Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa amewaagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama na Mkurugenzi wa
Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, wafike ofisini kwake Dar es Salaam kesho
asubuhi na taarifa kuhusu skimu wa umwagiliaji wa Narunyu.
Ametoa agizo
hilo leo mchana (Alhamisi, Oktoba 17, 2019) wakati alipoenda kukagua skimu hiyo
ambayo imekuwa ikilalamikiwa tangu 2017. Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Mtama ni Bw. Warioba Gunze na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, ni
Mhandisi Mndeme.
Amechukua
uamuzi huo baada ya kufika eneo la mradi na kupokea malalamiko ya wanajumuiya
ya umwagiliaji kutoka kwa Mwenyekiti wao, Bw. Bakari Awadhi juu ya kusuasua kwa
mradi huo lakini alipotaka apate maelezo ya wataalamu hakuna hata mmoja ambaye
alikuwepo.
"Nilitaraji
niwakute hapa Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Umwagiliaji wa Wilaya na
Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda. Nimeagiza wanikute uwanja wa ndege Lindi au Dar
es Salaam na kesho asubuhi waje ofisini kwangu wanipe taarifa kamili ya mradi
huu. Nataka nijue fedha zilizobakia zaidi ya sh. milioni 240 ziko wapi."
"Walipaswa
niwakute hapa wananisubiri kwa sababu nilitoa taarifa tangu jana kwamba
nitapita hapa. Nimepata taarifa kwamba wamesafiri kutoka Mtwara na leo asubuhi
walikuwepo Lindi mjini. Waje ofisini kesho, wakishindwa, nitachukua maamuzi mengine,"
amesema.
Akielezea
umuhimu wa mradi huo wakati akizungumza na baadhi ya wanaushirika waliokuwepo,
Waziri Mkuu amesema ni wa muhimu kwa sababu unatiririsha maji wakati wote.
"Huu ni mradi wa kuringia. Mradi huu unatiririsha maji wakati huu wa kiangazi,
tena mengi tu."
Amesema
kutokana na umuhimu wa mradi huo, hivi sasa wangekuwa wanazalisha mazao ya kila
aina. "Hapa ni mahali pa kuzalisha mazao mengi, leo unalima mahindi,
ukivuna unapanda matikiti, ukitoa unapanda nyanya. Sasa nitapasimamia mwenyewe,"
amesisitiza.
Amewataka
wanaushirika wanaounda jumuiya ya umwagiliaji wahakikishe kila mmoja anatambua
eneo lake na mara kazi ikianza wawe tayari kuanza kilimo. "Huu mradi una
manufaa kwa watu wa Ruo, Mahumbika hadi Mnazi Mmoja. Lazima tuung'ang'anie kwa
sababu kuna idadi kubwa ya wakulima wanaoutegemea. Huu mradi lazima tuuvalie
njuga."
Waziri Mkuu
alipofika uwanja wa ndege wa Lindi, maafisa hao walikuwa hawajafika kwa sababu
simu zao hazikupatikana, na akaagiza waje Dar es Salaam kesho asubuhi.
Mapema, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bw. Shaibu
Ndemanga alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika mafaili aliyoyapitia ofisini
kwake alibaini kwamba mradi huo ulitengewa sh. milioni 788 ambapo mkandarasi wa
kwanza Chest Investments Company alilipwa sh. milioni 121 lakini akashindwa
kazi.
"Mkandarasi
wa pili ambaye ni D & L naye alilipwa zaidi ya shilingi milioni 400 naye
pia akashindwa kazi ya kuondoka tope. Kwenye ripoti, inaonesha zilibakia sh. milioni
249," alisema.
Naye Mwenyekiti wa wanajumuiya ya umwagiliaji ya Narunyu, Bw.
Bakari Awadhi alisema skimu hiyo yenye ukubwa hekta 1,200 imekuwa ikijaa
maji na kufunika mitaro na hatimaye kujaa mchanga.
Alimwomba
Waziri Mkuu awasaidie kuifufua skimu hiyo kwa sababu inawanufaisha wakazi wa
mikoa ya Lindi na Mtwara.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.