Monday, October 7, 2019

UAGIZAJI BIDHAA ZA NJE UTAENDELEA KUPUNGUA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nje na kuongeza ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa ndani ili kukuza viwanda vya ndani mfano ni bidhaa za mbao na mafuta ya kula.

“Napenda kuwahakikishia kuwa, bidhaa zetu ni nzuri na zinapendwa na watu wengi hata wa nje ya nchi. Mnachotakiwa kukifanya ni kuzalisha bidhaa kwa wingi na kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwenye maeneo yenu, hii itawezesha kuwa na uzalishaji wenye gharama ndogo na kuwa na bei shindani katika soko."

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 7, 2019) wakati akifungua Maonesho ya Sido Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya BomberdiaManispaa ya Singida. Amesema Serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya madini nchini.

Niwasihi Watanzania wote hasa wale wanaofikiria kuwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi ndizo zenye ubora kuliko za hapa nchini, kuachana na dhana hiyo potofu, kwani bidhaa zetu ni bora na zina viwango vinavyostahili.” 

Amesema wakizalisha bidhaa kwa kutumia malighafi za ndaniitawezesha ajira endelevu kuwepo kwa vijana, itasaidia malighafi kutoharibika lakini pia bidhaa zitakazozalishwa zitakuwa na thamani kubwa badala ya kuuza malighafi kwa bei ya chini. 

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Amesema uanzishwaji wa viwanda umejikita zaidi katika uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo na maliasili yanayopatikana nchini, kama, kilimo, mifugo, misitu, uvuvi na madini kwani wananchi wengi wanategemea mazao na rasilimali hizo kwa maisha yao. 

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhimiza uongezaji thamani wa mazao husika kwa kuwa ndiyo njia sahihi.  “Kwa misingi hiyo, usindikaji, uchakataji na uchenjuaji, vitachangia kupunguza upotevu unaotokea msimu wa mavuno, kuongeza ajira na thamani ya mazao kwa lengo la kuwapatia wazalishaji kipato.” 

Amesema uongezaji thamani utahitaji teknolojia (mashine na ujuzi), ambapo baadhi ya teknolojia hizo zimeoneshwa kwenye maonesho hayo. “Vilevile, maonesho hayo yametoa fursa ya kuonesha teknolojia zinazoweza kurahisisha uzalishaji na kuleta ufanisi zaidi ili kuongeza tija na kuhimili ushindani katika soko la ndani na nje.”

Mapema, akitoa taarifa kuhusu maonesho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SIDO, Prof. Elifas Bisanda alisema wamekuwa wakiandaa maonesho hayo ili kuwahamasisha wajasiriamali wadogo na wa kati wapate mbinu mpya juu ya viwanda vidogo.

"Pia tumekuwa tukifanya maonesho haya ili kuwapa wananchi uelewa kuhusu bidhaa zinazozalishwa nchini. Tangu mwaka 2006, yalikuwa yakifanyika kikanda, lakini kwa sasa yanafanyika kitaifa," alisema.

Alisema kupitia maonesho hayo, wajasiriamali  hupata mafunzo ya ufungashaji wa bidhaa lakini pia hupata fursa ya kubadilishana uzoefu miongoni mwao na kupata taarifa kutoka kwenye taasisi zinazojihusisha na viwanda vidogo na vya kati.

Alisema anaiomba Serikali iwapatie fedha zaidi ili waweze kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imepeleka umeme hadi vijijini lakini wananchi wengi hawanufaiki na uwepo wa umeme huo. 

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi alisema hii ni mara ya pili maonesho hayo yanafanyika mkoani humo.


(mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.