Thursday, May 10, 2018

SERIKALI YAKUSUDIA KUTAFUTA MBIA MWINGINE MRADI WA UDART

*Yasema haitosita kumuondoa mwendeshaji wa sasa 

SERIKALI imesema inakusudia kuongeza mtoa huduma mwingine katika uendeshaji wa  Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ambaye ataingiza mabasi yake na kutathmini ufanisi wa mbia wa sasa ili kuimarisha huduma ya usafiri Jijini Dar es salaam . 

Amesema iwapo itabainika kwamba mwendeshaji wa sasa  ana matatizo yaliyokithiri, Serikali haitasita kumuondoa na kumpa mwendeshaji mwingine kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa uhakika.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei  10, 2018) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Bw.Maulid Mtulia katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma.

Katika swali lake Bw. Mtulia alitaka kupata kauli ya Serikali juu ya uboreshaji wa wa mradi wa UDART unaotoa huduma ya usafirishaji wa abiria Jijini Dar Es Salaam ili kuweza kuwaondolea wananchi changamoto ya usafiri.

“Tunatafuta mbia mwingine aweze kuingiza mabasi yake kwenye mradi huu ili aweze kuongeza ushindani na nasi tupate kupata huduma bora kwa maana ya ushindani utaongeza  huduma bora zaidi,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ameongeza kuwawako wawekezaji wa ndani na nje ukiwemo Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar Es Salaam (UWADAR) ambao  wameonyesha nia na uwezo wa kutoa huduma hiyo na kuufanya mradi huo kutoa huduma kwa ubora unaotakiwa.

Katika hatua nyingineWaziri Mkuu, amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia vizuri suala la usafi wa mazingira katika maeneo yao la sivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Mheshimiwa Spika Kupitia Bunge lako tukufu, nawaagiza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi pamoja na Maafisa Afya wasimamie zoezi la usafi na kuboresha miundombinu yote na utawapima kupitia zoezi hili,” amesema.

Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Busega, Dkt. Raphael Chegeni aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kutatua tatizo la usafi wa mazingira pamoja na miundombinu hususani katika masoko hali ya kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinakusanya fedha nyingi bila kuboresha  maeneo na kukithiri kwa  uchafu.

Waziri Mkuu amesema suala la usafi limekuwa likifanyika kila jumamosi ya mwisho wa mwezi baada ya kuasisiwa na Rais Dkt. John Magufuli, hivyo ametumia fursa hiyo kuwaagiza watendaji hao wahakikishe maeneo yao yanakuwa safi na miundombinu inayoweza kutumika wakati wote.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.