kama haujaridhika, sema wazi kwamba hujaridhika na kazi iliyofanywa,” alisema Waziri Mkuu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Andrea Chezue alisema kiasi chote kilichotolewa na Serikali cha sh. bilioni 1.5 kimeshatumika, na kwamba Halmashauri illitumia zaidi ya sh. milioni 100 ili kusafisha eneo na kulipa fidia ili wapate eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 56.

“Mchango wa Halmashauri ya Wilaya kwenye ujenzi wa hospitali hii, mpaka sasa ni kwamba tumelipa sh. milioni 88.266 zikiwa ni fidia ya eneo la ujenzi na sh. milioni 14.418 zimetumika kusafishia eneo lote,” alisema.

(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.