WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amewataka waislamu kote nchini waendeleze
utulivu, amani na uadilifu waliouonesha katika kipindi cha Mwezi Mtukufu
wa Ramadhani kwani kwa kufanya hivyo, watasaidia kukuza umoja wa
kitaifa, uchumi na kuboresha huduma za jamii.
Amesema
ni vema wakatambua kwamba uadilifu waliouonesha ndani ya Mwezi Mtukufu
wa Ramadhani ni silaha muhimu hususan katika kuimarisha maendeleo na
kudumisha haki, umoja, usawa, upendo na utulivu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Juni 5, 2019)kwenye Baraza la Eid El Fitri, lililofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Tanga Beach Resort jijini Tanga.“Nawashi sana kuyaenzi mema yote mliyoyafanya kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan’’.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amezipongeza taasisi za Kiislamu na imani nyingine ambazo
zimejenga shule ili kuchangia maendeleo ya elimu kitaifa lakini
amesisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongeza shule nyingine na vyuo zaidi
pamoja na kuziboresha zile zilizopo ili kusaidia jitihada za Serikali
katika kuboresha huduma za jamii nchini
Amesema
licha ya juhudi inazozichukua, Serikali peke yake haina uwezo wa
kueneza huduma za jamii kama vile elimu, afya na maji katika kila pembe
ya nchi hivyo, inapotokea taasisi za Kiislamu au madhehebu mengine
yakaweka mikakati ya kueneza huduma hizo, basi bila shaka Serikali ipo
tayari kuunga mkono juhudi hizo na kuchangia ufanisi wake.
Wakati huo huo,
ameitaka BAKWATA ichukue hatua za makusudi katika kuhakikisha huduma
nyingi za maendeleo na za kijamii zinaifikia kwenye mikoa mingi zaidi ya
pembezoni. “Huu ni wakati muafaka sasa wa kutafakari ni namna gani
Watanzania wa maeneo mengine nao watanufaika na uwepo wa huduma
mbalimbali kama vile elimu, afya na nyinginezo.“
Kwa upande wake,Mufti
na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally ametumia
fursa hiyo kuwataka waislam wote nchini wabadilike na waache mazoea ili
waweze kusonga mbele kielimu na kiuchumi.
Sheikh
Zubeir amesema ni vema kwa waislamu wakajiimarisha kiuchumi kwa sababu
kutawaondolea changamoto za kuendesha shughuli zao mbalimbali na hivyo
watakuwa wamejiletea maendeleo na kuboresha maisha yao.
Mbali
na wito huo pia amewataka waislamu wote wahakikishe wanatii
mamlaka yaliyo juu yao , viongozi waliopo madarakani wawe wa kiserikali
na wa kidini kama ilivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
[TAKUKURU], Diwani Athuman amesema ili nchi iweze kuendelea kuwa na
amani, utulivu na usalama watanzania wote hawana budi kuungana pamoja
katika kupiga vita vitendo vya rushwa.
"Rushwa
ni dhambi kubwa na hukumu yake mbele ya Mwenyezi Mungu ni moto kwa
sababu rushwa ni kipingamizi kikubwa cha maendeleo, hivyo tuungane
pamoja kupinga rushwa ndani ya nchi yetu kama Rais Dkt. John Magufuli
anavyotuongoza."
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.