Monday, May 21, 2018

WAZIRI MKUU AZINDUA UMEME WA GRIDI LINDI, MTWARA

*Ataka Wakurugenzi wa Halmashauri wafikishe umeme shuleni, hospitalini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya kote nchini wahakikishe wanafikisha umeme kwenye vituo vya kutolea huduma za kijamii zikiwemo shule na hospitali.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Mei 21, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mikoa ya Lindi na Mtwara baada ya kuzindua kituo cha kuunganisha umeme wa gridi ya Taifa katika kijiji cha Mahumbika, wilaya ya Lindi mkoani Lindi.

"Wakati tukizindua miradi kama hii, niwasihi Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe kuwa umeme unapelekwa kwenye taasisi za kutolea huduma zikiwemo shule zote za msingi na sekondari. Wakurugenzi tekelezeni hilo," amesema.

"Tunataka umeme huu upelekwe kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati. Na kama kuna visima vya maji katika maeneo yenu, navyo pia vipelekewe umeme. Hatutaki kusikia wananchi wanakosa maji eti kwa sababu dizeli imekwisha, " amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema malengo ya Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli na Serikali yake ni kutaka Watanzania watumie umeme huo kukuza uchumi wao kupitia biashara za saluni, kuuza maji baridi au vinywaji baridi.

Amewataka wakazi wa mikoa hiyo washikamane kulinda miundombinu ya umeme ili iweze kuwa endelevu na isaidie vizazi vijavyo. "Kuna baadhi ya watu wanajihusisha na biashara ya vyuma chakavu, na wanang'oa vifaa ili wakauze bila kujali ni hasara gani wanasababisha. Ninawasihi wananchi wenzangu, kila Mtanzania awe mlinzi wa mwenzake kwenye miundombinu ya umeme. Ukiweza pita pale kwa wauzaji na uchungulie aina ya vifaa anavyouza kama ni vipya au ni chakavu kweli. Ukikuta kuna vifaa vyetu vya umeme vinauzwa huko, toa taarifa polisi naye atachukuliwa hatua kwa sababu sheria zipo,” amesema.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhara hiyo, Waziri wa Nishati,  Dk. Medard Kalemani alisema miezi mitatu iliyopita hapakuwa na nyaya wala nguzo za umeme kutoka Lindi kwenda Mtwara lakini mafundi wa TANESCO wamejitahidi na kuifanya kazi hiyo ndani ya muda mfupi.

"Lazima tuwapongeze vijana kwa sababu wamefanya kazi kubwa na nzuri na wala  hatujatumia washauri waelekezi (consultants). Ndani ya miezi mitatu, wamejenga laini yenye urefu wa km. 80 kutoka Mtwara hadi Mahumbika. Na kutoka hapa, watajenga laini yenye urefu wa km. 120 kwenda Ruangwa ambayo pia itaunganishwa kwenda Liwale na Nachingwea," alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi,  Bw. Erasto Zambi alisema tukio la uzinduzi wa mradi wa kuunganisha umeme wa gridi ya Taifa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni la kihistoria.

"Uzinduzi wa leo ni hatua kubwa ya maendeleo, kwani sasa hivi tukizungumza na wawekezaji tuna uhakika na nishati ya umeme. Nitumie fursa hii kuwakaribisha wawekezaji mkoani Lindi. Na huu ni uthibitisho wa Serikali kuamua kuondoa kero kwa Watanzania," alisema.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.