Friday, May 18, 2018

WADAU WA AFYA MOJA WAJIPANGA KUIOKOA TANZANIA NA MAGONJWA AMBUKIZI

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Prof. Faustin Kamuzora  akieleza umuhimu wa sekta za Afya kutekeleza Mpango mkakati wa Afya moja nchini, wakati wa kikao kazi cha wadau wa Afya  moja kilichokuwa kikijadili utekelezaji wa Mkakati huo, jijini Dodoma.

NA MWANDISHI WETU:

Dunia imekumwa na tishio kubwa la magonjwa ya kuambukiza yanayoweza kusambaa kwa muda mfupi, kusababisha madhara makubwa kwa binadamu, mifugo, wanyama pori na kuleta uharibifu wa mazingira. Tafiti zinabainisha kuwa kila mwaka huibuka magonjwa ambukizi mapya kati ya matano hadi Nane duniani. Hivyo inakadiriwa ifikapo mwaka 2030, dunia itakuwa na magonjwa ambukizi mapya 30.


Hayo yamebainishwa na wadau wa afya moja ambao ni kutoka sekta ya Afya ya binadamu, sekta ya mifugo, sekta ya afya ya wanyamapori na mazingira, walipokutana jijini Dodoma kujadili Utekelezaji wa Mpango mkakati wa Afya moja nchini, ambao umezinduliwa rasmi Februari mwaka huu na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim majaliwa.

Akiongea wakati wa kufungua kikao kazi hicho Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa, Faustin Kamuzora amefafanua kuwa Mpango Mkakati huo  unalenga kuimarisha mfumo wa Afya moja nchini, kwa kuimarisha juhudi na ushirikiano uliokuwepo wa sekta mbalimbali katika kuzuia, kujiandaa na kukabili magonjwa yanayoambukiza kuzingatia dhana ya Afya moja.

“Hatunabudi sekta zote kushirikiana katika kudhibiti magonjwa ambukizi kwakuwa sekta moja isipojidhatiti lazima binadamu ataathirika. Tutumie elimu na maarifa kwa pamoja katika kushughulikia tishio la magonjwa hayo kwa kuzitatua  changamoto za kiafya katika sekta za binadamu, wanyama, na mazingira” Amesema Prof. Kamuzora.

Wakichangia katika kikao kazi hicho wadau wa Afya moja wamebainisha kuwa mambo yanayochangia kutokea kwa magonjwa ambukizi mapya ni pamoja na ongezeko la watu duniani, mahitaji makubwa ya mazao ya wanyama hususani nyama, uharibifu wa mazingira pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya ardhi na shughuli za kilimo.

Aidha, wadau wa Afya moja, katika kikao hicho wamekubaliana kwa pamoja kutekeleza majukumu yaliyoainishwa katika mpango mkakati huo ili kuweza kukidhi kanuni za kitaifa, kikanda na kimataifa ambazo zinahitaji ushirikiano  wa sekta mbalimbali kwa kutumia dhana ya afya moja.

Kikao hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dawati la Uratibu wa Afya Moja, kwa washirki  kutoka  Wizara, Idara na Taasisi za serikali, wadau wa maendeleo nchini,  Vyuo vikuu  na sekta binafsi. Aidha kikao hicho kililenga  kuongeza msukumo na ufanisi katika utekelezaji wa  Mpango Mkakati wa Afya moja nchini.


Afya Moja ni dhana inayojumuisha sekta ya Afya ya binadamu, Mifugo, Wanyamapori na Mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri sekta hizo.
Mdau wa Afya Moja kutoka AFRIQUE ONE, Dkt. Coletha Mathew akieleza jinsi taasisi hiyo inavyofanya tafiti za kisayansi katika kutekeleza Mkakati wa  Afya Moja nchini wakati wa kikao kazi cha wadau wa Afya  moja cha kujadili utekelezaji wa Mkakati huo, jijini Dodoma.


Mdau wa Afya Moja kutoka OHCEA, Prof. Japhet Kilewo akieleza jinsi wanavyowajengea uwezo wanafunzi wa elimu ya juu katika kutekeleza Mkakati wa Afya Moja nchini wakati wa kikao kazi cha wadau wa Afya  moja cha kujadili utekelezaji wa Mkakati huo, jijini Dodoma.

Baadhi ya wadau wa Afya Moja kutoka wakiendelea kufuatilia  kikao kazi cha wadau wa Afya  moja kilichokuwa kikijadili utekelezaji wa Mkakati wa Afya Moja nchini, jijini Dodoma.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.