Saturday, May 19, 2018

WAZIRI MKUU AAGIZA TOZO ZA KAHAWA ZIPITIWE UPYA


*Akerwa na utitiri wa tozo za zao hilo wilayani Karagwe
*Asema zinawekwa na vyama vya msingi kuwaumiza wakulima

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Warajis Wasaidizi wa Mikoa na Maafisa Ushirika wa Halmashauri za Wilaya nchini wakutane na wadau wa vyama vya msingi vya zao la kahawa na wapitie upya tozo zilizo kwenye zao hilo.

Amesema tozo nyingi haziko kisheria bali zinawekwa na vyama vya msingi na zimelenga kuwanyonya wakulima badala ya kuwasaidia kuinua vipato vyao.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Mei 19, 2018) wakati akizungumza na Warajis Wasaidizi wa Ushirika wa Mikoa 25 na Maafisa Ushirika wa Halmashauri za Wilaya 140 zinazolima mazao makuu ya biashara yaani kahawa, chai, tumbaku, pamba na korosho kwenye kikao alichokiitisha jijini Dodoma ili kujadili namna bora ya kuongeza uzalishaji wa mazao hayo na kufanya ufuatiliaji wa maagizo ambayo alikwishayatoa kwenye ziara zake mikoani.

Tangu mwaka jana, Waziri Mkuu ameshafanya vikao zaidi ya sita na wadau wa pamba, korosho, tumbaku na kahawa nchini ili kubaini namna bora ya kufufua mazao hayo makuu.

Akizungumzia kero ya tozo za mazao kwa wakulima, Waziri Mkuu alisema: “Kuna tozo nyingi zinazowekwa na vyama vya msingi na hazina uhalali wowote; tozo nyingine si za vyama vikuu, bali ni za AMCOS tu (vyama vya msingi),” alisema.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema: “Wakati napitia nakala za baadhi ya vyama vya zao la kahawa, nimekuta chama kimoja cha Karagwe kimeweka sh. bilioni tano zikiwa ni gharama za kukagua maghala na ili kufidia gharama hizi, mkulima anakatwa sh. 260 kwa kilo moja. Nimejumlisha makato ya tozo zote nimepata sh.1,600 kwa kilo.”

“Nikauliza bei ya kilo moja ya kahawa ni shilingi ngapi nikajibiwa ni dola 1.7 (sh.3,500) kwa kahawa aina ya Robusta na dola 2.7 (sh.5,500) kwa Arabica. Sasa kama mkulima analipwa sh. 3,500 kwa kilo moja halafu anakatwa sh. 1,600; hivi ataacha kupeleka kahawa yake Uganda kweli, na ninyi maafisa ushirika mpo tu mnaangalia makato yote hayo?” alihoji.

“Je mkulima atapata motisha gani ya kuendelea kulima zao hili? Hivi mnasubiri kupewa dokezo kwamba mna mamlaka ya kuzuia wizi na ubadhirifu unaofanyika kwa wakulima? Nendeni mkapitie upya hizi tozo, nendeni mkafanye kazi, nendeni mkawalinde wakulima,” alisisitiza.

“Nimegungua pia tozo hizi zimetofautiana kwa wilaya na mikoa; Kagera wana zao, Moshi wana zao, Ruvuma wana zao. Kuna tozo ya nyuzi, ya magunia, kuna mpaka tozo ya unyaufu; hivi kahawa ina unyaufu? Na inachukua miezi mingapi hadi kufikia kunyauka wakati ilishakobolewa na kukaushwa?” alihoji Waziri Mkuu.

Alitumia fursa hiyo kuwahimiza maafisa hao watekeleze maamuzi ya Serikali ya awamu ya tano juu ya kutumia mfumo wa ushirika na minada kununua mazao ambayo msimu wake wa mavuno umekaribia. “Sasa hivi pamba imeanza kuuzwa katika baadhi ya maeneo, na zao linalofuata ni kahawa. Lazima ununuzi ufuate mfumo wa ushirika. Nataka mkasimamie suala hili kwa umakini kabisa,” alisisitiza.

Aliwataka wakasimamie ipasavyo mifumo ya masoko ili kupambana na wanunuzi nje ya mifumo iliyokusudiwa. “Kwa mfano, Kagera wanunuzi wa kahawa wasio rasmi wanaitwa butura, Moshi wanaitwa katakichwa, kwenye korosho wanaitwa kangomba na kwenye tumbaku wanaitwa vishada. Ninawasihi msikubali kuwe na uonevu, dhuluma na wizi kwa wakulima wetu,” alisisitiza.

Pia aliwataka maafisa hao wahakikishe wanapata takwimu za maeneo yao ambazo zitaonesha kila wilaya ina vyama vya msingi vingapi, kila chama kina wanachama wangapi na wamelima ekari ngapi kwani itawasaidia kujua mahitaji yao iwe ni dawa, mbegu au mbolea.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kuanza na mazao matano makuu ya biashara ya kahawa, chai, tumbaku, pamba na korosho ili kuongeza usimamizi wa uzalishaji na masoko kwenye mazao hayo ambao ulishuka kutokana na changamoto mbalimbali.

Katika hatua nyingine, maafisa ushirika kutoka wilaya za Newala, Chunya, Kaliua, Sengerema, Babati, Sumbawanga, Uvinza na Mbinga waliopewa nafasi kutoa maoni yao, waliomba ushirika upewe hadhi ya idara au kitengo katika Halmashauri zote nchini ili kuendanana na kasi ya sasa; pia waliomba waongezewe watumishi na vitendea kazi vikiwemo kompyuta na usafiri.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini, Dk. Titus Kamani aliwataka maafisa hao wawe wabunifu na waondokane na utendaji wa mazoea ili wawasaidie wananchi kwa sababu ushirika ni silaha ya wanyonge na adui wa matajiri wanaowanyonya wakulima.

“Wananchi wanautaka sana ushirika kwa sababu wamechoka kuibiwa, wamepigika sana na bei za soko huria. Wana matumaini na ushirika mpya kwa sababu hakuna mkulima anayekataa malipo ya awamu ya pili,” alisema.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.