Saturday, June 15, 2019

TUMIENI MASHABIKI KUJIJENGA KIUCHUMI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amevitaka vilabu vya soka nchini kutumia vema fursa ya kuwa na mashabiki wengi katika kuvifanya viweze kujitegemea kiuchumi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Juni 15, 2019) katika hafla ya kuchangia klabu ya Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.Ameichangia klabu hiyo sh. milioni 10.

“Natambua kwamba Yanga ni klabu kubwa na kongwe nchini ikiwemo Simba Sport Club ambazo ndizo zina wanachama na mashabiki wasiopungua milioni 20 au zaidi.” 

Hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuvitaka vilabu vya soka nchini kutafuta njia nzuri na endelevu ya kupata mapato ili kuendesha timu zao na kujiimarisha kiuchumi. 

Amesema kwamba, kuimarika kwa vilabu hivyo vyenye ushawishi mkubwa katika soka nchini ni muhimu kwa mustakabali wa soka la Taifa letu. 

Waziri Mkuu amesema kufanya vizuri kwa vilabu hivyo kuna uhusiano wa mkubwa na wa moja kwa moja na mafanikio ya timu ya soka ya Taifa.

“Nampongeza kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kwa kazi nzuri aliyoifanya msimu ulioisha na kuiwezesha timu ya Yanga kufanya vizuri ingawa haikupata ubingwa.” 

Pia, Waziri Mkuu amesema yeye ni mpenzi wa timu zote zinazoshinda na zinazoshindwa. “Kama kuna timu naipenda sana ni siri yangu, hata nyie hamuijui.”

Waziri Mkuu amesema soka ni mchezo maarufu na una wapenzi wengi duniani na hapa nchini na umejipambanua kwa fursa nyingi ikiwemo biashara, uwekezaji na ajira. 

Amesema Serikali imeendelea kusimamia maendeleo ya michezo, ukiwemo mchezo wa soka ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015-2020.

“Mhe. Rais Dkt. John Magufuli amekuwa akiungana na wanamichezo kuhamasisha kuendeleza michezo na anatamani kuona mkishinda hadi katika ngazi ya Afrika.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amezipongeza timu zote za soka zinazofanya vizuri katika ngazi mbalimbali. “Tumeshuhudia Polisi na Namungo FC zikipanda hadi ligi kuu.”

Ameipongeza timu ya Simba kuwa klabu bingwa, Azam kuwa bingwa wa FA, Serengeti boys na Twiga kuliwakilisha Taifa na Taifa Stars inashiriki AFCON – Misri.

“Kitendo cha Azam kushinda FA na Simba kushiriki vizuri AFCON sasa kumewezesha timu zetu mbili zaidi, Yanga na KMC kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya CAF.”

Kuhusu harambee ya Kubwa Kuliko, Waziri Mkuu amesema ni mwanzo mzuri kuelekea kwenye mabadiliko yatakayoiwezesha Yanga kujitegemea na kujiendesha bila kutarajia michango kama ilivyo sasa. 

Naye, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete amewataka wanachama wa Yanga warudishe hisia na mapenzi kwa timu yao kama ilivyo kwa timu ya Simba, pia wawe na ubunifu wa kutengeneza mfumo mzuri wa mapato.” Siku hizi Yanga imekuwa baridi sana, viongozi wa Yanga lazima mbadishe hali hii.”

Amesema viongozi wa sasa wa klabu ya Yanga chini ya Uwenyekiti wa Dkt. Mshindo Msolla ni wazuri na wanaujua mpira vizuri, hivyo watengeze mifumo mizuri itakayoinufaisha klabu. Wahakikishe wanawekeza kwenye timu ya watoto badala ya kuangalia wachezaji wa kutoka nje ya nchi pekee.

Amesema wasipowekeza kwenye timu ya watoto siku zote watakua mafahari wa kuwa na wachezaji kutoka nchi za nje jambo ambalo ni sawa na kuwafundishia wenzao. “Leo mnajisifia na akina Makambo, Kagere siku ikicheza timu ya Taifa inakuwaje. Oneni fahari ya kuwa na wachezaji wa ndani hivyo waendelezeni Tanzania kuna vijana wana vipaji.” 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Dkt. Mosolla amesema yeye pamoja na viongozi wenzake watahakikisha wanajenga umoja ndani ya klabu na kuipeleka jirani na wananchi kwa kufufua matawi na kuwa na wanachama wapya wengi.

Pia watawatumia wachezaji wa zamani katika kupata wanachama wengi na pia watakuwa na wiki ya klabu hiyo ambayo wataitumia kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kurudisha utaratibu wa kwenda mikoani baada ya ligi kuisha kwa ajili ya kutembelea wananchi na kujiongezea wsanachama.

Kuhusu suala la mabadiliko ya katiba amesema watalifanya kwa kufuata utaratibu wa kisheria. Pia Dkt. Msolla amesema uongozi wake utahakikisha unazingatia utawala bora na tayari wametoa matangazo ya nafasi za ajira.

Akizungumza kuhusu hali ya usajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu, amesema hadi sasa tayari wamekamilisha kwa asilimia 90 kuwasajili wachezaji wote aliowataka kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera kutoka nje ya nchi na wa ndani ya nchi.

Dkt. Msolla ametumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mkuu awasaidie ili Serikali iweze kuwapunguzia changamoto mbalimbali zinazoikabili klabu hiyo ya Yanga ikiwemo ya madeni.
Awali,Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa wa klabu ya Yanga, Anthony Mavunde, alisema kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 27 waliofanikisha kupatikana kwa fedha ambazo zimetumika katika kusajili wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Ajira na Vijana alisema walisambaza kadi kwa ajili ya kukusanya fedha za kuimarisha klabu yao ili iweze kujiendesha na kutatua changamoto za wachezaji.

Alisema mbali na kukusanya michango pia kamati yao imependekeza kufanyika kwa mabadiliko ya katiba ili kutengeneza mfumo mzuri utakaoisaidia timu hiyo kuweza kujiendesha na kuweka mfumo mzuri wa kutumia vifaa vya klabu kukuza uchumi.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la klabu ya Yanga na Mke wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Fatma Karume amewataka wananchi wasitumie vilabu vya soka kama njia ya kutaka kujipatia nafasi za kisiasa. Pia amewataka wanachama wampe ushirikiano Mwenyekiti wao mpya.

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alisema hakuna kipindi kigumu kilichompa tabu katika kuongoza wizara hiyo kama kipindi ambacho timu ya Yanga ilipokuwa katika mgogoro wa kiuongozi.

Pia, Dkt. Mwakyembe alionesha kutoridhishwa na upangwaji wa ratiba za michezo mbalimbali ya ligi kuu msimu uliopita, hivyo alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wapenzi wa soka nchini kwamba mambo hayo hayatajirudia tena katika msimu ujao.

(Mwisho)


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.