Saturday, June 1, 2019

AZAM FC YAUNGANA NA SIMBA KIMATAIFA

*Ni baada kuifunga Lipuli fainali za ASFC

TIMU ya Azam FC imefuzu michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika msimu ujao baada ya kuifunga Lipuli FC bao 1-0 kwenye fainali za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Mbali na kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika, timu ya Azam imeondoka na kitita cha sh. milioni 50, medani pamoja na kombe.

Fainali hizo zimefanyika leo (Jumamosi, Juni 1, 2019 katika uwanja wa Ilulu, Manispaa ya Lindi ambapo ushindi huo unaifanya Azam FC kuungana na Simba kuliwakirisha Taifa kwenye michezo ya Kimataifa itakayoanza Novemba mwaka huu.

Mshambuliaji wa Azam Obrey Chirwa ndio aliyeiwezesha timu yake ya Azam kuibuka na ushindi katika mchezo huo baada ya kufunga bao la ushindi katika kipindi cha pili.

Katika mchezo huo ulioshuhudiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, timu ya Lipuli FC iliyong’ara kwa kutawala mchezo kwenye kipindi cha kwanza, ilishindwa kutumia nafasi nyingi ilizozipata kuifunga Azam.

Mbali na timu ya Lipuli kuwa mshindi wa pili katika mashindano hayo, pia timu hiyo imetoa mchezaji bora wa mechi ya fainali, Paul Ngalema pamoja na mfungaji bora wa mashindano hayo Seif Rashid.

 (mwisho)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi kikombe cha Ubingwa wa Shirikisho la Azam (ASFC), nahodha wa Azam, Aggrey  Moris baada ya  Azam kuifunga Lipuli 1-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye uwnja wa Ilulu mjini Lindi Juni 1, 2019.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.