Wednesday, May 23, 2018

SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI KATIKA MAKAZI YA WATU WENYE UKOMA YA SAMARIA HOMBOLO


NA.MWANDISHI WETU
Serikali imejipanga kuwajengea Kisima cha kisasa watu wenye mahitaji maalum kitachoweza kuhudumia Kaya 26 zenye jumla ya watu 56 wenye ukoma na wazee katika Kambi ya Samaria Hombolo jijini Dodoma.
Hatua hiyo inakuja mara baada ya wakazi wa kambi ya Samaria kueleza changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo; ukosefu wa maji salama, changamoto za matibabu kwa kukosa bima za afya, uchakavu wa  magodo kwa ajili ya malazi, uhaba wa chakula cha uhakika.
Changamoto hizo zimeibuliwa wakati ya Ziara ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe.Stella Ikupa alipoambatana na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe.Jumaa Aweso Mei 23, 2018 katika Makazi ya watu wenye mahitaji maalum ikiwemo wazee na watu wenye ukoma.
“Watu wenye mahitaji maalum ikiwemo wenye ukoma wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji eneo la Samaria, sisi kama Serikali tumedhamiria kuwajengea kisima cha kisasa kitakachotoa maji baridi na kuweza kuhudumia makambi haya pamoja na kijiji chote cha Samaria”.alisema Naibu Waziri Ikupa
Naye Naibu Waziri Wizara ya Maji na Umwagiliaji Jumaa Aweso ameiagiza timu ya waataalamu kutoka Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa kuanza kazi hiyo mara moja.
“ Naagiza timu ya wataalamu kuja kupima maeneo ambayo yatafaa kwa ajili ya uchimbaji wa kisima hicho” .alisema Aweso
Kwa upande wake, Katibu Chama cha Wenye ulemavu Samaria, Richard Kongawadodo aliipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua ya kujenga kisima cha maji baridi kitakachosaidia kutatua changamoto zilizokuwepo awali na kusaidia katika shughuli za maendeleo ikiwemo za kilimo, umwagiliaji na matumizi mengineyo.

“Naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutujali watu wenye mahitaji maalum hasa sisi wenye ukoma kwani tumekuwa tukikabiliwa na changamoto ya kukosa maji ya uhakika na salama, hivyo ujenzi wa kisima hicho utaleta tija hususan katika shughuli za kilimo ili kujipatia fedha na kukidhi mahitaji muhimu”,alisisitiza Kongawadodo
Kwa kumalizia Diwani wa Kata ya Hombolo Bwawani Mheshimiwa Mathayo Ndahilo aliwataka wanakijiji wa Samaria kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali pindi inapohitajika ili kufanikisha adhma ya ujenzi wa kisima hicho.
AWALI:
Kituo cha Samari kilianza mwaka 1993 ambacho kipo umbali wa Kilometa Moja na nusu kutoka Hombolo mjini mkoani Dodoma, kwa sasa kinahudumia jumla ya watu wenye ukoma 52 wanaotoka katika Kaya 26 Kijijini hapo.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.