*Apokea wanachama kutoka CUF, CHADEMA na ACT
*Yumo aliyekuwa Katibu Mwenezi wa kata wa CHADEMA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea wanachama saba kutoka vyama vitatu vya upinzani ambao wameamua kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM) na wengine 82 kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao walikuwa wapiga debe.
Wanachama hao wamepokelewa leo mchana (Ijumaa, Mei 25, 2018) wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua uwanja mpya wa michezo unaojengwa katika kijiji cha Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Waziri Mkuu ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alipokea kadi nne za CUF, moja ya ACT na mbili za CHADEMA kutoka kwa wanachama hao saba kabla hajawakabidhi kadi za CCM. Wanachama hao saba waliokabidhiwa kadi mpya za CCM pamoja na wenzao 82, walikula kiapo cha uaminifu mbele ya Waziri Mkuu.
Shangwe zililipuka uwanjani hapo wakati aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA kata ya Nachingwea, Bw. Ismail Hamisi alipokabidhi kadi yake kwa Waziri Mkuu.
Akisoma risala kwa niaba ya wanachama wenzake walioamua kujiunga na CCM, mkazi wa Ruangwa mjini, Bw. Fred Mnimbo alisema wameamua kurudi kwa sababu yale waliyotarajia yafanyike upinzani hayaonekani.
“Tumegundua upinzani wa sasa ni maslahi binafsi na si wa kuwatumikia wananchi; kinachosemwa sicho kinachotendwa na wapinzani na pia tumeamua kuunga mkono juhudi anazofanya Rais John Pombe Magufuli,” alisema Bw. Mnimbo katika risala hiyo.
Alisema wameamua kuhamia CCM kwa sababu Serikali iliyopo madarakani kwa sasa inatekeleza mahitaji ya Watanzania kwa asilimia 90 na pia wanataka kumuunga mkono mbunge wao wakiwa katika chombo kimoja ili waijenge vizuri Ruangwa na Tanzania kwa ujumla.
“Tunataka kuunga mkono usimamizi mzuri wa rasilmali zetu hasa mazao ya korosho na ufuta kutokana na jinsi unavyoyasimamia kikamilifu hasa mikoa ya Kusini. Kaulimbiu ya Ruangwa kwa maendeleo inawezekana, imedhihirika kwa vitendo kwa sababu kila mmoja anaona kwamba Ruangwa ya jana si Ruangwa ya leo, maendeleo yanaonekana kwa mafanikio makubwa,” alisema huku akishangiliwa.
Akitoa utambulisho wa wanachama hao wapya, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Bw. Barnabas Essau alisema wanachama hao wameamua kujiunga na CCM kwa sababu wameridhishwa na utendaji wa Serikali ya awamu ya tano.
Novemba 5, mwaka jana, Waziri Mkuu alipokea wanachama 37 kutoka vyama vya CUF na CHADEMA kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mbekenyera, wilayani Ruangwa. Pia Desemba 29, 2017, alipokea wanachama 60 kutoka CUF kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Nkowe kata ya Nkowe, wilayani Ruangwa.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.