Saturday, May 26, 2018

TIMU YA SOKA YA NAMUNGO YAPATA WADHAMINI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema timu ya soka ya Namungo ya Wilaya ya Ruangwa imepata udhamini wa sh. milioni 150 katika msimu ujao wa ligi daraja la kwanza.

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, ametoa kauli hiyo jana (Ijumaa, Mei 25, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa wilaya na mkoa mara baada kukagua uwanja mpya unaojengwa katika kijiji cha Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

Amesema timu hiyo ambayo imepanda daraja msimu huu wa ligi, imefanikiwa kupata mdhamini mkubwa ambaye ni kampuni ya Haojue ya kutoka China inayouza pikipiki za aina ya SanLG.

“Bado tuko kwenye mazungumzo na kampuni ya Uranex, hivi sasa wako mbioni kukamilisha taratibu za udhamini, na wakikubali watakuwa wadhamini wetu namba mbili,” alisema.

Aliyataja makampuni na taasisi nyingine ambazo zimeshatoa udhamini kwa timu hiyo kuwa ni Ngureme Co. Ltd (madini), Lindi Jumbo Ltd (madini), Benki ya NMB, Halotel, CocaCola (ambao wametoa mipira 25 na jezi), Mzee Bakhresa, kampuni ya AZAM, kampuni ya Nazareth, Masoud Jaba na Gemini Exploring Ltd.

Alisema hivi sasa kocha wa timu hiyo anaendelea na usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao, na tayari wachezaji 17 wamekwishasajiliwa, na wengine 10 bado wanaendelea kufuatiliwa.

Waziri Mkuu aliishukuru kampuni ya Haojue kwa kukubali kuidhamini timu hiyo. “Tuna uhakika kwamba wana-Namungo hawatalala njaa wakiwa kambini,” alisema.

Kwa upande wake, mshauri wa kampuni ya Haojue hapa nchini, Bw. Martin Mbwana alisema wamekubali kuwa wadhamini wakuu kwa gharama ya sh. milioni 150 kwa mwaka na udhamini wao utajumuisha jezi na viatu vya wachezaji.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.