Tanzania ikiwa ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa inaungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya kwa lengo la kuikumbusha jamii juu ya tatizo kubwa lilipo katika jamii yetu juu ya Biashara na Matumizi ya Dawa za hizo.
Kitaifa Maadhimisho haya kwa mwaka huu
yatafanyika jijini Tanga siku ya Jumatano tarehe 26 mwezi Juni, 2019 katika
viwanja vya Tangamano na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa George H.
Mkuchika (Mb).
Kauli mbiu ya Kimataifa ya
maadhimisho haya kwa mwaka huu inasema Waathirika
wa Dawa za Kulevya Wana Haki ya Kupata Huduma za Afya. Kwa
kuzingatia Kauli mbiu hii inakumbusha kuwa mapambano dhidi ya Tatizo la Dawa za
Kulevya yanahitaji mikakati mtambuka na jumuishi ikiwemo suala la tiba kwa
waathirika. Ni muhimu kwa Waathirika wa Dawa za Kulevya kupata tiba stahiki na
zilizothibitishwa kisayansi (evidence based practices) ili kuweza kupunguza
madhara ya dawa hizo kwa waraibu na jamii inayowazunguka.
Baada ya tiba hizo,
huduma endelevu za Stadi za Kazi pamoja na Ushauri Nasaha kuzingatiwa ili
kuwasaidia waathirika wasirudi kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Aidha,
mkakati huu unaenda sambamba na mkakati wa utoaji wa elimu kwa vijana ili
wasiingie kwenye matumizi ya Dawa za Kulevya pamoja na Udhibiti wa
wafanyabiashara wa Dawa hizo.
Maadhimisho haya ni fursa kwa umma wa
Watanzania kwa vile Tatizo la Dawa za Kulevya linaathiri
nchi yetu katika nyanja za kiafya, kijamii, kiuchumi pamoja na kutishia ulinzi
na usalama wa nchi yetu. Katika
maadhimisho haya Watanzania wataweza
kupata elimu na kukumbushwa kuwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya yana
athari kubwa kwa mtumiaji, kwa jamii na kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi
yetu.
Tatizo la dawa za kulevya husababisha
madhara kiafya ikiwa ni pamoja na kuchochea kuenea
kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI, virusi vya homa ya ini aina ya B na C,
Kifua Kikuu, magonjwa ya akili, pamoja na usugu wa tiba ya kifua kikuu na
UKIMWI. Aidha, baadhi ya dawa za kulevya husababisha matatizo ya uzazi ikiwemo
upungufu wa nguvu za kiume, kuharibika kwa mimba, kuzaliwa kwa watoto wenye
matatizo ya akili pamoja na kuenea kwa kansa mbalimbali kama vile kansa ya koo,
mapafu na mara nyingine husababisha vifo ghafla vya kutokana na dozi kuwa kubwa “overdose”.
Aidha Serikali imeendelea kusimamia utoaji tiba kwa
waathirika wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya
dawa hizo, na kufanikiwa kuongeza idadi ya waathirika wa dawa za kulevya katika
vituo vya tiba kutoka wagonjwa 2,400 mwaka 2015 hadi wagonjwa 7000 mwaka 2018.
Hali hii imeasaidia kupunguza maambukizi ya UKIMWI kwa waraibu wa dawa za
kulevya wanaojidunga kutoka 35% mwaka 2015 hadi 18.5%.
Pia, Serikali
inamtaka kila mwananchi kwa nafasi yake katika jamii kushirikiana na vyombo vya
dola kutoa taarifa endapo kutabainika kuwepo kwa matumizi na biashara ya dawa
za kulevya. Pamoja na hilo Serikali inatoa wito kwa viongozi wa dini kulikemea
suala la matumizi ya dawa za kulevya misikitikini na makanisani. Sambamba na
hilo, Serikali inawakumbusha Viongozi wa
dini zote kuwa wana nafasi kubwa katika
jamii ya kuhakikisha watoto, vijana pamoja na jamii yote kwa ujumla
wanapata mafunzo ya kuwajenga kiroho, kimwili na kisaikolojia ili wawe na tabia
njema katika jamii na mfano wa kuigwa kwa matendo mema.
Serikali inaikumbusha jamii kushiriki
kikamilifu katika kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, kujenga
malezi bora kwa watoto katika ngazi ya familia, na kuwapeleka kwenye matibabu
watumiaji wa dawa za kulevya. Vilevile, Serikali inasisitiza Jamii kuzitambua,
kuzienzi na kuziendeleza tamaduni zetu nzuri ili kuinusuru Wananchi wote hasa
vijana ambao ndo nguvu kazi ya taifa na matumizi ya dawa za kulevya.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.