Tuesday, October 22, 2019

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZITAKA HALMASHAURI KUWAWEZESHA VIJANA KIUCHUMI KUPITIA ZABUNI ZA HALMASHAUR


Na; Mwandishi Wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde amezitaka Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Majiji nchini kuwawezesha Vijana kiuchumi kwa kutumia Vikundi na Kampuni za Vijana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwa kuzipa zabuni kampuni na vikundi hivyo kupitia utaratibu wa “force account” hasa katika utengenezaji wa madawati na ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo, zahanati na vituo vya Afya.
Naibu Waziri Mavunde kayasema hayo Wilayani Musoma wakati alipotembelea Chuo cha Ufundi cha Mt. Anthony ambapo jumla ya Vijana 240 wanasoma hapo fani mbalimbali kwa ufadhili wa Serikali kupitia Programu ya Ukuzaji Ujuzi Nchini iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo mwaka huu wa fedha 2019/2020 inatrajiwa kuwajengea uwezo Vijana 46,000 katika fani mbalimbali.
"Serikali inayo nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba tunaijengea Ujuzi stahiki nguvukazi ya Taifa hili ili vijana wengi zaidi waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji mali.Mamlaka za Serikali za Mitaa ziwe kichocheo katika kuwawezesha Vijana kiuchumi kwa kutoa zabuni kwa vikundi na makampuni ya Vijana nchini kote hasa zile zinapitia katika mfumo wa manunuzi wa force account," alisema Mavunde
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Naano amewahakikishia Vijana hao kupata mikopo ya asilimia 4 na asilimia 2 kwa wenye ulemavu itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri na kuwataka kuunda vikundi kutokana na fani zao za Ufundi.
Akizungumza kwa niaba ya Vijana wenzake wanafuika ya Programu ya kukuza Ujuzi, Bw. Baraka Emmanuel ameishukuru Serikali kwa kuwajali Vijana na kuwawezesha kupata Ujuzi kupitia mafunzo wanayoyapata hapo Chuoni ambayo pia yatawafanya waweze kujiajiri na kuajiri Vijana wengine.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akizungumza jambo na vijana wanaojifunza fani ya Uchomeleaji na uungaji vyuma alipotembelea karakana kujionea mafunzo ya vijana hao.
Baadhi ya vijana wanaojifunza ufundi wa magari wakijishughulisha ikiwa ni sehemu ya mafunzo yao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akizungumza jambo na vijana wanaojifunza fani ya Ushonaji alipotembelea kujionea mafunzo ya vijana hao.
Sehemu ya vijana wa Chuo cha Ufundi cha Mt. Anthony wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (hayupo pichani) alipowatembelea vijana hao kwa lengo la kukagua maendeleo ya mafunzo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Naano akieleza jambo wakati wa ziara hiyo.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.