*Ashiriki mbio za mwenge kijijini kwao
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kushikamana na wazingatie ujumbe wa mbio za mwenge za mwaka huu unaohimiza umuhimu wa maji, uchaguzi wa Serikali za mitaa, vita dhidi ya rushwa, malaria, UKIMWI na dawa za kulevya.
Ametoa wito huo leo asubuhi (Jumatano, Oktoba 9, 2019) wakati akizungumza na viongozi wa Halmashauri za Lindi na Ruangwa na wananchi wa kijiji cha Nangumbu kwenye uwanja wa shule ya msingi Nangumbu ambako mwenge huo ulipokelewa saa 1:44 asubuhi ukitokea Nyangao wilayani Lindi.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, aliwasili wilayani Ruangwa jana jioni, ili kushiriki mbio za mwenge. Kesho (Alhamisi, Oktoba 10) mwenge huo utaelekea Nachingwea, ambapo Ijumaa (Oktoba 11) utaenda Liwale, Jumamosi (Oktoba 12) utaenda Kilwa na Jumapili (Oktoba 13) utakuwa Manispaa ya Lindi ambako utahitimisha mbio hizo na kuzimwa Oktoba 14, mwaka huu.
Waziri Mkuu amewataka wananchi wote wajiandikishe kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili Tanzania iweze kupata viongozi bora. “Tuitikie kaulimbiu ya mwaka huu kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hapa Ruangwa, hadi jana jioni watu 28,000 walikuwa tayari wamejiandikisha. Tukachague viongozi wachapakazi na waadilifu watakaoleta maendeleo kwa nchi yetu,” amesisitiza.
Mapema, akizungumza baada ya kupokea mwenge huo saa 2:21 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Hashim Mgandilwa alisema utakimbizwa kwenye kata saba na vijiji 17 ambapo miradi mitatu mikubwa yenye thamani ya sh. bilioni 2.9 itazinduliwa.
Katika kijiji cha Nangumbu, mwenge ulizindua mradi wa mabweni na klabu ya kupiga vita rushwa kwenye shule ye sekondari ya Hawa Mchopa. Ukiwa njiani, mwenge huo ulipitishwa kijiji cha Nandagala ambako Waziri Mkuu alizaliwa. Pia aliupokea na kuukimbiza kidogo akiwa na wanakijiji wenzake, kisha mwenge huo ukaendelea kukimbizwa kuelekea kata ya Likunja ambako watazindua mradi wa maji wa Kitandi. Pia mwenge huo utazindua mradi wa barabara ya lami kwenye kata ya Nachingwea, iliyoko Ruangwa mjini.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mbio za mwenge wilayani Ruangwa, kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa, Bw. Mzee Ali Mkongea alimshukuru Waziri Mkuu kwa kujumuika na wananchi kushiriki ratiba ya mapokezi ya mwenge wilayani humo.
Alisema Serikali ya awamu ya tano, ndani ya miaka mitatu (2015-2018) imekamilisha kwa wakati miradi 124 ya maji ambapo aliitaja baadhi yake kuwa ni miradi mikubwa ya Chalinze, Bagamoyo, Arusha, Tabora na Musoma. Pia alisema Serikali imeendelea na uchimbaji wa visima virefu na vifupi vya maji kwa gharama ya sh. bilioni 14.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzana kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimeingia mkataba na Serikali ya India wa dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji kwenye miji 28 ya Tanzania. Lakini kuna changamoto nyingi kwenye miradi hii ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za umma na wakandarasi kujenga baadhi ya miradi chini ya kiwango.”
“Pia kumekuwa na shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji. Wananchi tusaidiane kuvilinda vyanzo hivi kwa sababu kazi ya kuvitunza si ya Serikali peke yake bali inaanza na mimi na wewe,” alisema.
Aliwasihi wananchi hao wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kuchagua viongozi wazalendo ambao wana calibre ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.
Akitoa takwimu za ugonjwa wa malaria nchini, Bw. Mkongea alisema mkoa wa Kigoma unaongoza kwa maambukizi ya ugonjwa huo kwa asilimia 24, ukifuatiwa na Geita (asilimia 17), Mtwara (asilimia 15) na Lindi wenye asilimia 12.
“Niwasihi wananchi tumieni vyandarua vinavyotolewa bure na Serikali hasa akinamama wajawazito na watoto walio na umri chini ya miaka mitano. Kuna maeneo tumekuta baadhi ya watu wakivitumia kuvulia samaki na kufungia bustani ili kuku wasiingie. Haya si matumizi yake hata kidogo,” alisisitiza.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.